Wazazi walaumiwa kuwafelisha wanafunzi kipindi cha mitihani

Dodoma. Katibu Tawala Wilaya ya Bahi, jijini Dodoma,  Mwanamvua Bakari amewataka wazazi kuacha mara moja tabia ya kuwapotosha watoto  katika kipindi cha mitihani kwa kuwashawishi wasijibu vizuri maswali ili wafeli kisha waende mijini wakafanye kazi za ndani.

Mwanamvua ametoa kauli hiyo leo Jumanne Juni 17,2025 alipotembelea Shule ya Msingi Chiboli iliyomo wilayani humo.

Amesema wazazi wengi wamekuwa wakiwaelekeza watoto wao kujibu vibaya mitihani ili wakose fursa ya kuendelea na masomo kwa lengo la kuwapeleka mijini kufanya kazi za ndani, jambo ambalo ni hatari kwa maendeleo ya  Taifa.

Kauli ya Katibu Tawala amekuja katika kipindi ambacho Bahi inaendelea kupigania nafasi ya 10 bora kitaifa katika mitihani ya kuhitimu elimu ya msingi kutokana na mkakati waliyojiwekea.

“Sisi Bahi tuna changamoto, watoto wetu wengi wakiacha shule hukimbilia mijini kufanya kazi za ndani na sisi wazazi tunawakatisha kwa kuwa tunaona wakienda kufanya kazi tutapata mapato,”amesema Mwanamvua.

Katibu huyo amesema baadhi ya wazazi wamewachukulia watoto wao kama vyanzo vya kipato kwa kuwapeleka katika majiji makubwa ikiwemo Dar es Salaam kufanya kazi za ndani, jambo linaloweka watoto katika mazingira hatarishi ya ukatili na unyonyaji.

“Serikali haitavumilia vitendo vya aina hiyo, tutachukua hatua kali dhidi ya wahusika kwa kushirikiana na vyombo vya dola ikiwemo watendaji wa Kata na Polisi,” amesema.

Pia amewataka wazazi kuacha tabia za kumaliza kesi za ukatili wa  kijinsia kifamilia badala yake waachie mamlaka za kisheria kumaliza masuala hayo ili kuhakikisha haki inatendeka na kuwa fundisho.

Kwa upande wa watendaji na Polisi amewahimiza kushirikiana na wananchi ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa  muhimu juu ya matukio ya ukatili, kwa lengo la kufanikisha utolewaji wa hukumu stahiki kwa wanaotenda makosa.

Ofisa Mawasiliano wa mradi wa Save the Children, Fedrick Shija ametoa wito kwa Serikali kuimarisha utoaji wa huduma za afya kwa watoto na kuhakikisha upatikanaji wa haki kwa wanaofanyiwa ukatili.

Shija amesema jambo hilo litachochea mapambano dhidi ya ukatili kuwaweka mbali na  uwezekano wa kukumbana na masuala ya ukatili.

Hata hivyo ametoa wito kwa jamii na Serikali kuwapa watoto nafasi ya kushiriki katika kufanya maamuzi kuanzia ngazi ya familia hadi Taifa ikiwemo upangaji wa bajeti za familia.

Gift Emanueli mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Chiboli ameiomba Serikali kuongeza upatikanaji wa vifaa vya kujifunzia na kujenga mabweni ili kuwanusuru kutembea umbali mrefu kufuata masomo.

Related Posts