Tehran, Iran. Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayattolah Ali Khamenei ameionya Marekani kutojihusisha na mzozo unaoendelea kati ya taifa lake na Israel, huku akidai kuwa ikifanya hilo kosa mzozo huo utageuka kuwa vita kamili.
Shirika la Habari la Serikali la Tasnim limeripoti kuwa, Khamenei ametoa kauli hiyo leo Jumatano Juni 18, 2025, wakati ambao Israel na Iran zinabadilishana mashambulizi yanayoendeshwa kwa kutumia ndege za kivita na makombora ya masafa marefu yakiingia siku ya sita.
Katika taarifa ambayo awali vyombo vya habari vya serikali ya Iran vilisema ingetangazwa katika runinga leo, Khamenei ametoa onyo kali kuwa Marekani inapaswa kufahamu kuwa Iran haitasalimu amri, na mashambulizi yoyote kutoka nchi hiyo (Marekani) yatakuwa na madhara makubwa yasiyoweza kurekebishwa.”

“Kama kuna jambo historia ya Iran inafundisha ni kwamba watu wa Iran hawajibu vyema lugha ya vitisho,” amesema Khamenei katika maneno yaliyonukuliwa, ingawa hakujitokeza hadharani kwa njia ya video.
Ameongeza kuwa Israel imefanya makosa makubwa na taifa hilo litalipia gharama ya kuishambulia Iran.
Usiku wa kuamkia leo, mashambulizi mapya ya makombora kutoka Israel yalipenya katika anga la Iran na kugonga baadhi ya maeneo ya Mji Mkuu, Tehran.
Ingawa mengi yalidhibitiwa na mifumo ya ulinzi ya anga ya Iran, Jeshi la Israel pamoja na Shirika la Kimataifa linalosimamia matumizi ya nyuklia duniani (IAEA) walithibitisha kuwa kituo kingine kinachohusishwa na mpango wa nyuklia wa Iran kulengwa na mashambulizi hayo.

Akizungumza na wanahabari leo, Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Israel, Brigedia Jenerali, Effie Defrin amesema kuwa, “operesheni ya usiku wa manane ilihusisha ndege zaidi ya 50 za kivita zilizoishambulia Iran kwa awamu tatu tofauti.”
Amesema katika mashambulizi hayo, Israel ililenga kutengeneza mitambo ya kurutubisha madini ya urani (centrifuge), ambao ungeuwezesha utawala wa Iran kuendelea kuimarisha mpango wake wa nyuklia.
“Hatua hii ni mwendelezo wa mashambulizi ya awali yaliyolenga vipengele vya mpango huo wa nyuklia,” amesema Defrin.
Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) limeeleza kupitia mitandao ya kijamii kuwa lina taarifa vituo viwili vya kuzalisha mitambo ya urani nchini Iran, karakana ya Tesa huko Karaj na Kituo cha Utafiti cha Tehran vimepigwa.
Shirika hilo limeongeza kuwa vituo hivyo vilikuwa chini ya uangalizi na uthibitishaji wa IAEA kama sehemu ya makubaliano ya pamoja ya nyuklia (JCPOA), ambayo Marekani ilijiondoa wakati wa kipindi cha kwanza cha utawala wa Rais Donald Trump.

Iran imejibu mashambulizi hayo kwa kurusha tena makombora kupitia Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Vifaa vya tahadhari vililia kwa nguvu katika miji mbalimbali ya Israel kuonya kuhusu mashambulizi hayo, lakini makombora mengi yalitunguliwa angani, huku milipuko ikishuhudiwa juu ya anga la Tel Aviv, Jerusalem, na maeneo yanayokaliwa kwa mabavu katika Ukingo wa Magharibi.
Mvutano huo unaoendelea wa kurushiana makombora umesababisha maafa makubwa kwa binadamu.
Tangu mwishoni mwa juma, serikali ya Iran haijatoa takwimu mpya, zaidi ya kusema kuwa zaidi ya watu 220 wamepoteza maisha.
Hata hivyo, shirika huru la Haki za Binadamu nchini Iran lenye makao yake makuu Marekani, ambalo hutegemea mtandao wa waangalizi ndani ya nchi hiyo, jana lilisema kuwa limeweza kuthibitisha vifo vya watu wasiopungua 452 tangu Israel ilipoanza mashambulizi yake, miongoni mwao ni wanajeshi 109.

Vita hii imeibua hofu kubwa na kusababisha wimbi la wakazi kuikimbia Tehran, mji mkuu wa Iran, huku video zikionesha maelfu ya magari yakiwa yamesongamana barabarani yakielekea nje ya jiji hilo.
Hofu hiyo imeongezeka kufuatia onyo la moja kwa moja la Trump mapema wiki hii, aliyewataka wakazi takriban milioni 10 wa Tehran kuhama mara moja.
Ingawa Israel imeisababishia Iran madhara makubwa zaidi, nayo pia haijanusurika na machungu.