Mwanza. Ukiacha sifa ya kuwa daraja refu zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, Daraja la JP Magufuli ni matumaini mapya ya kurahisishwa kwa shughuli za usafiri na usafirishaji kwa wakazi wengi wa visiwa vya Ziwa Victoria.
Wakati wakazi wa Kigongo na Busisi wakifurahia kuepukana na adha ya kutumia muda mrefu kuvuka kutoka eneo moja kwenda lingine, wananchi wa visiwa vya Kome na Ukerewe wanatazama kukamilika kwa daraja hilo kuwa mwisho wa maumivu ya miaka mingi ya kukosa vivuko.
Kwa muda mrefu, visiwa hivyo vimekuwa na uhaba wa vivuko, hali inayosababisha ugumu wa kupatikana kwa huduma mbalimbali.
Wakati mwingine, hali huwa ngumu kwa wanafunzi wanaolazimika kutumia mitumbwi kwenda na kurudi shuleni.
Matumaini ya uhakika ya usafiri kwa visiwa hivyo, yanatokana na kile kilichoelezwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, kuwa vivuko vilivyokuwa vinatumika katika eneo lilipo daraja la JP Magufuli, havitahitajika tena, hivyo vitahamishiwa Kome na Ukerewe.
Katika mahojiano na Mwananchi Digital, Mtanda anaeleza kukamilika kwa daraja hilo, kunaenda sambamba na mpango wa kuboresha upatikanaji wa vivuko katika maeneo ya mbalimbali kama Ukerewe, Kome na Sengerema.
“Vivuko vilivyokuwa vikihudumu Kigongo-Busisi sasa vitapelekwa maeneo yenye uhitaji mkubwa zaidi. Hii ni fursa ya kipekee kwa wananchi wa visiwani walioteseka kwa miaka mingi,” anasema Mtanda.
Kwa mujibu wa Mtanda, Mkoa wa Mwanza unamiliki jumla ya vivuko 11 kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa) na tayari Serikali ina mkakati wa kuvigawa upya kwa kuzingatia mahitaji halisi ya wananchi.
“Kwa mfano, kivuko cha Kome kipo katika hali mbaya sana. Tumekubaliana kupeleka huko kimojawapo kati ya vivuko vilivyokuwa Kigongo-Busisi. Pia, kingine kitaelekezwa Sengerema na Ukerewe,” anasema.
Uamuzi huo umewafurahisha wananchi wa maeneo hayo, “Sikuwahi kufikiria siku hii ingefika,” anasema Christina Yona, mke na mama wa watoto watano kutoka kijiji cha Bwiro, Ukerewe, baada ya taarifa kuwa, vivuko hivyo vitapelekwa katika maeneo yao.
Anasema: “Tumepoteza wajawazito na wagonjwa njiani kwenda hospitalini. Ikiwa kivuko kingine kitaongezwa katika njia yetu, basi kwa baadhi yetu hiyo ni tofauti kati ya uhai na kifo,” anaeleza.
Kwa upande wa Hamisi Sungu, mkulima mwenye umri wa miaka 60 kutoka Kisiwa cha Kome, taarifa ya kupelekwa kivuko katika eneo hilo ni njema kwake.
“Kwa miaka mingi tulipaza sauti na hazikusikika. Boti tuliyonayo sasa ni hatari kwa sababu imechoka kupitiliza. Tunashukuru Serikali kwa kulifikiria hili hatimaye,” anaeleza.
Kwa wananchi wa Ukerewe, Kome na Irugwa, daraja hilo halihusiani tu na saruji au vyuma. Ni ishara ya hadhi yao kama raia wa taifa hili.
“Hata kama hatulivuki kwa miguu, kuwepo kwake kumetufanya nasi tujihisi kuwa sehemu ya nchi hii,” anasema Mwanaidi Mbwana, mfanyabiashara kutoka Irugwa mkoani Mwanza.
Katika mahojiano na Mwananchi, Mtanda anasema kwa sasa, ujenzi wa vivuko vipya vinne unaendelea kwa gharama ya Sh28 bilioni na vitapelekwa katika maeneo yenye changamoto zaidi ya usafiri majini.
Kabla ya kuwepo kwa daraja hilo, safari ya kuvuka Kigongo hadi Busisi ilikuwa ya saa mbili ikiwajumuisha foleni na kusubiri kivuko.
Lakini sasa, anasema inachukua dakika tano. Muda uliookolewa ni mtaji wa kiuchumi kwa watu waliokuwa wakipoteza saa kadhaa barabarani badala ya kuyatumia katika uzalishaji.
“Haikuwa tu Sh400 za nauli ilikuwa ni saa zilizopotea. Maelfu ya watu walipoteza uchumi kila siku. Hilo linakwenda kubadilika,” anasema.
Sambamba na hilo, anasema soko kubwa la kisasa linaendelea kujengwa jijini Mwanza kwa thamani ya Sh123 bilioni, linalotarajiwa kuwa mithiri ya lile la Kariakoo na hivi karibuni wataanzisha biashara ya saa 24.
Daraja hilo pia linaiunganisha Mwanza na mkoa ya Geita na maeneo yake kama Katoro na Sengerema hivyo kuwa chachu ya biashara na usafirishaji wa mazao, bidhaa na huduma.
“Daraja hili ni mwanzo tu. Mwanza itakuwa kitovu cha biashara za majini. Ziwa Victoria halitakuwa tena eneo la mateso, bali fursa,” anasema.
Ujenzi wa daraja hilo uliasisiwa na Rais wa awamu ya tano, John Magufuli na alifariki dunia likiwa na asilimia 24.6, kisha Rais Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani aliendeleza ujenzi wake hadi linakamilika.
Daraja la JP Magufuli lina urefu wa kilometa 3.2, ikiwa ndilo refu kuliko yote ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na lina upana wa mita 28.45 na barabara unganishi zenye urefu wa kilomita 1.66.
Daraja hilo lina njia mbili za magari zenye upana wa mita saba kila upande na njia za waenda kwa miguu kila upande yenye upana wa mita 2.5 na maegesho ya dharura yenye upana wa mita 2.5 kila upande.
Hili ndilo daraja lenye upenyo wa mita 120 ikiwa ni mkubwa zaidi ya madaraja yote nchini.
Kijiografia, daraja hilo liko katika ushoroba wa Ziwa Victoria unaoanzia kuanzia mpaka wa Sirari Wilaya ya Tarime nchini Tanzania na mpaka wa Isibani County ya Migori nchini Kenya hadi katika mipaka ya Mutukula Wilaya ya Misenyi mkoani Kagera inayopakana na nchi jirani ya Uganda.