Wamisri wamedhihirisha kuwa Kiswahili kinakubalika na kwamba kinaweza kupenya kila kona ya dunia.
Baadhi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Ain Shams, wamebuni tamthilia ya kwanza inayotumia Kiswahili, ikiwa ni sehemu ya kuipaisha lugha hiyo inayokua kwa kasi duniani.
Tamthiliya hiyo, iliyopewa jina la Ndoto Bandia, ina vipindi vinne na imeongozwa na mhadhiri na mtalaam wa Kiswahili katika chuo hicho Dkt Shimaa Tarek, ambaye kwa muda sasa ameendelea kujitokeza kama kielelezo cha wanazuoni wa nje wanaojitolea kueneza lugha ya Kiswahili katika nchi zisizozungumza lugha hiyo kiasili.
Akizungumza na Mwananchi, Dk Shimaa ambaye unaweza kumweleza kama balozi mwema wa Kiswahili nchini Misri, anasema, tamthilia hiyo iliyochezwa na wanafunzi wake, inaeleza masaibu ya vijana wa Kimisri wanaokimbia nchi yao na kwenda ughaibuni kutafuta maisha.
” Pia tamthilia hii inaonesha sura ya Misri ughaibuni na maisha ya watu wa Misri na ustaarabu wa Kifarao na maana ya urafiki,’’ anasema Dk Shimaa na kuongeza kuwa tamthilia hiyo ni mwanzo wa kazi za Kiswahili wanazotarajia kuzifanya siku zijazo.
Aidha, anasema kazi hiyo ya kisanaa haikuwalenga watazamaji pekee, bali ni mradi wa kitaaluma wenye dhamira ya kuonyesha uwezo wa Kiswahili katika kuwasilisha hoja za kijamii, kifalsafa na kihistoria.
“Tutafanya kazi nyingi sana kwa lugha ya kiswahili nchini Misri na tutachangia kukuza lugha adhimu kama lugha ya Kiswahili ndani ya Misri na nje. Tumeonyesha kuwa Kiswahili kinaweza kutumika kuelezea hisia, migogoro ya kijamii na matumaini ya watu wa kawaida,” anasema Dkt Shimaa.
Tamthiliya hiyo imehusisha jumla ya wanafunzi 41 kutoka idara ya Kiswahili ya chuo hicho, huku wataalamu wa sanaa nchini humo wakisifu ubunifu na matumizi ya lahaja mbalimbali za Kiswahili ndani ya kazi hiyo
Akizungumzia mwamko wa Wamisri kujifunza Kiswahili anasema wengi wao wanaupenda kujifunza wakiwamo wanafunzi na kwamba idadi ya wanaojifunza lugha hiyo ikazidi kuongezeka.
‘’Wamisri wanapenda sana kujifunza lugha ya Kiswahili, idadi ya wanafunzi wanaongezeka. Pia, sio wanafunzi tu wanajifunza lugha ya Kiswahili bali watu wa kawaida wanajifunza lugha hiyo kwa ajili ya kazi, utalii, safari na mengineyo,’’ anaeleza.
Anasema kwa sasa kuna vyuo vinne… vinavyotoa kozi za Kiswahili nchini humo. Anavitaja vyuo hivyo kuwa ni Al Azhar, Cairo, Ain Shams na Aswan.
Kwa yeye mwenyewe, anasema alipata msukumo wa kujifunza lugha hiyo kwa kuwa ni lugha maarufu barani Afrika, hasa ukanda wa Afrika Mashariki.
‘’ Pia, ni lugha rahisi sana kwa sababu maneno mengi nadhani asilimia 30 au zaidi yana asili kutoka lugha ya Kiarabu na lugha nyingine, jambo hilo linasaidia wanafunzi kujua zaidi kuhusu lugha ya Kiswahili,’’ anasema.
Ana wito upi kwa Watanzania kuhusu Kiswahili? Dk Shimaa anaeleza:’’ Watanzania waithamini lugha ya Kiswahili, kwa sababu ni lugha muhimu na kubwa na watu wengi kutoka madola mbalimbali wanajaribu kujifunza lugha hiyo adhimu.’’
Esraa Ahmed, mmoja wa washiriki wa tamthilia hiyo, anajivunia Kiswahili lugha ambayo awali hakuwa anaijua. Anasema lugha hiyo ni ya kipekee na anshukuru kuongeza luga moja katika akiba za lugha anazojua.
Akizungumzia tamthilia hiyo anasema: ‘’Nilipokuwa nikiigiza, nilihisi kama nafanya jambo jipya na la kipekee. Nilipata ujuzi wa kuzungumza na kusimama mbele ya watu wengi. Zaidi ya hayo, timu yote ya kazi ilikuwa marafiki zangu.Na ushawishi wa Dk Shimaa aliyekuwa akituhamasisha daima kuwa tunaweza kuigiza, kulikuwa na hali ya furaha na hamasa ya kuigiza kwa lugha hiyo.’’
Kwa upande wake, Ebrahim El- Saqa anasema: ‘’ Hakika nilipoingia kitivo hiki, nilichagua Kiswahili; kwani nimesikia kwamba kina nafasi nyingi na watu wengi ndani ya nchi mbalimbali wanaongea lugha hii. Kwa hiyo sikusita kuchukua nafasi hiyo ya kujifunza lugha hii adhimu ya Kiswahili. Ninashukuru kwamba naongea Kiswahili sasa hivi kwa ubora, hakika ni fahari tupu.’’
Kuhusu ushiriki katika tamthilia, anaeleza: ‘’ ‘’Nilijihisi kama nina jukumu kubwa sana. Kucheza kama baba kulinifanya nifikirie juu ya wajibu wa mzazi katika familia kwa kuzingatia upendo, ulinzi, na uamuzi mgumu. Ilikuwa ni nafasi ya kipekee iliyoniwezesha kuonyesha hisia za ndani na kuelewa maisha kutoka kwa mtazamo wa baba na majukumu ya wazazi, hasa katika kuunda uamuzi na kutawala watoto wao.’’