Pembejeo, mikopo vyatajwa kuongeza uzalishaji tumbaku

Serengeti. Imeelezwa kuwa kilimo cha tumbaku mkoani Mara kinaendelea kuwa mkakati muhimu wa kukuza uchumi wa wakulima na jamii, hasa katika wilaya za Serengeti, Tarime na Rorya.

Ambapo wakulima 2,944 wamejisajili  kwenye Bodi ya Tumbaku kwa ajili ya kilimo cha zao hilo.

Katika mkutano wa Chama Kikuu cha Wakulima wa Mara (Wamacu) unaoshirikisha wadau wa zao la tumbaku na unaofanyika mjini Mugumu mkoani humo, leo Juni 18, 2025, kujadili maendeleo ya zao hilo, Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Dk Halfan Haule, na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, wamesisitiza umuhimu wa kutatuliwa haraka changamoto zinazohusiana na upatikanaji wa pembejeo na mikopo kwa wakulima.

Wameeleza kuwa changamoto hizo zimekuwa kikwazo kikubwa kinachokwamisha uzalishaji wa tumbaku.

Dk Haule ameeleza kuwa upatikanaji wa pembejeo kwa wakati ni suala la msingi linalotakiwa kufanyiwa kazi haraka ili wakulima waweze kuanza shughuli zao bila usumbufu msimu ujao, unaotarajiwa kuanza Julai Mosi. Ameongeza kuwa kilimo cha kisasa cha tumbaku kinaweza kuimarisha uchumi wa wakulima mara tatu zaidi na kusaidia kuondoa umaskini katika jamii.

Kwa upande wake, Meja Gowele ameomba taasisi za fedha zitoe mikopo kwa wakati na kwa riba nafuu ili kuwasaidia wakulima kupata pembejeo kwa gharama nafuu pia. Amesisitiza kuwa kilimo cha tumbaku kina mchango mkubwa katika mapato ya halmashauri na ustawi wa wananchi, hivyo wadau wanapaswa kushirikiana kwa karibu kuhakikisha zao hilo linaendelea kuleta tija.


Meneja Mkuu wa Chama Kikuu cha Wakulima wa Mara (Wamacu), Samwel Gisiboye amesema wakulima walikumbwa na changamoto za kuchelewa kupata pembejeo na mbegu, jambo lililosababisha uzalishaji kushuka na baadhi ya wakulima kukwepa kulipa mikopo. Ameahidi kuwa msimu wa kilimo wa 2025/26 utakuwa na mafanikio makubwa kwa kuhamasisha malipo ya mikopo na kuongeza tija.

“Tunajua kuwa wakati wa kupanda mkulima anatakiwa kuwa na mbegu na pembejeo tayari, ili aweze kutumia mbolea mara moja na baadaye kupulizia dawa za kuua wadudu.

“Hata hivyo, wakulima wa hapa walikuwa wakipokea mbegu tu, wakishapanda wanasubiri pembejeo, jambo ambalo limekuwa kikwazo kikubwa kwa ustawi wa zao la tumbaku,” ameeleza Gisiboye.

Wakulima pia wameonyesha matumaini makubwa. Rhobi Adam, mkulima kutoka Rorya, ametoa wito kwa mamlaka kuiga mfano wa Kenya kupanga msimu mapema ili kuleta mafanikio zaidi.

Mrajisi Msaidizi wa vyama vya ushirika mkoani Mara, Lucas Kihondere amesema uzalishaji wa tumbaku umeongezeka kutoka tani 700 msimu wa 2023/24 hadi tani 2,600 msimu wa 2024/25, na wanatarajia kufikia tani 5,000 msimu ujao kwa kuanzisha ushirika katika kila sekta ya kilimo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Kilimo wilayani Serengeti, Bwenda Bainga amesema mamlaka na wadau wanashirikiana kutatua changamoto, na mchakato wa kuagiza pembejeo unaendelea ili msimu mpya uanze bila vikwazo.

Related Posts