Dodoma. Serikali imewataka wataalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kutumia ujuzi wao kuunganisha mifumo ya utoaji huduma, ikisisitiza kuwa huo ndio mwelekeo sahihi kwa sasa katika kuboresha utendaji na utoaji huduma kwa Watanzania.
Agizo hilo limetolewa leo Jumanne, Juni 17, 2025, na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, wakati akizindua Wiki ya Utumishi wa Umma ambayo imeanza leo na itahitimishwa Juni 23, 2025.
Maadhimisho ya mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu isemayo: “Himiza matumizi ya mifumo ya kidijiti ili kuongeza upatikanaji wa taarifa na kuchagiza uwajibikaji.”
Simbachawene amesema kuunganisha mifumo ya Tehama kutasaidia kuongeza ufanisi na kuondoa urasimu, hivyo kuongeza imani ya wananchi kwa Serikali kwa sababu kero zao zitashughulikiwa kwa haraka na uhakika. Amesisitiza kuwa mifumo hiyo pia inasaidia viongozi kufuatilia moja kwa moja huduma zinazotolewa na kubaini maeneo yenye changamoto na hatua stahiki kuchukuliwa.
“Kwa mfano mfumo wa e-Mrejesho, kila hatua inayoendelea tunaiona. Na kwa kuzingatia agizo la Mheshimiwa Rais (Samia Suluhu Hassan), ninaagiza taasisi zote kuunganishwa kwenye mifumo ya pamoja kwa ajili ya kuleta mageuzi makubwa ya utoaji huduma kwa wananchi,” amesema Simbachawene.
Aidha, amewataka watumishi wa umma kutumia wiki hiyo kama fursa ya kutafakari kuhusu huduma wanazotoa na kama wanawatendea haki wananchi, sambamba na kutoa elimu juu ya huduma mbalimbali zinazopatikana serikalini.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Juma Mkomi amesema jumla ya wizara 23 kati ya 26 zinashiriki kwenye maadhimisho hayo. Ameeleza kuwa lengo la maadhimisho ni kutambua mchango wa watumishi wa umma, kuwahamasisha, kuwapa motisha na kuwaandaa kukabiliana na changamoto za kazi zao kwa lengo la kuchochea maendeleo ya Taifa.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Renatus Msangira amesema maadhimisho haya yanatoa fursa ya kuwapa wananchi taarifa sahihi kuhusu huduma wanazotoa. Amebainisha kuwa hadi sasa karibu vijiji vyote nchini vimeunganishwa na umeme, na kwa sasa juhudi zimeelekezwa katika kuunganisha vitongoji, huku wakitumia wiki hiyo kusikiliza maoni na mahitaji ya wananchi.
Msangira ameongeza kwa sasa kipaumbele kingine ni kampeni ya matumizi ya nishati safi ya kupikia, ambayo ni miongoni mwa ajenda muhimu kufuatia maelekezo ya Rais Samia.