Kutanuka kwa mito kunavyokwamisha usimamizi wa sheria -2

Dar/Arusha. Aprili 27, 2019 aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba alieleza ugumu wa kubomoa nyumba zilizojengwa ndani ya mita 60 kutoka kingo za mito, hususani maeneo ya mijini.

Alisema si rahisi kuondoa nyumba hizo kwa kuwa awali zilijengwa nje ya eneo hilo, lakini mabadiliko ya tabianchi, hasa kutanuka kwa mito kumezifanya zionekane sasa zipo ndani ya mita 60 kutoka kwenye kingo za mito.

Athari hizi za mabadiliko ya tabianchi mijini zinaonekana kutokana na kutanuka mito kama vile Ngarenaro mkoani Arusha na Gide, jijini Dar es Salaam, hali inayosababisha mafuriko yanayoathiri makazi ya watu ambayo awali yalikuwa nje ya eneo hatarishi.

Kwa mujibu wa mtandao wa UN-Habitat 2020, miji mingi ya Afrika, Dar es Salaam ukiwamo ipo hatarini kutokana na ukuaji holela wa miji na miundombinu duni ya kukabili majanga kama mafuriko.


Hali hii inathibitisha kuwa utekelezaji wa sheria bila kuzingatia athari za mabadiliko ya tabianchi unaweza kusababisha migogoro ya kijamii na kiuchumi.

Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004, kifungu cha 57(1), inapiga marufuku shughuli yoyote ya binadamu kufanyika ndani ya mita 60 kutoka kingo za mto, ziwa, bahari au eneo lolote la maji, isipokuwa kwa kibali maalumu kutoka kwa mkurugenzi wa mazingira na baada ya kufanyika tathmini ya athari kwa mazingira (EIA).

Ingawa sheria ipo wazi, hali halisi kwenye maeneo kadhaa mijini inaonyesha changamoto kubwa katika utekelezaji wake. Kwa mfano, katika Jiji la Dar es Salaam, kuna nyumba takribani 1,590 zilizojengwa ndani ya mita 60 kutoka kingo za Mto Gide, mbali na nyumba zaidi ya 50 ambazo tayari zimeshasombwa na maji ya mto huo.

Jijini Arusha, kwenye Mto Ngarenaro nyumba zaidi ya 300 zipo ndani ya eneo la mita 60 kutoka kwenye kingo zake na katika hatari ya kusombwa, kama ilivyotokea kwa nyingine zaidi ya 20 zilizopotea licha ya kujengwa nje ya eneo hilo kihistoria.

Kwa mujibu wa wananchi na viongozi wa maeneo haya, uwepo wa nyumba hizo hauwezi kuonekana kama ukiukwaji wa sheria, bali ni matokeo ya mabadiliko ya tabianchi yaliyosababisha mito kusogelea makazi ya watu.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Darajani, Kata ya Ngarenaro jijini Arusha, Hemedi Ally anasema Mto Ngarenaro awali ulikuwa mfereji mdogo na nyumba zilijengwa mbali na mkondo wake, lakini sasa umetanuka na kubadili mwelekeo kiasi cha kuingia kwenye makazi ya watu.

“Sasa unaposema uwahamishe wananchi kwa sababu wamejenga kinyume cha sheria, unakosea kwa sababu mto ndiyo umewafuata. Hili ni jambo gumu, hatuoni cha kufanya,” anasema Ally.


Anasema nyumba takribani 300 zipo ndani ya mita 60 kwenye mto huo, na nyingine zaidi ya 20 zimeshasombwa na maji.

“Hapa utamlaumu mwananchi kwa kumuonea, alijenga kwenye eneo sahihi mto umemfuata, afanyeje?” anahoji.

Hali kama hiyo inawakumba wananchi wanaoishi pembezoni mwa Mto Gide jijini Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mgundini, Said Kitogo anasema nyumba hizo hazikujengwa ndani ya mita 60 kihistoria, bali mto ndiyo umehamia maeneo hayo.

“Nyumba zimefuatwa, si kwamba zilijengwa ndani ya mita 60. Asiyejua historia atasema serikali ya mtaa ilikuwa wapi wakati nyumba zinajengwa, lakini mto umefuata nyumba,” anasisitiza.

Kitogo anasema Mto Gide wa miaka 20 iliyopita si sawa na wa sasa kwa kuwa umetanuka na hata kubadili njia yake.

“Mto Gide umetanuka na umefuata nyumba. Zipo zilizobomoka, nyingine zipo hatarini. Si kosa la wananchi,” anasema.

Kauli iliyotolewa na Makamba inayofanana na za viongozi hao wa mitaa, inaungwa mkono na Dk Samwel Gwamaka, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), aliyesema ni vigumu kutekeleza sheria hiyo katika mazingira ya sasa ya miji na mito.

Anasema sheria ilishaanza kukiukwa zamani na hivyo kusababisha shughuli za binadamu kuathiri mito kiasi cha kuhamia kwenye makazi ya watu.

“Nyumba iliyojengwa nje ya mita 60 kwa sasa utaikuta imefuatwa na mto, hivyo kuwa ndani ya eneo lililokatazwa kisheria,” anasema.

Dk Gwamaka anasema kwa sasa ukizungumza kuhusu watu wasifanye shughuli ndani ya mita 60 katika mikoa ya Dar es Salaam au Arusha, sheria haitabadilika, lakini hali halisi haikubaliani na mazingira hayo.

“Kuna ugumu wa kutekeleza sheria,” anasema.

Kauli hiyo inaungwa mkono na Kaimu Mkurugenzi wa Usimamizi wa Sheria wa NEMC, Jamal Baruti anayesema mara nyingi kutanuka kwa mito ni matokeo ya majanga ya asili.

“Ni changamoto kwa sababu unapomkuta mtu alikuwa mbali na mita 60 na tunajua kweli mito inatanuka, kwa hiyo inatoa ugumu wa kutekeleza sheria,” anasema.

Baruti anasema sheria ilikuja mwaka 2014, kipindi ambacho mito tayari ilikuwa imeshatanuka na baadhi ya watu walikuwa wanaishi ndani ya maeneo hayo. Kwa msingi huo, anasema hali hiyo imekuwa changamoto kwa sababu kutanuka kwa mito hakukusababishwa na wanadamu moja kwa moja, bali ni majanga ya asili.

Dk Gwamaka anapendekeza hatua mbadala kwa ajili ya kulinda mito na makazi ya watu. Anatoa mfano wa hatua zilizochukuliwa katika Mto Ng’ombe jijini Dar es Salaam, ambao kingo zake zilijengwa ili kuzuia kutanuka zaidi au kuhama njia.

Anashauri katika mito mingine kama Gide na Ngarenaro, jamii kwa kushirikiana na serikali za mitaa na kamati za mazingira wajenge kingo za mito ili kuzuia athari zaidi. Anabainisha si lazima kutumia zege, bali hata mawe makubwa yaliyofungwa kwa waya yanaweza kutumika kuimarisha kingo.

Wakati hatua hizi zikichukuliwa, anashauri waziri mwenye dhamana aweke mwongozo wa kitaifa juu ya jinsi ya kuendeleza maeneo ndani ya mita 60 ya kingo za mito mijini, baada ya kuhakikisha kuwa mito imejengewa kingo imara.

“Waziri anapaswa kutengeneza mwongozo wa kufanya maendelezo ndani ya mita 60 ya kingo ambazo zimeshajengewa. Hii itasaidia mito kufuata njia zake na hata malalamiko ya mto umefuata nyumba hayatakuwepo,” anasema.

Sambamba na hilo, anahimiza kila mwananchi kutambua kuwa usimamizi na utunzaji wa mazingira ni jukumu la pamoja, wala si la mtu mmoja au taasisi moja.

Akizungumzia hatua zinazochukuliwa, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk Immaculate Semesi anasema mafanikio ya utekelezaji wa sheria yatapatikana endapo kutakuwa na ushirikiano wa kweli kati ya taasisi zote zinazohusika, zikiwamo zinazohusika na mipango miji na utoaji wa vibali vya ujenzi.

Baruti anasema NEMC kwa kushirikiana na mamlaka nyingine, wameanza kuchukua hatua kadhaa, kama usafi wa mito na ujenzi wa kingo ili kuzuia kutanuka zaidi.

“Tunachokifanya kwa sasa ni kujaribu kuweka mazingira ya mito sawa, ilimradi isiendelee kutanuka. Tunafanya usafi kwa kushirikiana na mamlaka zinazotajwa kisheria, pia tunajenga kingo,” anasema.

Anasema ndiyo maana mpaka sasa NEMC haijaanza kubomoa wala kuwahamisha wananchi walioko ndani ya mita 60, kwa kuwa wanatambua athari hizo zimesababishwa na mabadiliko ya tabianchi, si makosa ya moja kwa moja ya wananchi.

Habari hii imeandaliwa kwa udhamini wa Gates Foundation

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.

Related Posts