Samia aweka jiwe la msingi shule 103 za amali, kiwanda cha pamba

Mwanza. Rais Samia Suluhu Hassan ameweka jiwe la msingi katika Shule ya Sekondari ya Amali ya MwamaPalala, iliyoko katika Wilaya ya Itilima, mkoani Simiyu.

Shule hii ni ya mfano, miongoni mwa shule 103 za amali zinazojengwa kote nchini, lengo kuu likiwa ni kumwandaa mwanafunzi si tu kwa mtihani wa kitaaluma, bali pia kwa ujuzi wa moja kwa moja wa ajira, kazi za mikono, ujasiriamali au kujiendeleza katika vyuo vya elimu ya ufundi.

Akizungumza katika hafla hiyo Leo Jumatano, Juni 18, 2025, Rais Samia amesema Serikali imelenga kukuza elimu ya amali kwa madhumuni ya kuwajengea vijana ujuzi wa kujiajiri na pia kuajirika, hususan katika sekta binafsi.

Akizungumza wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi, Rais Samia amesema mfumo wa sasa wa elimu umeelekezwa katika kuwapatia wanafunzi ujuzi wa vitendo mara baada ya kumaliza kidato cha nne, ili wasitegemee ajira pekee, bali waweze pia kujiajiri.

“Mtoto akimaliza kidato cha nne anatoka hana la kufanya, anasubiri ajira. Lakini, sasa tumeamua kubadilisha mwelekeo kiasi kwamba mtoto akimaliza kidato cha nne anakuwa na ujuzi wa kujiajiri, asisubiri kuajiriwa. Ndiyo maana Serikali imeamua kujenga shule za amali na ufundi kama hizi,” amesema Rais Samia.

Aidha, Rais Samia amewahimiza wazazi na walezi kuwapa watoto wao fursa ya kusoma katika shule za amali, akisisitiza umuhimu wa elimu hiyo katika kuwajengea vijana mustakabali bora.

Amesema Serikali itaendelea kuongeza idadi ya walimu ili kuboresha mazingira ya kujifunza; ambapo kwa sasa, Shule ya Amali ya MwamaPalala ina walimu watano pekee.

Vilevile, ameahidi kushughulikia changamoto mbalimbali zinazoikabili Wilaya ya Itilima, ili kuharakisha maendeleo ya elimu na huduma nyingine za kijamii. 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa, amesema ujenzi wa shule hiyo umetumia Sh1.6 bilioni na hadi sasa umefikia asilimia 96 ya utekelezaji.

Kwa mujibu wa Mchengerwa shule hiyo ina majengo 13, yakiwemo madarasa manane, bwalo, mabweni manne, vyoo vya wanafunzi (matundu manane), jengo la utawala, nyumba ya watumishi, pamoja na majengo matatu ya ufundi – yaani karakana za useremala, uashi na mabomba, ambayo bado hayajakamilika kujengwa.

Pia, majengo yote yameunganishwa kwa barabara ndogo zinazorahisisha usafiri na utembeaji kati ya jengo moja na jingine, hivyo kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.

Aidha, Mchengerwa amesema halmashauri zote zinazotekeleza mradi wa ujenzi wa shule za amali, zimekubaliana kujenga uzio kuzunguka shule hizo kwa kutumia mapato ya ndani, ili kuhakikisha usalama wa wanafunzi na mali za shule.

Akifafanua zaidi,  Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema mageuzi ya elimu yanayotekelezwa na Serikali yanahusisha kuanzishwa kwa shule za amali zinazotoa mafunzo ya ufundi na stadi mbalimbali za maisha.

Ameeleza kuwa mafunzo hayo yanagawanyika katika makundi mawili, la kwanza likihusisha stadi za maisha kama kilimo, uvuvi na ufugaji; na la pili mafunzo ya ufundi kama useremala, uashi, umeme na fani nyingine za kiufundi.

“Awali, tulikuwa na shule kama Ifunda Technical, Moshi Technical na Bwiru, ambazo zilitoa elimu ya amali, lakini kwa muda mrefu zilipoteza mwelekeo na kuacha kufundisha kwa mfumo huo. Sasa Serikali inarejesha mfumo huu muhimu kwa maendeleo ya taifa,” amesema Profesa Mkenda.

Amesema kuwa kati ya shule 103 za amali zinazojengwa nchini, 26 zinajengwa katika awamu ya kwanza upande wa Tanzania Bara, huku Zanzibar zikijengwa mbili.

“Wahitimu wa shule hizo watapewa vyeti viwili: cheti cha kidato cha nne kutoka Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) na cheti cha ufundi kutoka Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Nactvet), ambacho kitawawezesha kuingia moja kwa moja kwenye soko la ajira,” amesema.

Amesema wanafunzi watakaohitimu pia watakuwa na fursa ya kuendelea na elimu ya juu kupitia shule za sekondari za amali za juu kwa kipindi cha miaka miwili, au kujiunga na vyuo vya kati (polytechnics) kwa miaka mitatu, na baadaye kuendelea hadi chuo kikuu.

Profesa Mkenda ameeleza kuwa Serikali tayari imetenga vifaa vya kujifunzia vyenye thamani ya Sh40 bilioni ili kuhakikisha wanafunzi wanaanza masomo rasmi ifikapo Januari 2026.

Mpaka sasa, shule 115 tayari zimejisajili rasmi kama shule za amali nchini.

Kiwanda cha kuchakata pamba

Katika hatua nyingine, Rais Samia amefungua rasmi kiwanda cha kuchakata pamba cha Shree Rajendra Agro Industries Ltd, kilichopo katika Wilaya ya Itilima.

Kiwanda hicho kinajumuisha miundombinu mbalimbali ikiwemo jengo la kuchambua pamba na maghala ya kuhifadhi bidhaa hiyo.

Kiwanda hicho kinalenga kuongeza thamani ya zao la pamba, kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na India na kufanikisha usindikaji na usafirishaji wa pamba kwenda masoko ya kimataifa.

Aidha, mradi huo unatarajiwa kuinua kipato cha wakulima, kuongeza ajira kwa wananchi wa Itilima na kuchangia mapato ya halmashauri pamoja na Mkoa wa Simiyu kwa ujumla.

Hadi sasa, kilo moja ya pamba inauzwa kwa Sh1, 200, ikiwa ni ongezeko la Sh50 kutoka bei ya awali ya Sh1,150.

Related Posts