Rais Samia Suluhu Hassan ametoa pole za rambirambi kwa familia vifo vya vijana wanne waliopoteza maisha wakielekea wilayani Meatu mkoani Simiyu kusikiliza mkutano wa mkuu huyo wa nchi.
Ingawa Rais Samia hakuzungumza kwa undani kuhusu vifo hivyo, lakini amesema ajali hiyo imejeruhi watu kadhaa.
Rais Samia ameeleza hayo Jumanne Juni 17, 2025 akihutubia wananchi wa Meatu, ambapo mwanzoni mwa hotuba yake alitumia nafasi kutoa salamu za pole kwa familia zilizopoteza wapendwa wao.

“Nitoe pole nyingi sana…Tumepoteza vijana wetu wanne na wengine kadhaa wameumia katika usafiri kuja kwenye mkutano huu. Nitoe pole sana kwa WanaMeatu,”amesema Rais Samia.
Rais Samia yupo katika ziara ya siku tano mkoani Simiyu kwa lengo la kuzungumza na wananchi ili kujua changamoto zinazowakabili sambamba na kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Baada ya ziara ya Mkoa wa Simiyu kukamilika, mkuu huyo wa nchi ataelekea Mwanza kuzindua daraja JP Magufuli (zamani Kigongo –Busisi) ambalo ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 100.