Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimemtaka Jaji Hamidu Mwanga wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam ajitoe kwenye kesi inayohusiana na chama hicho, wakidai hawana imani naye.
Kimesema sababu za kumkataa Jaji Mwanga ni kuendesha shauri hilo, upande mmoja baada ya wakili wa Chadema, Jebra Kambole kujitoa, ilitakiwa mahakama hiyo kuahirisha kesi hiyo, ili walalamikiwa kupata muda wa kutafuta wakili mwingine.
Sababu nyingine ni historia ya Jaji Mwanga alikotoka kabla ya kushika wadhifa ujaji.
Kesi hiyo imefunguliwa na Said Issa Mohamed, Makamu Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho Zanzibar na wenzake wawili, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu, ambao ni wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema kutokea Zanzibar.
Wadaiwa katika kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Mwanga ni Bodi ya Wadhamini wa Chadema, ikiwa mdaiwa wa kwanza na Katibu Mkuu wa Chadema (John Mnyika), akiwa mdaiwa wa pili.
Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), John Heche ameeleza hayo wakati akizungumza na Watanzania kwa mtandao leo Juni 17, 2025 baada ya mkutano wake na wanahabari uliopangwa kufanyika Hoteli Seashells Millenium Tower kuzuiwa na polisi waliosema wanatekeleza sheria kama ambavyo mhimili mwingine umeagiza.
“Jaji Mwanga alisema Jebra (Kambole) si wakili wa chama, hivyo akaamu kesi isikilizwe upande mmoja na kutoa uamuzi ambao…Msingi wa mahakama ni haki ya asili ambayo mtu anapatiwa ili kusikilizwa.
“Sasa baada ya wakili kujitoa chama hakikuwa na wakili, Jaji alipaswa kuahirisha ili tupatiwe tarehe nyingine na atuombe kupeleka wakili kwa lengo la kupata uwakilishi katika kesi. Katika mazingira ya kawaida Jaji alifanya uamuzi pasipo kuzingatia jambo kubwa kama hili,”amesema Heche.
Heche amesema kitendo cha Jaji Mwanga kuendelea kusikiliza kesi hiyo, pasipo kuwapo kwa Bodi ya Wadhamini na Kaimu Katibu mkuu wa Chadema (John Mnyika), hakikuwa sawa.
“Sababu ya pili inatokana historia ya Jaji Mwanga aliyeteuliwa akitokea Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) na Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) ambazo msimamo wa Chadema mara zote tunazikosoa utendaji na muundo wake.
“Katika mazingira hayo kesi inayohusu Chadema anapangiwa Jaji anatoka katika taasisi tunazozilalamikia hatuoni kama tunatendewa haki. Kiukweli hatujatendewa haki, tunamuona na ana mgongano wa kimaslahi kutokana sababu hizo tunamuomba Jaji Mwanga ajitoe kusikiliza kesi yetu,”amesema Heche.
Juni 10 Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam ilizuia kwa muda shughuli zote za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), katibu mkuu, mawakala na wafuasi wa chama hicho kushiriki kwa namna yoyote shuguli zote za kisiasa hadi pale kesi ya msingi itakaposikilizwa.
Kwa mujibu wa Heche, zipo taratibu za kisheria zinazoendelea kuhusu shauri hilo, ikiwemo kukusudia kuomba mapitio upya ya hukumu ya Juni 10, 2025 kwa madai amri zilizotolewa hazina msingi wa haki.
Heche amewaelekeza viongozi na wanachama wa chama hicho kuendelea na shughuli za ujenzi wa Chadema, pasipo kutumia rasilimali za chama, akisema amri ya mahakama inawahusu katibu mkuu na bodi ya wadhamini.
“Hivi sasa chama kipo katika programu ya kuziba mapengo (viongozi waliohama), vikao hivi viendelee na kazi hizi zikamilike kama ilivyopangwa. Pia chama kinawaelekeza viongozi wote kuwa wakati tukisubiria wanasheria wetu hatua za msingi, rasilimali za chama zisitumike, wakati hatua hizi za kisheria zikiendelea,”
“Viongozi wengine wote na wanachama wajitolee na rasilimali zao binafsio kufanya shughuli za kisiasa ili kukamilisha programu za chama zilizotakiwa kukamilishwa. Chama kinaelekeza viongozi wengine kujihusisha katika shughuli za kijamii hasa kuchangia damu, kutembelea vituo vye uhitaji, kuwapa faraja wagonjwa na kujitolea kufanya usafi ndani ya siku 30,” amesema Heche.
Makamu mwenyekiti huyo, ameagiza kuwa matukio hayo yote yaratibiwe na viongozi kwa ushirikiano na wanachama, akisema shughuli hizo zina dumisha umoja, upendo na mshikamano kwa Watanzania.
“Uongozi wa Chadema upo, Chama hakitatetereka, mnavyotuunga mkono ndio unawaowatisha…Msitetereke wala kubabaika tupo kwenye ukweli, hii vita ya kuhakikisha rasilimali za Taifa zinatumikja kubadilisha maisha yenu,” amesema.