Dar es Salaam. Mfanyabiashara Wilson Elias, baada ya kutaka kukatishwa ndoto yake ya kuwania Urais wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa baadaye mwaka huu kwa tiketi ya Chama Cha Tanzania Labour Party (TLP), hatimaye ameibukia Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) kusaka nafasi hiyo.
Mei 26, 2025 Wilson alijikuta nje ya mashindano baada kushika nafasi ya pili kwenye mchakato wa ndani wa kutafuta mpeperusha bendera wa TLP katika nafasi hiyo akipata kura 47 ikiwa ni nyuma ya kura tano alizoibuka nazo Yustas Rwamugira aliyepata kura 52 huku Neema Nyerere aliyeshika mkia akipata kura sita.
Rwamugira mabaye ni Katibu Mkuu wa TLP, alitangazwa mshindi katika mchakato huo, licha ya washindani wake kulalamikia mchakato wenyewe hakuwa huru na haki kiasi cha kutoa ushindani uliosawa na kukubalika kidemokrasia.
Wilson ametua ADC na kesho anatarajiwa kukabidhiwa fomu tayari kwa kuchuana na mtia nia mwenzake, Mutamwega Mgaywa aliyewahi kuwa mbunge wa Mwibara mkoani Mara (1995-2005) kwa tiketi ya TLP aliyechukua fomu ya kuomba ridhaa hiyo tangu Mei 23, 2025.
Wawili hao wataingia kwenye mkutano mkuu wa chama hicho unaotarajiwa kufanyika Juni 22, 2025 unaotarajiwa kufanyika Ubungo Plaza ambapo wajumbe wa chama hicho watafanya uamuzi wa kuchaguliwa Wilson au Mgaywa.
Wilson anayefanya biashara zake nje ya nchi ikiwemo Namibia na Botswana amezungumza na Mwananchi, leo, Juni 17, 2025 na kusema ameshafanya mazungumza na uongozi wa ADC, wamemkaribisha kwa mikono miwili.
“Tayari mambo yameisha naenda kusaka ndoto yangu ya kusaka Urais wa Tanzania kupitia ADC, nimeshaongea nao na leo nilikuwa nao kwenye kikao cha ndani na kesho nitachukua fomu na kurejesha Jumamosi ya juma hili ,” amesema Wilson.
Amesema ndoto yake ni kutaka kuwatumikia watanzania ili waishi maisha ya furaha kama anavyoona wengine wanavyofaidi katika mataifa anayopita kufanya shughuli zake za kibiashara kwa kutumia raslimali zao.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa ADC, Hamad Aziz amesema Wilson ni mwanachama wao ingawa hajakubali kama kesho anaenda kuchukua fomu ya kuwania Urais.
“Kesho kuna mtu anakuja kuchukua fomu ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania siwezi kukutajia ninani ila jua hivyo itakuwa suprize na muda nitakuambia,”amesema Aziz.
Aziz amesema dirisha la kuchukua na kurejesha fomu bado liko wazi na litafungwa rasmi Juni 21 siku moja kabla ya kuingia kwenye mkutano mkuu wa kumpata mpeperusha bendera ya chama hicho.