Dar es Salaam. Zikiwa zimepita siku 42 tangu kutekwa kwa mwanaharakati Mdude Nyagali, familia yake imeiomba Serikali pamoja na vyombo vya dola kusaidia kupatikana kwa mpendwa wao, huku ikisisitiza inaamini bado yuko hai.
Imesema iko tayari kushirikiana kwa njia yoyote ile na Serikali na vyombo vya dola kuhakikisha anapatikana, kwa kuwa waliomchukua ni binadamu na hivyo inawezekana akapatikana.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne Juni 17, 2025 nyumbani kwake, Sije Mbugi ambaye ni mke wa Mdude, amesema mateso na sintofahamu kuhusu alipo mumewe, vinaitesa familia.
“Naumia zaidi ninapowaona wanangu wakiishi kwa hofu huku wakimkumbuka baba yao. Kila siku huwa tunadhani tutapata taarifa rasmi kumuhusu, lakini hakuna,” amesimulia mama huyo huku akibubujikwa machozi.
Mdude aliripotiwa kutekwa nyumbani kwake Mei 2, 2025 na watu wasiojulikana waliodai ni askari polisi na tangu siku hiyo, hajulikani alipo.
Licha ya jitihada za kumsaka kufanywa na vyombo vya dola na watu mblimbali, bado haijafahamika ni nani waliomchukua.
Kutokana na tukio hilo, vyama vya siasa hususan Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), viongozi wa dini, wanaharakati wa haki za binadamu na wadau wengine wameendelea kulaani tukio hilo.
Wote kwa pamoja wameiomba Serikali kuchukua hatua za dhati ili kuhakikisha mwanaharakati huyo anapatikana na haki inatendeka.
Akisimulia kwa ya kwanza namna tukio lilivyotokea, Sije amesema walikuwa wamelala wakashtushwa na sauti ya watu waliokuwa wakifungua geti la nyumba yao.
Anasema alimuamsha mumewe ili akaangalie kinachoendelea.
Kwa mujibu wa Sije, watu hao waliovunja geti, kisha wakagonga mlango kwa nguvu ukavunjika, wakaingia ndani wakiwa na silaha zenye ncha kali.
“Walipofika ndani walisema wanamtaka Mdude. Walimvuta kutoka chumbani, nikawa napiga kelele za kuomba msaada, lakini hatukupata msaada wowote, labda kwa sababu ilikuwa usiku sana, ilikuwa saa 8,” amesimulia Sije.
Amesema hakuweza kuwahesabu watu hao kwa sababu walikuwa wengi, baadhi yao walimpiga sana Mdude kabla ya kumbeba na kutoka naye nje, huku mmoja akisalia ndani akimtishia yeye (mke) kwa silaha.
“Mdude alipigwa na kuvutwa hadi nje akiwa anatokwa na damu nyingi. Kabla hajachukuliwa, aliniambia nibaki ndani kwa sababu nilikuwa nimembeba mtoto, akasisitiza itajulikana tu kilichotokea,” ameeleza.
Kwa sasa, anasema anaishi kwa hofu na hakuweza kurudi katika nyumba hiyo kutokana na kumbukumbu za tukio hilo.
Amesema tangu siku ya tukio hilo, hajawahi kurudi nyumbani hapo na leo walipofika kwa ajili ya kuifanyia usafi tu nyumba hiyo.
Amesema kwa sasa pamoja na wanawe, wanapitia changamoto kubwa ikiwamo ya malezi ya watoto wao watatu.
Hata hivyo, Sije anasema hachoki kumuombea mumewe kwa Mungu huku akiamini ipo siku atarejea akiwa hai.
“Naipigia magoti Serikali na mamlaka zote, zisaidie kumpata mume wangu. Watoto wake bado ni wadogo sana, wanamhitaji,” amesema kwa sauti ya majonzi.
Baba mlezi wa Mdude, Enock Mbalwa (71), ameeleza historia ya Mdude tangu utoto wake, akisema alizaliwa mwaka 1987 na kulelewa naye baada ya mama yake kufariki dunia akiwa bado mdogo.
Mbalwa amesema alimlea kijijini Itaka (sasa Itewe), wilayani Mbozi mkoani Songwe hadi alipomaliza darasa la saba.
Kwa mujibu wa Mbalwa, Mdude alianza kujihusisha na harakati za kisiasa akiwa kijana, akivutiwa na maandiko ya ukosoaji wa sera na elimu kwa jamii.
“Sikumkataza kwa kuwa hata mimi nilikuwa Chadema tangu 1995, ingawa baba yangu alikuwa kada wa CCM. Niliona anafuata nyayo zangu,” amesema mzee huyo.
Amesema baada ya kujiimarisha kwenye harakati, Mdude alianza kujulikana zaidi lakini pia alipitia changamoto nyingi kutokana na harakati zake hizo.
“Mara ya mwisho nilizungumza naye Novemba 2024. Tulipanga mambo ya kifamilia lakini Mei 2 nikasikia taarifa ambazo hadi leo hazijaniingia akilini,” amesimulia mzee huyo.
Hivyo, ameiomba Serikali na hasa Rais Samia Suluhu Hassan, kuingilia kati suala hilo kwa dharura.
“Naomba Rais atusaidie kumpata kijana huyu ambaye si tu mtoto wangu, bali ni baba wa watoto watatu wanaomtegemea,” amesema Mbalwa.
Kwa upande wake, mdogo wa Mdude, aliyejitambulisha kwa jina la Hodito Mbalwa, amesema alizungumza na kaka yake mara ya mwisho Aprili 30, wakipanga kukutana Mei 5 kwa masuala ya kifamilia.
“Lakini kabla tarehe hiyo haijafika, nilipokea taarifa kutoka kwa rafiki yake kuwa amevamiwa. Baadaye kiongozi mmoja wa Chadema alinipigia simu akisema twende Mbeya kuona kilichotokea,” amesema.
Hodito amesema walipofika nyumbani kwa Mdude walikuta mazingira ya kutisha, damu zikiwa zimetapakaa ndani ya nyumba hadi eneo lilikokuwa limeegeshwa gari lililombeba.
“Kwa sasa tupo tayari kushirikiana kwa namna yoyote na Serikali kuhakikisha tunampata ndugu yetu. Hili jambo haliwezi kufanywa na familia pekee,” amesema.
Mwananchi pia imezungumza na mjomba wa Mdude, anayeitwa Willy Mtafya, ambaye amesema familia inaendelea na maombi katika maeneo mbalimbali ya ibada kumuombea arejee salama.
“Ibada zinaendelea kila mara tukimuombea apatikane akiwa salama. Lakini pia tunaomba kama kweli anashikiliwa kwa kosa lolote, basi sheria ifuate mkondo wake. Afikishwe mahakamani kama mtu mwingine yeyote, sisi familia tupo tayari kwa lolote,” amesema Mtafya.
Kwa upande wake, Halima Nyagali ambaye ni dada wa Mdude, amesema mdogo wake alikuwa mhimili wa familia hiyo, na hicho kilichotokea ni pigo kubwa.
Amesema kabla ya tukio hilo, Mdude hakuwa kwenye mgogoro wowote wa wazi na mtu yeyote, wala hakukuwa na taarifa za kudaiwa.
“Hatukuwahi kusikia akitishia au kutishiwa na mtu yeyote. Alikuwa mtu wa amani na msaada mkubwa kwetu sote. Tunaomba Serikali na Jeshi la Polisi watusaidie kumpata. Tuko tayari kushirikiana kwa namna yoyote kuhakikisha anapatikana,” amesema Halima.
Mdude alipanga nyumba eneo la Iwambi ikiwa ndani ya uzio ulio na nyumba sita, kila moja ikijitegemea.
Nyumba yake ilikuwa ya kwanza kushoto baada ya kuingia getini, ikiwa na mlango wa sebuleni na mwingine wa chumbani. Kwa ujumla, eneo hilo lina utulivu na usalama wa wastani, na mwingiliano kati ya wakazi si mkubwa.
Tangu kutokea kwa tukio hilo, mke wa Mdude aliondoka nyumbani hapo ikielezwa ilikuwa ni kwa ajili ya usalama wake na kwenda kuishi kwa ndugu wa mumewe.
Hata hivyo, Juni 15 alirejea akiwa na wifi yake Halima kufanya usafi, ndipo waandishi walifika pamoja nao na kushuhudia damu zilizoganda zikiwa bado katika baadhi ya maeneo ya nyumba hiyo.
Mmoja wa majirani ambaye hakutaka kutajwa jina, amesema hakusikia wala kushuhudia tukio hilo usiku huo, hadi taarifa ziliposambaa asubuhi yake.
“Niliamka nikasikia Mdude amevamiwa usiku, ilinishangaza sana kwa sababu namfahamu kama mtu wa harakati tu, siyo mtu wa ugomvi,” amesema jirani huyo.
Mwananchi limemtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamini Kuzaga kujua uchunguzi umefikia wapi, lakini simu iliita bila majibu.
Hata hivyo, katika taarifa yake ya Kamanda Kuzaga alisema uchunguzi ulikuwa unaendelea huku akilitenga jeshi hilo na madai kuwa waliohusika ni askari polisi.