G7 yaiunga mkono Israel, Iran yadhibitiwa

Washington, Marekani. Nchi wanachama wa Kundi la G7 zimetoa taarifa rasmi usiku wa kuamkia leo, zikiunga mkono haki ya Israel kujilinda, huku zikitaja Iran kuwa chanzo kikuu cha machafuko na misukosuko katika ukanda wa Mashariki ya Kati.

Kwa mujibu wa Reuters, viongozi wa G7 wamehimiza kupunguzwa kwa mvutano kwa ujumla katika eneo hilo linalozidi kugubikwa na mzozo.

Vita ya anga kati ya Israel na Iran iliyoanza Ijumaa baada ya Israel kufanya mashambulizi ya ghafla dhidi ya maeneo ya Iran, imezua taharuki kubwa katika ukanda ambao tayari ulikuwa katika hali tete tangu Israel ilipoanzisha mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Ukanda wa Gaza Oktoba 2023.

“Tunasimamia msimamo kuwa Israel ina haki ya kujilinda. Tunarudia kusisitiza kuunga mkono usalama wa Israel,” ilisomeka sehemu ya taarifa ya viongozi wa G7.

Taarifa hiyo pia ilieleza: “Iran ndiyo chanzo kikuu cha machafuko ya kikanda na ugaidi,” na kuongeza kuwa, “msimamo wetu uko wazi kuwa Iran haipaswi kamwe kumiliki silaha za nyuklia.”

Israel ilifanya shambulio dhidi ya Iran Ijumaa iliyopita ikisema ilikuwa ni hatua ya kujikinga kabla ya hatari, kwa lengo la kuzuia Tehran kuendelea na mpango wa kutengeneza silaha za nyuklia.

Tangu wakati huo, mahasimu hao wawili wa Mashariki ya Kati wamekuwa wakibadilishana mashambulizi makali. Maofisa wa Iran wameripoti vifo vya zaidi ya watu 220, wengi wao wakiwa raia, huku Israel ikithibitisha vifo vya raia 24.

Iran, kwa upande wake, imekana kuwa na nia ya kutengeneza silaha za nyuklia, ikisisitiza kuwa ina haki ya kuendeleza teknolojia ya nyuklia kwa matumizi ya amani, ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa madini ya urani, kwa mujibu wa Mkataba wa Kuzuia Ueneaji wa Silaha za Nyuklia (NPT) ambao ni mwanachama wake.

Israel, ambayo haijasaini mkataba wa NPT, ndiyo nchi pekee ya Mashariki ya Kati inayotuhumiwa kwa kiasi kikubwa kuwa na silaha za nyuklia, ingawa haijawahi kuthibitisha wala kukanusha taarifa hizo.

Rais wa Marekani, Donald Trump, alipanga kuondoka mapema katika mkutano wa G7 uliofanyika nchini Canada ili kurejea Washington kufuatilia kwa karibu hali inayoendelea Mashariki ya Kati.

Hadi sasa, Marekani imeendelea kudai kuwa haijajihusisha moja kwa moja na mashambulizi ya Israel dhidi ya Iran, ingawa Trump alikiri Ijumaa kuwa Marekani ilikuwa na taarifa mapema juu ya mashambulizi hayo, akisema ni hatua nzuri sana.

Washington imeitahadharisha Tehran kutojaribu kushambulia masilahi au watu wa Marekani waliopo katika eneo hilo.

“Tunasihi kwamba suluhisho la mgogoro wa Iran liwe kichocheo cha kupungua kwa vita na uhasama katika ukanda mzima wa Mashariki ya Kati, likijumuisha pia usitishaji wa mapigano Gaza,” taarifa ya G7 ilieleza, na kuongeza kuwa mataifa hayo yako tayari kushirikiana katika kulinda utulivu wa masoko ya nishati duniani.

Katika hali ya taharuki inayoendelea, shambulizi la Israel liliilenga shirika la utangazaji la taifa la Iran siku ya Jumatatu. Wakati huohuo, Trump aliandika katika ukurasa wake wa mitandao ya kijamii akisema: “Kila mtu anatakiwa kuondoka Tehran mara moja,”

Kwa upande mwingine, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, alizungumza kwa njia ya simu na mawaziri wenzake wa Uingereza, Ufaransa na Umoja wa Ulaya kujadili hali ya vita kati ya Israel na Iran.

Related Posts