Mbeya. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia Steven Kipara (38), mkazi wa Ipwizi Wilaya ya Mbeya kwa tuhuma za kupanga njama na kukodi watu kwa lengo la kumuua mama yao mzazi Kweli Lugembe (75), badala yake kumjeruhi kwa risasi za mtoto Sinzo Jifwalo (4).
Imeelezwa tukio hilo limetokea Juni 13, 2025 saa 6:05 usiku huko Kijiji cha ipwizi kilichopo Kata ya Mjele, Wilaya ya Mbeya vijijini.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, SACP Benjamin Kuzaga amesema leo Jumanne Juni 17, 2025, kuwa mtuhumiwa alikuwa akimtuhumu mama yake mshirikina na kisha kukodi watu wawili kutoka Mkoa wa Lindi kwa lengo la kutimiza mauaji hayo.
Uchunguzi wa awali umebaini mtuhumiwa alipanga njama ya kumuua mama yake mzazi, Kweji Lugembe (75), kwa madai ya kuhusika na vifo vya watoto na wadogo zake.
Kuzaga amesema Juni 8, 2025 mtuhumiwa alikodi watu hao kutoka Kilwa Mkoa wa Lindi kwa lengo la kutimiza mpango huo na kisha kuwapangia nyumba ya kulala wageni katika eneo la Mbalizi Wilaya ya Mbeya.
Amesema Juni 10, 2025 saa 6.05 usiku walienda nyumbani kwa mama wa mtuhumiwa na kisha kupiga risasi kadhaa kupitia dirishani ambazo zilimjeruhi mtoto huyo.

Bastola ambayo ilipangwa kutumika kufanya mauaji.
“Mtuhumiwa aliwakodi watu hao kwa Sh5 milioni, kwa lengo la kutekeleza mauaji, lakini kwa bahati mbaya hawakufanikiwa na badala yake kumjeruhi mtoto aliyekuwa amelala na mlengwa,” amesema.
Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi lilifanya msako mkali na kufanikiwa kumkamata mmoja wa watu waliotumwa kutekeleza mauaji hayo Tabi Deus (35).
Kuzaga amesema baada ya kupekuliwa alikutwa akiwa na bastola moja iliyotengenezwa kienyeji isiyo kuwa na namba na risasi mbili za ‘shot gun’ zikiwa ndani ya mkoba mdogo.
Kuzaga amesema baada ya mahojiano, Juni 15, 2025 saa 1:00 jioni Tabi Deus (39) alikiri kutenda kosa na kisha kuwaongoza alipo mtuhumiwa Shija kwenye eneo lenye korongo na vichaka.
“Baada ya askari kufika katika eneo hilo lenye vichaka na korongo mtuhumiwa ghafla alikurupuka na kuanza kukimbia ndipo askari walifyatua risasi tatu hewani kwa lengo la kumtaka kutii amri, lakini alikaidi ndipo alipigwa risasi mguu wa kulia na kufanikiwa kumkamatwa,” amesema.
Hata hivyo baada ya kujeruhiwa kwa risasi aliwahishwa Hospitali Teule ya Ifisi kwa ajili ya kupatiwa matibabu lakini alifariki dunia.