Dar es Salaam. Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Ofisi za Umoja wa Mataifa Geneva, Uswisi, Balozi Abdallah Possi amelihutubia Baraza la Haki za Binadamu, akikanusha taarifa iliyowasilishwa na wataalamu wa UN kuhusu matukio ya utekaji na watu kutoweka nchini.
Amekanusha madai yaliyotolewa na mwakilishi wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu wa Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika, akisema taarifa iliyotolewa ni ya upotoshaji, uzushi na uwasilishaji wake si sahihi kwa hali halisi.
Balozi Possi amewasilisha majibu ya Tanzania leo Juni 18, 2025, katika mkutano wa tano wa kikao cha 59 cha Baraza la Haki za Binadamu na hotuba yake kupatikana jijini Dar es Salaam.
Katika tovuti ya Umoja wa Mataifa Juni 13, 2025 ilichapishwa taarifa ya wataalamu wa UN wakitoa wito kwa Serikali ya Tanzania kukomesha matukio ya watu kupotezwa, hasa wapinzani wa kisiasa, watetezi wa haki za binadamu na waandishi wa habari, kama njia ya kuwanyamazisha kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba, 2025.
“Kuminya uhuru wa vyombo vya habari na waandishi na kuwatisha watetezi wa haki za binadamu ni jambo lisilokubalika. Tumeshtushwa na taarifa za mwenendo wa ukandamizaji kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Tanzania Oktoba,” ilieleza taarifa ya wataalamu hao.
Kutokana na taarifa hiyo, Balozi Possi aliieleza Mwananchi kuwa Serikali ingetoa msimamo wa kidiplomasia kwenye vikao vya Baraza la Haki za Binadamu wiki hii.
Katika hotuba yake leo Juni 18, Balozi Possi amesema Tanzania inaheshimu kikamilifu wajibu wake unaotokana na Katiba na mikataba ya kikanda na kimataifa ya haki za binadamu na kuwa wananchi wana uhuru wa kujieleza na kutoa maoni hata kama ni kinyume cha msimamo wa Serikali.
Amesema kuwa, kama mzungumzaji alivyoonekana kukiri; Tanzania ina demokrasia iliyokomaa, ikiwa imeshafanya chaguzi saba huru, za haki na za amani chini ya mfumo wa vyama vingi.
“Tanzania haijawahi kukosa kufanya uchaguzi kama inavyotakiwa na Katiba na ikiwa mwenendo wa kihistoria utaendelea, hali hiyo inatarajiwa pia wakati huu,” amesema.
Dk Possi amesema uwezo wa Tanzania kudumisha amani katika jamii yenye tofauti kubwa za makabila, imani na itikadi za kisiasa unatokana na uzingatiaji wake wa utawala wa sheria.
Amesema uzingatiaji wa utawala wa sheria unahakikisha wananchi wote wanatendewa haki kwa usawa, wakiwamo waliotajwa na mwakilishi wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu wa Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika, ambao ameeleza kwa bahati mbaya walishindwa kutangaza kwa uwazi madhumuni yao halisi ya kuingia Tanzania -ambayo ni hitaji la kawaida katika sheria za uhamiaji za mataifa mengi.
Balozi Possi amesema ingawa madai hayo bado hayajathibitishwa kwa uchunguzi huru, Tanzania inazichukua kwa uzito tuhuma zilizotolewa za mateso, ukatili wa kijinsia na ukiukwaji wa maadili. Amesema ndiyo sababu Tanzania inafanya uchunguzi na iwapo ukweli utabainika, waliohusika watawajibishwa.
Ameeleza kusikitishwa na hatua ya taasisi hiyo kuibua malalamiko kwa mambo ambayo hayaendelei kujitokeza.
“Baraza linapaswa kuwa makini dhidi ya madai yasiyo na msingi yanayoelekezwa kwa nchi mwanachama (Tanzania). Jambo muhimu la kuzingatiwa kuhusu tuhuma zilizotajwa na mwakilishi wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu wa Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika ni kwamba, kwa uwazi, mashauri hayo yanaonyeshwa mubashara kupitia mtandao (online TV), kuruhusu mtu yeyote duniani kufuatilia,” amesema.
Balozi Possi amesema Tanzania imejizatiti kulinda haki za binadamu na utawala wa sheria katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 na hata baada ya hapo.
“Tanzania imejizatiti kuhakikisha mazingira wezeshi kwa vyama vyote vya siasa kufanya kampeni zao kwa amani,” amesema.
Katika madai yao, wataalamu hao walieleza kuhusu matukio ya kutoweka wanaharakati wa haki za binadamu na waandishi wa habari, Boniface Mwangi wa Kenya na Agather Atuhaire wa Uganda, jijini Dar es Salaam, Mei 19, 2025, ambao baadaye walipatikana kwenye mipaka ya nchi zao.
Wakati wengine wakizuiwa kuingia nchini, Mwangi na Atuhaire waliingia Tanzania kufuatilia kesi dhidi ya kiongozi wa Chadema, Tundu Lissu anayestakiwa kwa uhaini na kuchapisha taarifa za uongo.
Ilielezwa wawili hao walikamatwa na polisi pasipo taarifa kutolewa na baadaye Mei 22, 2025, Mwangi alipatikana akiwa ametupwa Ukunda, mji wa pwani nchini Kenya, na siku moja baadaye Atuhaire aliachwa mpakani mwa Tanzania na Uganda. Wawili hao walidai waliteswa na kudhalilishwa kijinsia.
Wataalamu wa UN katika taarifa yao walidai: “Zaidi ya matukio 200 ya watu kupotezwa yameripotiwa nchini Tanzania tangu mwaka 2019.”
“Kukamatwa kiholela, kuteswa na kutoweka kwa Mwangi na Atuhaire kunaashiria mkakati wa wazi wa kuzuia sauti za upinzani na kukwepa sheria na taratibu za haki,” walieleza.
Imeelezwa katika taarifa hiyo kuwa, viongozi wa upinzani na wafuasi wao wameripoti ongezeko la mashambulio na ukiukwaji wa haki za binadamu, hasa katika maeneo yenye mvutano mkubwa wa kisiasa.
Ukiukwaji huo umeelezwa unajumuisha kukamatwa kiholela, unyanyasaji, mateso na kutoweka kwa viongozi vijana, watetezi wa haki za binadamu, na wanachama wa vyama vya upinzani.
“Ni wito kwa mamlaka za Tanzania kuchukua hatua za haraka kuacha kuficha taarifa za waliokamatwa kwa kuwa kufanya hivyo, ni sawa na kuwapoteza. Pia zichunguze na kuwawajibisha wanaokiuka haki,” walisema wataalamu hao na kuongeza:
“Serikali inapaswa kutoa haki na fidia kwa waathirika zikijumuisha huduma za matibabu, msaada wa kisaikolojia na kisheria, vyote vikizingatia jinsia kwa waathirika wa mateso na unyanyasaji wa kijinsia.”
Wakati Balozi Possi akieleza hayo Geneva, nchini Jeshi la Polisi limetoa taarifa kwa umma leo Juni 18, 2025 kuhusu matukio ya watu kupotea au kutoonekana, likieleza uchunguzi umebaini mengi ni ya kujiteka.
Uchunguzi umebaini sababu nyingine ni wivu wa mapenzi, imani za kishirikina, kugombea mali, kulipiza kisasi, kwenda nchi nyingine kujifunza misimamo mikali na kukimbia mkono wa sheria baada ya kufanya uhalifu.
Taarifa hiyo iliyotolewa na msemaji wa Jeshi hilo, David Misime imeorodhesha na kufafanua matukio kadhaa ya mauaji na utekaji, huku ikiacha kuhusisha matukio yaliyoibua mijadala, yakiwamo ya utekaji wa mwanaharakati na kada wa Chadema, Mdude Nyagali aliyechukuliwa na watu wasiojulikana wanaodaiwa kujitambulisha kuwa askari nyumbani kwake, Mtaa wa Ivanga, Kata ya Iwambi, jijini Mbeya.
Lingine ambalo halijaelezwa ni la kutekwa kwenye basi na baadaye kuuawa kwa kada wa chama hicho, Ali Kibao, la vijana watatu wa Chadema, Deusdedith Soka, Jacob Mlay na Frank Mbise ambao mpaka sasa hawajulikani walipo, wala lile la Shadrack Chaula aliyechukuliwa nyumbani Mbeya na gairi aina ya LandCruiser na hadi sasa hajaonekana.
Misime amesema kwa mujibu wa kifungu cha 117 cha Sheria ya Ushahidi Sura ya 6 marejeo ya mwaka 2022 na kifungu cha 161 cha Sheria ya Ndoa Sura ya 29 marejeo ya mwaka 2019, dhana ya mtu kuchukuliwa kuwa amekufa inapaswa kuthibitishwa na Mahakama baada ya miaka mitano kupita, kulingana na vielelezo na ushahidi utakaowasilishwa.
“Kumekuwapo kuripotiwa kwa taarifa katika vituo vya Polisi na nyingine katika mitandao ya kijamii zikijulisha kwamba mtu au watu fulani wamepotea, hawaonekani au wamekamatwa na watu waliojitambulisha kuwa askari wa Jeshi la Polisi,” imesema taarifa ya Polisi na kuongeza:
“Jeshi la Polisi linapopokea taarifa hizo, huanza uchunguzi kwa kukusanya ushahidi kutoka vyanzo mbalimbali ili kupata ukweli wa taarifa ya nini kilichotokea kwani hauwezi kusema moja kwa moja kuwa mtu aliyeripotiwa kupotea, kutekwa, kulazimishwa kupotea au kuuawa bila ya kumpata anayedaiwa kupotea na ushahidi wa kuthibitisha taarifa hiyo ya nini kilichomtokea, kama alitendewa uhalifu ni nani wahusika, kulingana na sheria, kanuni na taratibu.”
Kuhusu matukio yote yaliyoripotiwa yakihusisha watu kupotea, Misime amesema uchunguzi bado unaendelea hadi pale ukweli utakapopatikana.
Jeshi hilo limewataka ndugu, jamaa na marafiki wa watu hao kuendelea kuwa watulivu wakati vyombo vya dola vikiendelea na uchunguzi wa matukio hayo.
“Ikumbukwe kitendo cha kusambaza taarifa za uongo ni kinyume cha sheria kwa mujibu wa kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao namba 14 ya mwaka 2015 na adhabu yake ni kulipa faini ya kiasi cha fedha kisichopungua Sh5 milioni au kifungo gerezani kisichopungua miaka mitano au vyote kwa pamoja,” imesema taarifa ya Polisi.