Kaizer yaingilia dili la Tau Yanga

MAMBO yanaendelea kuwa mambo katika viunga vya Jangwani wakati huu ambapo Yanga imeshaanza kufanya biashara ikifanikiwa kumuuza aliyekuwa kiungo wake, Stepahie Aziz KI kwenda Wydad Casablanca ya Morocco ambako chama lake jipya linashiriki pia fainali za Kombe la Dunia la Klabu.

Yanga ilifanya biashara na Wydad hivi karibuni, lakini ikiwa haijapoa kwani inadaiwa kwamba iko katika mazungumzo na timu mbalimbali za nje ya nchi juu ya straika wake, Clement Mzize anayetakiwa kwa udi na uvumba na timu za Kaskazini mwa Afrika, na hivyo lolote linaweza kutokea kuanza sasa.

Lakini wakati unawaza juu ya hilo, mastaa wengine kikosini pia huenda wakapigwa bei, huku nyuma Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini imeingilia harakati za Yanga iliyokuwa ikimnyemelea mshambuliaji nyota wa Bafana Bafana, Percy Tau ambaye kwa sasa ni mchezaji huru, jambo linaloweka ugumu kwa Wananchi kumnasa nyota huyo aliyewahi kutikisa akiwa na Al Ahly ya Misri.

Yanga ilivutiwa na Tau baada ya kujua hana timu tangu alipoachana na Qatar SC, Januari, mwaka huu, lakini sasa Kaizer imeonyesha nia ya kumsajili ikiahidi kumlipa mshahara wa zaidi ya Sh60 milioni kwa mwezi.

Akizungumza na kipindi cha Marawa Sports Worldwide kupitia Kituo cha Redio 94.7, Tau mwenye umri wa miaka 31 alifichua kuwa yupo tayari kurejea Ligi Kuu Afrika Kusini, lakini kwa masharti maalumu.

“Sitaki kudai kitu ambacho najua klabu haiwezi kunipa. Mimi ni mchezaji mwenye mantiki katika makubaliano ya mikataba,” alisema Tau.

Pia alisema iwapo Chiefs au timu yoyote ya Afrika Kusini itampa mkataba wa miaka miwili ukiwa na chaguo la kuongeza mwaka mmoja, basi yupo tayari kurudi nyumbani kucheza soka la ushindani akiwa na moja ya vigogo.

“Kama Kaizer watanipa R450,000 (zaidi ya Sh60 milioni) kwa mwezi kwa miaka miwili na chaguo la mwaka wa tatu, ni ofa ya kuvutia sana,” alisema Tau alipohojiwa. “Lakini siwezi kufunga milango kwa timu yoyote ninaweza kucheza Orlando Pirates, SuperSport United au hata Stellenbosch. Nitafuata klabu inayokuja na mkataba mzuri.”

Yanga ambayo ipo kwenye harakati za kuboresha kikosi kwa ajili ya msimu ujao, ilikuwa imeanza mawasiliano ya awali kumshawishi Tau, lakini hatua hiyo huenda ikayeyuka endapo Kaizer itaharakisha dili hilo.

Nyota huyo alisema ana mapenzi na klabu yake ya zamani ya Mamelodi Sundowns, lakini kama haitakuwa tayari kumrejesha na Kaizer au timu nyingine imtupie ndoano, basi hatakataa

“Sundowns ni klabu niliyowahi kuichezea, nilishinda nayo, ninawapenda mashabiki wake lakini nisiporudi huko basi siyo kosa langu,” alisema.

Hadi sasa, Tau amekuwa akihusishwa na klabu nyingi baada ya kuachwa na Qatar SC, lakini kwa mujibu wa mahojiano yake, anaipa Kaizer nafasi ya kwanza kutokana na namna ilivyoanza mazungumzo kwa uwazi.

Mchezaji huyo mwenye jina kubwa barani Afrika, alikumbusha mafanikio yake ya nyuma akisema: “Nilikutana na changamoto Ulaya na Afrika, lakini bado nina kiu ya kucheza na kushindana. Nataka kurejea kwenye kiwango bora kuelekea AFCON 2025 nchini Morocco.”

Percy Tau alipata umaarufu mkubwa akiwa Mamelodi Sundowns kabla ya kuuzwa Brighton ya England 2018/19. Akiwa Brighton alitolewa kwa mkopo Club Brugge na Anderlecht za Ubelgiji, kabla ya kurejea Januari 2021.

Baadaye alijiunga na Al Ahly ya Misri ambapo alitwaa mataji mawili ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Related Posts