Wasaka ubunge majimbo ya Mwanza wakoleza joto

Mwanza. Haikuwa na haitakuwa kazi rahisi hata kidogo! Huo ndio usemi unaofaa kuelezea hali ya kisiasa, hasa nafasi za ubunge katika majimbo ya Nyamagana, Ilemela, Sengerema na Buchosa ambayo ni sehemu ya majimbo manane ya uchaguzi mkoani Mwanza.

Ugumu wa uchaguzi mwaka huu unaanzia kwenye mchakato wa uteuzi ndani ya vyama kutokana na mwamko wa kisiasa wa makada bila kusahau majina ya wale wanaotajwa au kuhusishwa na nafasi za ubunge katika majimbo hayo ambayo kwa sasa, yote yanaongozwa na wabunge kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi, (CCM).

Hata hivyo, Mwananchi imezungumza na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Michael Smart anasema chama hicho tawala kimejiandaa siyo tu kushinda uchaguzi, bali kuanzia kwenye uteuzi sahihi wa wagombea wtakaopeperusha bendera ya chama hicho.

“Tunataka kuweka historia tena kwa kupata kura nyingi kwa wagombea wetu tutakaowateua wa ubunge na udiwani,” amesema Smart.

Katika mkoa huo, majimbo ya Sengerema na Buchosa yanawakilishwa na wabunge kupitia CCM tangu chaguzi za mfumo wa vyama viliporejeshwa mwaka 1995.

Majimbo ya Ilemela na Nyamagana yalikombolewa mwaka 2015 baada ya wagombea kupitia CCM kuwashinda waliokuwa wabunge kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

CCM kupitia kwa Mabula wawili wanaotofautisha kwa jinsi zao kwa utambulisho wa Mabula ‘Baba’ na Mabula ‘Mama’ iliyakomboa majimbo ya Nyamagana baada ya Stanslaus Mabula kumshinda Ezekhia Wenje jimbo la Nyamagana, huku Angelina Mabula akimwangusha Highnes Kiwia jimbo la Ilemela.

Wenje na Kiwia walishinda nafasi hizo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 ambao pia ulishuhudia Chadema ikinyakua majimbo ya Maswa Mashariki, Musoma mjini, Biharamulo, Maswa Magharibi, Bukombe na Meatu kabla ya kuyapoteza yote mwaka 2015 ikibakiwa na jimbo la Ukerewe pekee.

Licha ya kupokwa majimbo ya Nyamagana na Ilemela, Chadema nayo ilijibu mapigo kwa wagombea wake kuwashinda wenzao wa CCM katika majimbo ya Bunda, Tarime Mjini, Tarime Vijini na Bukoba mjini.

Ingawa hadi sasa hakuna aliyetangaza rasmi kugombea ubunge, ni wazi wabunge wa sasa wa Nyamagana, Ilemela, Sengerema na Buchosa, wote kupitia CCM watatetea nafasi zao.

Tofauti na uchaguzi uliopita wa mwaka 2020 ambapo hali haikuwa tete sana kuanzia kura za maoni kabla ya kuteuliwa kuwakabili wagombea kutoka vyama vingine, mwaka huu wote wanaofikiria nafasi za ubunge ni sharti wajipange kikamilifu kutokana na majina ya makada wenye nia au wanaotajwa kuweza kuingia kwenye kinyang’anyiro cha ubunge kupitia chama hicho.

Hamisi Tabasamu, mbunge wa Sengerema anayemaliza kipindi chake Juni 28, mwaka huu bunge litakapovunjwa rasmi, sasawitalazimika kukaza misuli kuhimili kishindo cha makada na vigogo wa CCM na Serikali wanaotajwa kwenye nafasi hiyo.

Katika orodha hiyo, yumo Ngusa Samike, ambaye siyo tu ana mizizi ya kuzaliwa na kisiasa ndani ya jimbo la Sengerema, bali pia wanaomuunga mkono tayari ‘wanapitapita’ kusafisha njia.

William Ngeleja, mbunge wa zamani wa Sengerema, Mganga Mkuu Mkoa wa Geita, Dk Omar Sukari na Joshua Simiyu ni miongoni mwa makada wa CCM wanaotajwa kujipanga kujitosa kwenye kinyang’anyiro cha kuomba uteuzi kupeperusha bendera ya CCM uchaguzi mkuu ujao.

Mbunge wa sasa wa Buchosa, Erick Shigongo ambaye hiki ni kipndi chake cha kwanza bungeni naye atalazimika kufanya kazi ya ziada kutetea nafasi hiyo ili kupenya kwenye kinyang’anyiro hicho cha kuomba ridhaa ya kutetea kiti hicho.

Hii ni kutokana na nguvu ya kisiasa inayochagizwa na uzoefu wa mbunge wa zamani wa jimbo hilo, Dk Charles Tizeba anayetajwa kujitosa tena kuomba ridhaa ya chama chake baada ya kutoswa uchaguzi wa 2020.

Kwa sababu tayari Mhandisi wa Maji kutoka Wilaya ya Maswa, Mathias Nandi naye havumi lakini yumo katika orodha ya wanaotajwa kukinyemelea kiti cha ubunge Buchosa.

Mabula Baba na Mama wajipange

Tofauti na mwaka 2020 ambapo walipata mchekea, safari hii, Mabula Baba wa Nyamagana na Mabula Mama wa Ilemela wanapaswa kusimika miguu chini kwa kutumia uzoefu na misiuli yao ya kisiasa kupenya katika mchakato wa kura za maoni hadi uteuzi ndani ya CCM kutokana na aina ya majina ya makada wanaoweza kuingia kwenye kinyang’anyiro.

Kwa Ilemela, Angelina Mabula atalazimika kumkabili Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (MNEC), Leonard Mahende maarufu ‘Manguzo’ ambaye siyo tu jina lake linatajwa, bali pia ana misuli ya kisiasa, kiuchumi na wingi wa watu wanaomuunga mkono nyuma yake.

Ingawa hajatangaza nia yake, jina la Mehende limo midomoni mwa wana CCM na kwenye duru za siasa za Jimbo la Ilemela kutokana na ushiriki wake wa muda mrefu kwenye shughuli za kijamii ikiwamo misaada ya kiutu kwa wanaopata majanga bila kujali itikadi zao za kisiasa.

Jina la Abubakar Kunenge, Mkuu wa Mkoa wa Pwani pia ni kati ya makada wanaotajwa kwamba wanaweza kujitosa kumkabili Mabula pale Nyamagana.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda ambaye pia ni mwenyeji wa Nyamagana naye anatajwa kama ilivyokuwa uchaguzi wa mwaka 2020 kabla hajaibukia Kigamboni. Pamoja na Nyamagana, Makonda pia anahusishwa na ubunge wa Jimbo la Arusha mjini.

Nguvu ya kisiasa inayoonyeshwa sasa na Chama cha Ukomozi wa Umma (Chaumma) baada ya kuwapokea makada waliojiengua kutoka Chadema ni jambo linaloongeza joto la uchaguzi katika majimbo ya Mkoa wa Mwanza.

“Chaumma hatuwaachia CCM wapiti au washinde kirahisi katika nafasi za ubunge, udiwani na Urais; tuko kwenye mchakato wa kutambua na kuandaa wagombea wenye uwezo wa kushinda,’’ anasema John Ongito, Katibu wa Chaumma Mkoa wa Mwanza.

Akizungumza na Mwananchi kwa simu, Ongito ameongeza; “Tunao makada wengi wenye sifa na uwezo wa kushinda ubunge katika majimbo ya Ilemela, Buchosa, Nyamagana na Sengerema; pia tunatarajia kupokea wagombea wengine wenye sifa kutoka vyama vingine pindi mchakato wa uteuzi utakapoanza.”

Related Posts