Miili ya wanandoa ilivyoagwa Dar, kuzikwa kesho Mwanga

Dar es Salaam. Mamia ya waombolezaji wamejitokeza kushiriki safari ya mwisho hapa duniani ya wanandoa Antony Ngaboli (46) na Anna Amiri (39) katika Kanisa Katoliki, Parokia ya Yohana Mbatizaji Bonyokwa, jijini Dar es Salaam.

Wanandoa hao walikutwa wamefariki dunia usiku wa kuamkia Juni 12, 2025 chumbani mwao Tabata Bonyokwa Gk, Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam huku miili yao ikiwa na majeraha sehemu mbalimbali.

Waombolezaji hao waliojaa ndani na nje ya kanisa hilo, walikuwa na simulizi za kila mmoja jinsi alivyowafahamu marehemu hao. Huku swali lililokuwa likiulizwa na wengi ‘ni nani amewaua’ kwa nini amewaua na familia nani ataiangalia.

Familia na ndugu wa marehemu Antony Ngaboli (46) na mkewe Anna Amiri (39) wakitoa heshima ya mwisho kwa marehemu, katika Kanisa Katoliki Parokia ya Yohana Mbatizaji  Bonyokwa, jijini Dar es Salaam. Picha na Michael Matemanga



Wawili hao walioishi pamoja zaidi ya miaka 20, walikuwa wakijishughulisha na biashara mbalimbali, wameacha watoto watano kati yao watatu wa kiume na wawili wa kike.

Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro akizungumzia tukio hilo amesema uchunguzi unaendelea.

Leo Jumanne, Juni 17, 2025, shughuli ya kuaga miili hiyo imefanyika, imeanza asubuhi nyumbani kwao huku familia na majirani wakiiaga kisha kuhamishiwa kanisani.

Baada ya hapo, ikasafirishwa kwenda Kijiji cha Ngulu Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro kwa mazishi yatakayofanyika kesho Jumatano.

Ibada ya kuwaaga marehemu hao imeongozwa na Paroko wa Parokia hiyo, Padri Jeremia Msaki ambaye kwenye mahubiri yake amesema marehemu hao walikuwa waumini wazuri waliokuwa wakishiriki shughuli za kanisa.

“Kama parokia tutawakumbuka kwa namna walivyokuwa wanajitolea kwa ajili ya kanisa,” amesema.

Pia, amegusia wiki tatu zilizopita wawili hao walimfuata na kueleza nia yao ya kutaka kufunga ndoa rasmi ya kikatoliki hivi karibuni.

“Walinieleza nia hiyo lakini kwa bahati mbaya na mapenzi ya Mungu hawakufanikiwa kulitimiza,” amesema huku nyuso za simanzi zikionekana kwa waombolezaji.

Padri Msaki amewataka waumini na watu wote waliojitokeza msibani kujikumbusha kuwa zawadi ni uhai kutoka kwa Mungu.

Amewasisitiza kuhakikisha wanaitumia zawadi vyema vizuri kwa kuishi na watu vizuri.

“Maisha tunayoishi ni zawadi kutoka kwa Mungu, tuoneshe shukrani kwake na tumuombe atuwezeshe kuishi maisha yanayompendeza,” amesema Padri Msaki.

Akizungumza kwa niaba ya familia, Nuhu Mziray, baba mdogo wa marehemu, Antony amewashukuru Jeshi la Polisi na watu wote waliojitokeza kushirikiana na familia hiyo tangu tukio hilo lilivyojitokeza.

Mziray amewataka ndugu, jamaa na majirani kuwa watulivu na kujiepusha na taarifa zisizo rasmi zinazozagaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu tukio hilo.


“Tujiepushe na taarifa zisizo na ukweli zinazozagaa mitandaoni na kuliacha Jeshi la Polisi kukamilisha uchunguzi wake na kuja na taarifa rasmi,” amesema.

Mwanasha Amiri ambaye ni dada wa marehemu Anna amesema wawili hao walikuwa msaada mkubwa ndani ya familia.

“Ukikutwa na tatizo hawawezi kukuacha kama wana uwezo wa kuwasaidia, msiba huu ni pigo kubwa kwetu,” amesema Mwanasha.

Ester Jones ambaye ni jirani wa marehemu hao amesema wanabaki na kumbukumbu ya upendo na ushirikiano kwa majirani.

“Walikuwa wanapenda sana kushirikiana na majirani, hata baadhi ya vikao vya jumuiya au ujirani mwema tulikuwa tukifanyia nyumbani kwao, Mungu awapumzishe mahala pema,”amesema.

Juni 12, 2025, akisimulia namna alivyobaini kutokea kwa tukio hilo, msaidizi wa kazi za ndani wa familia hiyo, Mariam Said alisema waligundua kutokea kwa tukio hilo baada ya mtoto wa marehemu kugonga kwa muda mrefu chumba cha wazazi wake asubuhi akihitaji nauli ya kwenda ‘tuisheni’ (kwenye masomo ya ziada) bila ya mafanikio.

Alisema baadaye akiwa anafanya usafi nje ya dirisha la wanandoa hao aliona dirisha la wanandoa hao limevunjwa kidogo huku pazia likiwa na madoa mithili ya damu, hali iliyomtia shaka.

“Nilikimbia kumueleza mtoto wao mkubwa ambaye alikimbia kwa haraka kuingia chumbani kwao na kukuta miili yao ikiwa imejeruhiwa,” alisema Mariam.


Alisema baada ya kuwapigia baadhi ya ndugu waliwashauri kutoa taarifa kwa majirani waliowasaidia kutoa taarifa kwa uongozi wa mtaa.

Mariam alisema awali kabla ya tukio hilo kutokea majira ya saa mbili usiku (ya Juni 11, 2025) wanandoa hao walirudi nyumbani na baada ya kula chakula usiku waliingia ndani kupumzika.

“Baada ya hapo hatukusikia makelele wala kiashiria chochote kibaya hadi asubuhi tulipoiona miili ya dada na kaka ikiwa imejeruhiwa,” alisema Mariam huku akibubujikwa na machozi.

Related Posts