:::::::
Na Daniel Limbe, Torch Media
SERIKALI mkoani Kagera imedai kufarahishwa na matumizi mazuri ya fedha za umma katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye halmashauri ya wilaya ya Biharamulo, hali iliyo sababisha kuendelea kupata hati safi katika ukaguzi wa Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG) mwaka 2023/24.
Pongezi hizo zimetolewa na mkuu wa mkoa wa Kagera, Fatma Mwasa,wakati akizungumza kwenye kikao maalumu cha Baraza la madiwani wa halmashauri hiyo kilicholenga kupitia, kujadili na namna zilivyojibiwa hoja zilizoibuliwa na CAG.
Katika mazungumzo yake mkuu huyo wa mkoa, amesema wilaya hiyo imefanya vizuri sana katika matumizi ya fedha za umma na kwamba jitihada zaidi zinapaswa kuendelea kufanywa ili kupunguza wingi wa hoja kwa mwaka ujao wa 2024/25.
Kadhalika ametumia fursa hiyo kutoa maelekezo ya kiserikali ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kila kituo cha kutolea huduma za afya wilayani humo kinakuwa na mtumishi mmoja ambaye atajikita zaidi katika uhakiki wa fedha za Bima ya afya ili kunusuru mapungufu yanayojitokeza na kuisababishia halmashauri hasara ya kutolipwa fedha zake na serikali kuu.
Pia hakusita kuipongeza kwa kufanya vizuri sana katika mapokezi ya mwenge wa uhuru 2024 ambapo halmashauri hiyo ilifanikiwa kushika nambari ya tatu kitaifa na ya pili katika mkoa wa Kagera.
Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Innocent Mkandala, amesema siri ya mafanikio hayo ni Ofisi yake kufanya kazi kwa uwazi, ushirikiano wa watumishi wa halmashauri hiyo, madiwani pamoja na wananchi ambao wamekuwa wakitoka ushirikiano mkubwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo huko vijijini.
Aidha amesema wanaendelea kuufanyia kazi ushauri na maelekezo yote yanayotolewa na viongozi mbalimbali wa serikali ili kuhakikisha halmashauri hiyo inaendelea kufanya vizuri katika ukusanyaji na utumiaji wa mapato yanayotokana na vyanzo vya ndani,wahisani pamoja na ruzuku kutoka serikali kuu.
Hatua hiyo ni mafanikio ya halmashauri hiyo kupata hati safi kwa miaka mitatu mfululizo kutokana na ripoti ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo,Leo Rushahu,amempongeza Mkurugenzi wa halmashauri hiyo,kwa kuendelea kusimamia vyema maelekezo yaliyokuwa yakitolewa na madiwani wa halmashauri hiyo ikiwa ni pamoja na kutozalisha madeni mapya badala yake kujikita katika kulipa yaliyopo.
Licha ya kuwa hivi karibuni serikali itakwenda kuyavunja mabaraza ya madiwani kote nchini kutokana na maelekezo yaliyotolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mohamed Mchengerwa, ili kupisha Uchaguzi mkuu wa Rais,Wabunge na Madiwani, Rushahu amesema wanayo matumaini makubwa ya kurejea kwenye nafasi zao za udiwani kutokana na miradi mingi ya maendeleo iliyotekelezwa kwenye kata zao.
“Hatuwezi kuacha kumpongeza rais wetu mpendwa Samia Suluhu Hassan kwa jinsi alivyoturahisishia kazi kwenye kata zetu, maana halmashauri yetu imepokea fedha nyingi sana za maendeleo ambazo hazikuwa kutolewa tangu kupatikana kwa uhuru wa nchi yetu”amesema Rushahu.
Baadhi ya Madiwani wa halmashauri hiyo,wameipongeza serikali kwa kuendelea kutoa ushirikiano wa dhati kwa halmashauri hiyo ikiwa ni pamoja na ushauri mwema iliyosababisha halmashauri hiyo kuendelea kupata hati safi mfululizo
Mwisho