TLS yatangaza kiama ofisi zinazotoa huduma ya sheria bila mawakili

 Dar es Salaam. Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) imetangaza kuwafungia na kuwafuta mawakili ambao wanatoza malipo chini ya kiwango kilichoweka kisheria.

TLS kupitia kamati ya malipo ya mawakili na mapambano dhidi ya vishoka, imetangaza kiama cha vishoka na wenye ofisi zinazotoa huduma za kisheria bila uwepo wa mawakili.

“Utakuta tu huko mtaani kuna kiofisi kimeandikwa tunatoa huduma za kisheria, ukifuatilia kina muhuri, anayetoa huduma hiyo si wakili, aidha amepewa tu muhuri na wakili au vinginevyo, hawa tunakwenda kula nao sahani moja,” amesema mwenyekiti wa kamati hiyo,

Sweetbeart Nkuba leo Juni 17, 2025 jijini Dar es Salaam.

Amesema wakishirikiana na Jeshi la Polisi, wanaanza msako mkali jijini Dar es Salaam kuanzia kesho Juni 18, 2025 katika kampeni maalumu ya kutokomeza vishoka, itakayoanzia Dar es Salaam na Kisha kuhamia kwenye kanda nyingine kote nchini.

“Kuna ofisini huko mtaani zinajitangaza kutoa huduma ya kisheria, lakini hazina mawakili, utakuta ni mtu tu aidha amepewa muhuri na wakili au vinginevyo anafanya kazi hiyo, jambo ambalo ni kosa kisheria,” amesema.

“Hii inadhoofisha taaluma ya uwakili, lazima tuwakamate wote ili hatua zingine dhidi ya zifuatwe na kutokomeza kabisa watu hawa kwenye taaluma,” amesema Nkuba.

Mbali na kundi hilo, Nkuba amesema tasnia hiyo imeingiliwa na vishoka ambao wanatoa huduma za kisheria wakati si mawakili.

“Huko nyuma tulikuwa tukiwasaka, lakini katika kampeni hii tunakwenda kuwatokomeza ni sisi na wao, wao na sisi,” amesisitiza.

Amesema mwananchi anapomtumia kishoka au wakili ambaye hajasajiliwa, kiapo au mkataba atakaouingia wa kisheria kupitia wakili huyo utakuwa ni batili.

“Mahakama imeweka utaratibu rafiki wa kumjua wakili halisi ni yupi kwa ku-Google kwa kuandika neno mjue wakili na kuingiza jina la wakili unayetaka kumtumia katika kiapo au mkataba wako ili kuona kama ni halali au la.

Amesema ikitokea mwananchi akamtumia kishoka au wakili ambaye hajasajiliwa, changamoto atakayokutana nayo ni kuwa kiapo au mkataba aliouingia utakuwa batili kwa mujibu wa sheria.

Nkuba pia amegusia mawakili ambao wanatoza pesa kutoa huduma ya kisheria chini ya kiwango kilichowekwa.

Amesema wakili anatoza malipo kulingana na kiwango kilichowekwa kisheria katika malipo ya viapo au mikataba mbalimbali.

“Wapo mawakili wanaotoza kiwango kidogo cha malipo ili kuvutia wateja, hawa wanakwenda kinyume na sheria kwani viwango hivi vilipangwa na kila malipo yana kiwango chake na viliwekwa kisheria  ili kulinda hadhi ya taaluma na kuepusha ushindani haramu wa mawakili,” amesema.

Amesema wakili atakayebainika kutoza malipo kinyume cha sheria iliyowekwa atasimamishwa au kufutwa kwenye orodha ya mawakili.

“Mfano ni mtu ananunua ardhi kwa Sh100 milioni, anamlipa dalali asilimia 10, lakini wakili anayetunza nyaraka anamlipa Sh20,000 au Sh50,000, hiki sio kiwango kilichowekwa kisheria,” amesema.

Amesema kisheria kwa kiwango cha pesa chini ya Sh10 milioni, tozo ya wakili ni asilimia sita au Sh3 milioni.

“Kwa kiwango cha Sh100 milioni tozo ya wakili ni asilimia tatu au Sh6 milioni.”

“Wananchi waepuke kushawishiwa kupewa huduma za kisheria na kwa bei ya chini, kwani inaweza kupelekea viapo au mikataba waliyoingia kubadilishwa,” amesema.

Related Posts