Dar es Salaam. Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam, Jumanne Muliro ameeleza sababu za jeshi hilo kuzuia mkutano wa Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), John Heche na wanahabari.
Mkutano huo ulipangwa kufanyika leo Jumanne Juni 17, 2025 saa tano asubuhi katika Hoteli ya Seashells Millennium, iliyopo Makumbusho jijini Dar es Salaam.
Muliro amesema Jeshi la Polisi limesimamia sheria kama ambavyo mamlaka zingine za dola zilivyoagiza, hivyo si sahihi kwa watu au kundi fulani kwenda kinyume.
Heche ndiye alitarajiwa kuwa mzungumzaji mkuu katika mkutano huo uliopangwa kufanyika saa 5: 00 asubuhi, lakini hadi saa 4:45 asubuhi hakuwa amefika kwenye hoteli iliyopangwa, ndipo polisi walifika na kuwaamuru waandishi wa habari waondoke na waandaaji wasitishe shughuli hiyo.
Akizungumza na Mwananchi baadaye, Kamanda Muliro amesema: “Tunachokifanya ni kusimamia sheria, sasa kama unadharau mamlaka zingine watu watakwenda wapi? Wakati mwingine tunawakumbusha, si umeona tumemkubusha (Brenda Rupia, mkurugenzi wa mawasiliano na uenezi Chadema).”
“Tulikwenda kuangalia anataka kufanya nini (Heche) ambacho ameshaelekezwa na Mahakama, sisi ni wasimamizi wa sheria na si jambo jingine lolote. Tunasimamia sheria iliyoelekezwa pia na mamlaka fulani kwa usifanye kitu fulani basi usifanye,” amesema.
Kamanda Muliro amesisitiza polisi ni wasimamizi wa sheria na mamlaka za kisheria zikielekeza jambo lisifanyike basi halifanyiki, au lifanyike basi linafanyika.
“Mamlaka zikielekeza sisi wasimamizi, sasa ukijitoa ufahamu, tunakukumbusha kwamba mamlaka za kisheria zimesema jambo hili. Hii ndio maana ya kufuata utawala wa sheria, vinginevyo basi hakuna haja ya mahakama kuwepo, kama kundi fulani linakiuka mhimili huo,” amesema Kamanda Muliro.
Juni 10, 2025 Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, iliamuru chama hicho kusitisha shughuli za siasa na matumizi ya mali zake hadi kesi ya msingi inayohusu mgawanyo wa rasilimali za chama itakaposikilizwa.
Uamuzi huo ulitolewa na Jaji Hamidu Mwanga kufuatia kesi iliyofunguliwa na wanachama wa Chadema, akiwemo aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti- Zanzibar, Said Issa Mohamed na wengine wawili, ambayo usikilizwaji wake utaanza Juni 24, 2025.
Wakati waandishi wakiwa tayari wamekusanyika wanamsubiri Heche katika ukumbi wa uliopo ghorofa ya tano, ndipo akafika Brenda Rupia ambaye ni mkurugenzi wa mawasiliano na uenezi wa Chadema, akawa anabadilishana mawazo baadhi wanahabari kisha akaketi pembeni mwa meza kuu.
Ghafla wakaingia maofisa watatu wa Polisi, mmoja akiwa amevaa sare, wakajitambulisha wanatoka Kinondoni na Kanda Maalumu Dar es Salaam, kisha wakauliza nani muhusika wa mkutano huo:
Askari Polisi 1: Nani kiongozi wa hili jambo?
Hawakujibiwa, kukawa kimyaa.
Askari Polisi 1: Nani muhusika wa hili jambo?
Ndipo Brenda akasimama na kujibu: Ni mimi.
Askari Polisi 1: Unafanya mkutano kama nani?
Askari Polisi 1: Humjui kama hamtakiwi kufanya mnachokifanya?
Breda: Nafanya kama Brenda
Askari Polisi 1: Kwa taarifa za uhakika, hapa kuna mkutano wa Chadema uliotangazwa toka jana, ambao hauruhusiwi kufanyika kutokana na amri ya Mahakama iliyotolewa.
Askari Polisi 1: Anyway, iwe ni Brenda au Chadema, sitisheni mara moja.
Brenda: Sioni kama ninachokifanya ni kosa kisheria.
Askari Polisi 2: Iwe ni wewe au Chadema sitisheni mara moja kinachoendelea.
Brenda: Kwani ni lazima nisitishe mbele yenu, nipeni japo muda nizungumze na niliowaalika.
Askari Polisi 1: Sio jambo la kutaka muda tena, sitisheni sasa hivi.
Askari Polisi 2: Hili sio ombi, ni amri na waandishi si mpo hapa, hakuna mkutano wala jambo litakaloendelea, naomba mtoke nje ya ukumbi.
Baada ya muda wanahabari wakatoka nje ma ukumbi kushuka chini ambapo walikuta magari mawili ya polisi aina ya Defender yenye askari polisi waliovaa kiraia na sare.
Licha ya amri hiyo, Brenda na makada wa wengine wa Chadema walikuwa bado kwenye viunga vya hoteli, kabla ya kuwataka waondoke hata nje ya hoteli.
Hadi makada hao wanaondoka, Polisi waliendelea kuzunguka eneo hilo wakiimarisha kuhakikisha mkutano huo haufanyiki.
Heche hakupatikana kuzungumzia tukio hilo baada ya simu yake kuita mara kadhaa bila kupokewa.