Mkuranga yapata hati safi miaka tisa mfululizo, RC Kunenge atoa angalizo

Mkuranga. Wakati Halmashauri ya Mkuranga ikiwa imepata hati safi kwa miaka tisa mfululizo, Mkuu wa Mkoa wa Pwani (RC), Abubakari Kunenge ametaka hati hizo ziendane na miradi inayowagusa wananchi moja kwa moja kwenye maeneo yao.

Kunenge ameyasema hayo leo Jumanne Juni 17, 2025 katika kikao maalumu cha baraza la madiwani cha kupitia taarifa za utekelezaji wa hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, 2024.

Amesema ukaguzi ni namna walivyokusanya na walivyotumia fedha, hivyo ni vema wakahakikisha wanakusanya na kutumia kwa tija ikiwemo katika miradi inayoanzishwa kuwagusa wananchi.

Katika kufanikisha hilo pia amewataka madiwani wapeleke mapendekezo ya miradi wanayotaka itekelezwe katika maeneo yao kwa kuwa wao ndio wanakaa na wananchi huko.

“Ni aibu Rais anakuja eneo lako anakunadi kwa kusema hapa tutaleta maji, wananchi wanakataa kwa kupiga kelele wanasema wanataka shule. Msipofanya hivyo sisi tutafanya kwa hisia, tutaweka tunachojua wakati nyie ndio rahisi kujua wananchi wanataka nini kwa kuwa mnakaa huko,” amesema Kunenge.


Akielezea kupata hati safi, Kunenge amewapongeza na kuwashukuru madiwani kwa ushirikiano waliouonyesha katika ukusanyaji mapato na kusimamia matumizi ya fedha zinazopatikana.

“Malengo yenu kwenye makusanyo mlitakiwa kukusanya Sh14.35 bilioni, lakini mmekusanya Sh16.72 bilioni hivyo kukusanya zaidi ya asilimia 116.49,” amesema Kunenge.

Kutokana na hilo, amesema halmashauri hiyo imekuwa ya tatu katika makusanyo ikiongozwa na Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha na kufuatiwa na Halmashauri ya Chalinze.

Hata hivyo, amesema kwa ardhi waliyonayo Mkuranga na idadi kubwa ya watu anaamini wanaweza kukusanya zaidi ya mapato hayo kwani wakati Kibaha ikipata fedha zaidi kupitia uuzaji wa viwanja, Mkuranga inaongoza kwa kuwa na viwanda lakini pia imejaliwa kuwa na fukwe ambazo bado hazijatumiwa ipasavyo.

Awali, akiwasilisha ripoti ya  utekelezaji wa taarifa hiyo ya CAG kwa niaba Mkurugenzi wa Halmashauri, Mweka hazina wa Halmashauri ya Mkuranga, Cornery Sima amesema  halmashauri hiyo imepata hati safi kwa miaka tisa mfululizo.

Sima amesema katika ukaguzi huo walikuwa na jumla ya mapendekezo 44 katika ripoti tatu walizokuwa nazo.

Katika Ripoti Kuu amesema walikuwa na mapendekezo 33 na kati ya hayo mpaka sasa yaliyofungwa ni 16 na 17 yaliyobaki wanaendelea kuyafanyia kazi.

“Tulikuwa na mapendekezo katika kitabu cha wenye ulemavu na wanawake matano, ambayo mpaka sasa bado hayajafungwa na kwa mfuko wa pamoja wa afya kulikuwa na mapendekezo sita na yote yamefungwa,”amesema mweka hazina huyo.

Naye Mkaguzi Mkuu wa ndani wa Mkoa, Pastory Massawe amesema bado kuna hoja 22 zinatakiwa kufanyiwa kazi katika ripoti hiyo ikiwa ni pamoja na kuhakiki miradi mbalimbali na kubainisha, ana imani menejimenti itaendelea kushirikiana nao katika kaguzi zinazofuata.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Mkuranga, Omar Mwanga amesema hoja zilizoibuliwa katika taarifa hiyo wanachukulia kwa umakini ambapo lengo mbele kusiwe na hoja kabisa.


“Hoja zipo kwenye afya na uwezeshaji wa vijana na wenye ulemavu. Tunasisitiza uwezeshaji wa makundi haya katika wilaya lakini kuhakikisha tunawasimamia vizuri kwenye miradi wanayoianzisha ili hela hizo za Serikali ziweze kurejeshwa,” amesema Mwanga.

Kwa upande wake, Meya wa Halmashauri hiyo, Mohammed Mwera, akitoa shukurani kwa niaba ya madiwani, amesema Mkuranga hadi kufika hapo wanajivunia uwepo wa Mkuu wa Mkoa huyo na timu yake, kwani kila mwaka imekuwa ikipaa na kueleza kile walichokuwa wanataka amekuwa mwepesi kukifutilia na kuleta matokeo chanya.

Related Posts