Mwanza. Yalianza matarajio, ikafuata mipango, kisha mikakati na utekelezaji, hatimaye, Daraja la Kigongo-Busisi maarufu daraja la JPM limekamilika na kesho litaanza rasmi kutumika.
Kiu waliyonayo wakazi wa Mkoa wa Mwanza, kutumia dakika tatu hadi tano kuvuka daraja hilo badala ya saa moja hadi tatu kwa kutumia vivuko inakwenda kukatika.
Kukamilika na hatimaye kuzinduliwa kwa daraja hilo kunakofanyika kesho, Alhamisi Juni 19, 2025, kunaiwezesha Tanzania kuandika historia ya kuwa na daraja refu zaidi Afrika Mashariki na Kati.
Daraja hilo lenye urefu wa kilomita 3.2 limegharimu Sh716.3 bilioni zilizotolewa na Serikali, na linatajwa kuwa ufunguo wa uchumi wa Mwanza na maeneo ya jirani.

Rais Samia Suluhu Hassan ndiye anayetarajiwa kulizindua daraja hilo, ikiwa ni sehemu ya ratiba ya ziara yake ya kikazi katika mikoa ya Simiyu na Mwanza.
Kuanza kutumika kwa daraja hilo, kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, kutakomesha matumizi ya vivuko katika eneo la Kigongo-Busisi.
Amesema vivuko vitatu vilivyokuwa vinatumika katika eneo hilo vitapelekwa visiwa vingine ikiwemo Kome na Ukerewe, hivyo wananchi wa maeneo hayo watanufaika na ujenzi wa daraja hilo.

Mathalan, wakazi wa visiwa vya Kome na Ukerewe, amesema, watanufaika kwa kupelekewa vivuko vilivyokuwa vinatumika Kigongo-Busisi, hivyo adha ya uhaba wa vivuko inakwenda kuwa historia kwao.
Mtanda amesema hilo linakwenda sambamba na kuwaepusha wananchi na gharama ya Sh400 walizokuwa wanalipa kila wanapotumia kivuko, sasa watavuka kupitia darajani bila malipo.
“Kwa siku tulikuwa tunakusanya Sh5.2 milioni zinazotokana na nauli za wananchi kutumia vivuko. Kwa mwaka ilikuwa kama Sh1.8 bilioni. Fedha hizi zote zinakwenda kubaki kwa wananchi na wakaendelea kuzitumia kwa mahitaji mengine,” amesema.
Uhakika wa faida kwa wafanyabiashara wa samaki ulitegemea hali ya vivuko kwa siku husika katika eneo hilo, kama anavyoeleza Salma Sani, mfanyabiashara wa samaki mkoani Mwanza.
Kuna wakati, amesema, walilazimika kusubiri kivuko hadi samaki wanaharibika, lakini kuanza kutumika kwa daraja hilo kutakomesha jambo hilo.
“Hatuna tena haja ya kusubiri, sasa hivi ukiwa na mzigo wako utavuka tu na gari au pikipiki kuwapeleka unakotaka, na wanafika ndani ya muda,” amesema.

Kwa David Mayunga, kuanza kutumika kwa daraja hilo kutampa uhakika wa kusafirisha abiria wengi kwa daladala, kwa kuwa hana sababu tena ya kutumia muda mrefu kusubiri kivuko; badala yake, atapita darajani.
“Ujue hapa tulikuwa tunaingiza gari kwenye kivuko, unavuka, ndipo upakie abiria wako uendelee na safari. Lakini daraja linapotumika, maana yake tunapita darajani dakika tatu au tano badala ya masaa,” amesema.
Hatua hiyo, amesema, ilimfanya kuwa na safari chache za kupeleka abiria mkoani Geita, lakini sasa zitaongezeka na kipato kitaongezeka.
Kuchelewa kulikosababishwa na kusubiri vivuko ni adha iliyowakabili hata madereva wa malori, wanaosema hakukuwa na namna zaidi ya kuvusha gari kupitia kivuko, jambo ambalo kwanza ni gharama; pili, linapoteza muda mwingi.
“Hapa isingewezekana kuvusha lori ukiwa na mzigo, kwa hiyo unavusha bila mzigo. Sasa huwezi kupata faida katika mazingira hayo. Lakini daraja hili linatuwezesha kupita na lori lenye mzigo kwa muda mchache,” amesema.
Akizungumzia kuzinduliwa kwa daraja hilo, Meneja wa Kivuko cha Kigongo-Busisi wa Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa), Mboka Kibonde, amesema eneo hilo lilikuwa na vivuko vitatu.
Katika vivuko hivyo, amesema, tayari viwili vimeshapangiwa maeneo ya Ukerewe na Kome, huku mchakato wa kukipangia MV Sengerema eneo la kwenda ukiendelea.
Amesema hatua ya kuzinduliwa kwa daraja hilo ni muhimu kwa maslahi ya kiuchumi, kwa kuwa vivuko hutumia muda mwingi kuvusha watu na mizigo.

Muda uliokuwa ukitumika, amesema, ulitokana na masuala ya kiusalama yanayopaswa kuzingatiwa kabla ya kuanza kwa safari ya kivuko husika.
Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) Mkoa wa Mwanza, Paschal Ambrose, anasema daraja hilo, refu kuliko yote katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, lina urefu wa kilomita 3, upana wa mita 28.45, na barabara unganishi zenye urefu wa kilomita 1.66.
Daraja hilo lina njia mbili za magari zenye upana wa mita 7 kila upande, njia za watembea kwa miguu kila upande zenye upana wa mita 2.5, na maegesho ya dharura yenye upana wa mita 2.5 kila upande.
Katika barabara kutoka jijini Mwanza kuelekea lilipo daraja hilo, mabango mbalimbali yaliyopambwa kwa rangi za bendera ya Tanzania na picha ya Rais Samia yamesambaa.
Katika mabango hayo, jumbe mbalimbali zimeandikwa, ikiwemo kumkaribisha Rais Samia katika uzinduzi huo, lakini zipo picha zinazoonyesha taswira halisi ya daraja lenyewe.

Unapofika mwanzoni mwa daraja, unakutana na bango kubwa lililoandikwa: “Karibu Daraja la JP Magufuli (Kigongo-Busisi),” na ulinzi mkali umeimarishwa kuanzia mwanzoni.