Masharti mapya meli za kimataifa zenye usajili wa Tanzania mbioni

Unguja. Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA) imetangaza kuwa, licha ya mafanikio ya kusajili jumla ya meli 973 za kimataifa chini ya bendera ya Tanzania, sasa inakusudia kuweka masharti maalumu kwa wamiliki wa meli hizo.

Miongoni mwa masharti hayo ni kuhakikisha kila meli iliyosajiliwa kwa bendera ya Tanzania inamwajiri angalau baharia mmoja mzawa, ili kuhakikisha Watanzania wananufaika moja kwa moja na usajili huo.

Hayo, yameelezwa leo Jumatano Juni 18, 2025 na Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo, Mtumwa Said Sandal wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi za Habari Maelezo Zanzibar.

“Mamlaka hii imesajili meli 973 za kimataifa na ina mpango wa kuweka masharti maalumu kwa meli yoyote itakayosajiliwa kwa bendera ya Tanzania, lazima ichukue baharia mmoja nchini ili kufaidika,” amesema Mtumwa.

Pia, mkurugenzi huyo amesema mamlaka hiyo imesajili meli 86 za ndani kati ya hizo 73 za mizigo na 13 za abiria.

Mbali na hayo, amesema kuwa mamlaka hiyo ina mkakati wa kufungua chuo cha ubaharia kisiwani Zanzibar, kwa lengo la kuongeza idadi ya mabaharia wa ndani, kufuatia uhitaji mkubwa unaotokana na ongezeko la meli zinazosajiliwa chini ya bendera ya Tanzania.

Amesema kuwa kwa sasa kuna jumla ya mabaharia 4,441 waliosajiliwa, na idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka hadi kufikia 6,000 baada ya kuanzishwa kwa chuo cha ubaharia Zanzibar. Chuo hicho kinatarajiwa kuanza rasmi kutoa mafunzo mwakani.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari Zanzibar (ZPC), Akif Ali Khamis amesema kuwa ujenzi wa bandari sita pamoja na miundombinu ya mafuta na gesi unatarajiwa kugharimu Dola 733 milioni za Marekani, sawa na takriban Sh2 trilioni.

Ameeleza kuwa fedha hizo zinalenga kuimarisha bandari za Zanzibar kwa madhumuni ya kufungua fursa za kiuchumi na kuongeza ufanisi katika sekta ya usafirishaji.

Khamis amesema kwa sasa, ZPC tayari imeingia mikataba ya uwekezaji katika bandari yenye thamani ya Dola 400 milioni, sawa na Sh1 trilioni.

Katika hatua nyingine, Khamis amesema kuwa ifikapo mwaka 2030, bandari zote za Zanzibar zitakuwa na uwezo wa kuhudumia hadi kontena 400,000 kwa mwaka, ikilinganishwa na uwezo wa sasa wa kuhudumia kontena 100,000 kwa mwaka hadi kufikia mwaka 2025.

Aidha, amesema kuwa shirika hilo linaendelea na ujenzi wa bohari kubwa ya kisasa ya mafuta yenye uwezo wa kuhifadhi hadi lita 60 milioni.

Kwa mujibu wa Khamis, bohari tatu zilizopo katika eneo la Mtoni zina uwezo wa kuhifadhi jumla ya lita 15 milioni pekee, kiwango ambacho hakikidhi mahitaji ya mafuta kwa jamii, hususan nyakati za uhaba wa bidhaa hiyo kutoka nchi jirani.

Kwa upande mwingine, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar, Seif Abdalla Juma, amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepanga kujenga jengo la nne la abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume.

Amesema ujenzi huo ni sehemu ya mkakati mpana wa kuimarisha miundombinu ya usafiri wa anga ili kuendana na ongezeko la idadi ya wasafiri wanaotumia uwanja huo.

Juma amesema kuwa hatua hiyo inalenga kuongeza uwezo wa kuhudumia abiria pamoja na kuboresha huduma za kisasa za uwanja wa ndege, ili kuifanya Zanzibar kuwa kitovu bora cha usafiri wa anga katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini.

Amesema uboreshaji huo pia unatarajiwa kuchochea ukuaji wa sekta ya utalii na uchumi kwa ujumla visiwani humo.

Related Posts