Mapato Halmashauri ya Rungwe yaongezeka hadi Sh8.6 bilioni

Rungwe. Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe iliyopo mkoani Mbeya imeongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani kutoka zaidi ya Sh4.5 bilioni mpaka Sh8.6 bilioni kutokana na vyanzo mbalimbali vya mapato.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera ameyasema hayo leo Juni 16, 2025 wakati akifungua kikao cha baraza maalumu la madiwani la kupitia na kupokea taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Homera amesema alipoteuliwa kushika wadhifa huo, halmashauri hiyo ilikuwa ikikusanya Sh4.5 bilioni, lakini sasa imeongeza umakini wa ushirikishwaji na kufikia Sh8.6 bilioni kwa kipindi cha miaka minne.

“Ni jambo la kujivunia, mmepiga hatua kubwa sana ya ukusanyaji mapato ya Serikali, jambo hilo linatokana na ushirikiano mkubwa baina ya yenu na Mkurugenzi Mtendaji, Renatus Mchau sambamba na watendaji wa kata na vijiji,” amesema.


Amesema ubunifu na usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo ni sababu iliyofanya CAG kuibua hoja 14 kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.

“Niwapongeze kwa kusimamia utekelezaji wa miradi ndio maana leo hamjampa kazi kubwa CAG, sasa niwatake hizo hoja zilizoibuliwa zijibiwe kwa kutekeleza miradi isiyokamilika kwa wakati,” amesema.

Mkaguzi wa nje wa hesabu za serikali za mitaa mkoani humo, Michael Maganga ameagiza watendaji wa Halmashauri ya Rungwe kujibu hoja zilizoibuliwa na kuongeza umakini wa ukusanyaji wa mapato na kutekeleza miradi iliyosuasua tangu mwaka 2010.

Miongoni mwa hoja hizo ni usimamizi usioridhisha na kukosekana kwa taarifa za ushuru wa mabango na wa huduma bila taarifa kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

“Nataka sababu za maeneo hayo kutosimamiwa kama sehemu ya ukusanyaji wa mapato ya ndani na kutekeleza maagizo ya kamati ya kudumu ya Bunge Tamisemi,” amesema.

Maganga ametaja hoja nyingine ni pamoja na Sh393 milioni  zilizoelekezwa kutekeleza miradi ya shule ya sekondari na msingi Bulyaga sambamba na ujenzi wa zahanati ya Simike, wilayani humo.

Akijibu hoja zilizoibuliwa na CAG, Ofisa Mipango Wilaya ya Rungwe, Belton Galigu amesema miradi hiyo itaendelea kutekelezwa kulingana na bajeti.

Kuhusu ushuru wa huduma bila kuwa na taarifa ya TRA, amesema watalifanyia kazi ikiwepo kufanya tathimini ya mabango na kuingiza kwenye takwimu za vyanzo vya mapato.

Related Posts