Mgawanyo majimbo ya Zanzibar ‘ngumu kumeza’

Miongoni mwa mambo muhimu ambayo kila taifa linapaswa kuyatekeleza kwa uwazi, uadilifu na bila kuacha maswali ni uchaguzi mkuu wa nchi.

Nasema hivyo hasa tukitazama historia za uchaguzi wa nchi nyingi za Afrika, Tanzania ikiwa miongoni, mara nyingi kipindi hicho hugeuka kuwa chanzo cha migogoro.

Ikitafakariwa kwa kina, mingi ya migogoro hiyo ingeweza kuepukika kama kungekuwepo na utashi katika kutekeleza mchakato wake kwa haki na usioegemea upande wowote.

Lakini kadiri tunavyoelekea katika uchaguzi mkuu ujao utakaofanyika baadaye mwaka huu hususan kwa upande wa Zanzibar, kumekuwa na malalamiko kuhusu baadhi ya masuala hasa la upangaji wa majimbo ya uchaguzi.

Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) inalaumiwa kwa kutotoa ufafanuzi wowote kuhusu hatua zake, hali inayoonekana kama kutojali haki ya wananchi kuuliza au kuelewa uamuzi unaohusu mustakabali wao wa kisiasa.

Malalamiko makubwa yanahusu hatua ya kuunganisha majimbo matano ya Mji Mkongwe na maeneo jirani kuwa jimbo moja.

Awali, maeneo hayo yalikuwa majimbo tofauti kama Malindi, Mkunazini, Mlandege na sehemu za Kikwajuni na Makadara, lakini sasa yameunganishwa na kuwa jimbo moja.

Chama cha upinzani cha ACT Wazalendo kinalalamika kuwa hatua hiyo imechukuliwa kwa makusudi ili kupunguza nguvu ya ushindi katika maeneo wanayodai kuwa ngome yao. Utakumbuka asilimia kubwa ya makada na viongozi wa chama hicho kwa upande wa Zanzibar, waliamua kujivua uanachama wa Chama cha Wananchi (CUF) na kuamua kujiunga na chama hicho cha ACT Wazalendo.

Kwa historia ya uchaguzi kwa huko Zanzibar tangu mfumo wa vyama vingi urejee, Chama cha CUF ndicho kilikuwa mpinzani mkuu wa CCM, kabla ya kukumbwa na misukosuko na kujikuta kikipoteza makada wake wengi waliohamia ACT Wazalendo.

Wananchi wanataka majibu ni kwa nini majimbo matatu kamili na sehemu za mawili yameunganishwa bila maelezo ya wazi.

Aidha, kuna utata kuhusu kuundwa kwa jimbo jipya la Fuoni na kupanuliwa kwa jimbo la Mji Mkongwe katika uchaguzi wa 2020.

Inadaiwa kuwa majimbo mengine yana idadi ya wapiga kura zaidi ya 7,000, lakini jimbo la Mji Mkongwe lina wapiga kura wasiopungua 1,600 pekee, jambo linaloibua maswali kuhusu usawa wa ugawaji huo.

Kwa mfano, ukubwa wa jimbo hilo ni kama kiwanja cha mpira, lakini lina hadhi ya kuwa jimbo kamili, hali inayofifisha imani ya wananchi kuhusu haki ya uchaguzi.

Ikiwa viwango vya kawaida vya idadi ya wapiga kura kwa jimbo ni takribani 10,000, ni kwa vipi jimbo lenye idadi ndogo kiasi hiki linaendelea kuwepo bila marekebisho?

ZEC inapaswa kutoa maelezo ya wazi juu ya vigezo vilivyotumika kupanga majimbo hayo. Kama ni bahati mbaya, basi hatua zichukuliwe kufanya marekebisho kabla ya uchaguzi ujao ili kurejesha imani kwa wananchi.

Zanzibar ina historia ya chaguzi zenye mvutano, na ZEC ndiyo yenye dhamana kubwa ya kuhakikisha hali hiyo haijirudii.

Viongozi wa Tume hiyo wanapaswa kufahamu kuwa maisha, furaha na amani ya Wazanzibari iko mikononi mwao. Historia itawahukumu kwa mema au mabaya kulingana na jinsi wanavyosimamia uchaguzi huu kwa uwazi au kwa usiri unaozua mashaka.

Kwa sasa tayari zimeshaanza kusikika kauli za chuki kutoka kwa baadhi ya wanasiasa, jambo ambalo linapaswa kukemewa bila kujali anatoka chama gani.

Hatua hizi si tu zinapaswa kukemewa, bali pia zishughulikiwe kwa ukali ili kuhakikisha mazingira ya uchaguzi yanabaki kuwa ya utulivu.

Aidha, ni muhimu kuzuia vitendo vinavyotishia usalama wa wananchi wakati wa uchaguzi. Matukio ya chaguzi zilizopita kama ya magari yenye bendera nyekundu yanayoongozana na askari wa vikosi vya ulinzi kuvamia maeneo ya mikutano na kuwapiga wananchi kama vile miili yao ni mazulia ya vumbi hayapaswi kurudiwa.

Hali kama hiyo huzalisha makundi ya kihuni kama vile ‘Janjaweed’ au ‘Mazombi’ wanaodaiwa kuivamia nyumba za watu, kupiga wananchi na kupora mali.

Wapo waliouawa katika mazingira haya, jambo ambalo linahitaji kushughulikiwa kwa nguvu zote na Jeshi la Polisi ambalo lina dhamana ya kulinda raia na mali zao.

Kwa kuwa muda uliobaki kabla ya uchaguzi si mrefu, ni muhimu hatua zote za tahadhari zichukuliwe sasa.

Lengo ni kuhakikisha uchaguzi unaokuja unafanyika katika mazingira ya amani, uhuru na haki kwa kila upande.

Related Posts