Alhamisi iliyopita, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba alisoma Bajeti Kuu ya Serikali. Kwa kawaida bajeti hii hutanguliwa na bajeti za wizara. Bajeti kuu inakuwa na mambo kadha wa kadha ikiwemo mapendekezo ya sheria ya fedha ambayo inatoa unafuu ama kuweka kodi au tozo mpya kwenye sheria za sasa (au za mwaka huu wa fedha unaoisha Jun 30).
Bajeti ya Serikali ndio bajeti kubwa kuliko bajeti zote nchini na inatoa mwelekeo wa uchumi pamoja na maendeleo ya nchi. Bajeti iliyosomwa inaonyesha mwelekeo kuleta unafuu na fursa za kibiashara na kiuchumi kwa wananchi na wawekezaji wa ndani. Kwa kuzingatia hotuba ya bajeti, tunategemea kama itapitishwa na Bunge na sheria ya fedha mpya kuwa ni sheria, nafuu na fursa zifuatazo zinaweza kuchukuliwa kwa manufaa:
Mosi, unafuu kwa familia ama watu binafsi. Bajeti inatoa unafuu kwa wakulima kwenye kutoa unafuu wa kodi kwenye viatilifu pamoja na pembejeo, pia viwanda vya mbole. Bajeti pia inatoa unafuu wa kodi kwa viwanda vya ujenzi ikiwemo viwanda vya kutengeneza nondo, mabati na sementi.
Tunategegemea ushindani kwenye viwanda hivi na hivyo kushuka kwa bei ya vifaa vya ujenzi. Bajeti pia inatoa unafuu kwenye viwanda vya sabuni. Kwa sabuni ni bidhaa inayotumiwa na wananchi wengi na hivyo ni matarajio kuwa kutakuwa na unafuu wa bei wa sabuni hasa zinazozalishwa ndani ya nchi.
Bajeti inatarajiwa kunufaisha watu waliokuwa wanapata Kiwango cha chini cha mshahara kwani serikali imeongeza kima cha chini cha mshahara kwa Watumishi wa Umma kwa asilimia 35.1 ambapo kwa ongezeko hili sasa kima cha chini kitapanda kutoka Sh370,000 hadi Sh500,000 kuanzia Julai 2025. Hii itaongeza fedha kwenye mzunguko.
Pili, unafuu wa kodi.Bajeti itaangazia uboreshaji wa mazingira ya biashara kupitia kupunguzwa kwa mzigo wa kodi na urahisishaji wa mifumo ya ushuru. Kodi kadhaa zimepunguzwa ambazo zinaweza kuchochea uwekezaji lakini pia kuleta unafuu kwa mtu mmoja mmoja. Mathalani kodi ya ushuru wa hoteli, kupunguzwa kwa kodi ya ya usajili ya pikipiki na hivyo kurahisisha usafirishaji, kupunguzwa kwa gharama za miamala ya kifedha kati ya benki na makampuni yanayotoa huduma za kifedha kama M-Pesa na AirtelMoney.
Tatu, ongezeko la Uwekezaji kwenye kilimo na viwanda.Tunategemea kukua kwa sekta ya kilimo na viwanda kwa kuzingatia mipango ya kuongeza tija na ufanisi wa uzalishaji. Hii inaweza kuwa fursa kwa wawekezaji kuingia kwenye uzalishaji wa mbegu bora, mitambo ya usindikaji wa mazao, na biashara ya usambazaji wa chakula.
Viwanda vya mazao ya kilimo pia vinakuwa na kipaumbele, hasa kwa kuongeza thamani ya mazao kama kahawa, chai, na korosho. Serikali imepunguza kodi kwenye vifungashio vya mazao na bidhaa mbali mbali na hivyo ni mategemeo kuwa uwekezaji wa viwanda unaweza kuwa na tija zaidi.
Viwanda vingine vinavyonufaika na bajeti hii ni nivwanda vya fenicha, uzalishaji wa siagi, viberiti, vifaa vya plastiki, nk. Hii inaweza kuwa fursa kwa wawekezaji kuingia kwenye viwanda vidogo na vikubwa vya usindikaji wa mazao ya kilimo.
Tatu, uwekezaji kwenye hati funga za Serikali.Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana inatarajia kutoa elimu kwa umma kuhusu fursa za masoko ya mitaji kwa watu milioni 15, pamoja na kuongeza idadi ya wataalamu wa masoko ya mitaji kwa asilimia 10.
Ongezeko hili lina maana kuwa kutakuwa na mwako wa uwekezaji na pia ni fursa kuwekeza kwenye soko la hisa na mitaji. Serikali inatarajia kukopa jumla ya Sh14.95 trilioni kupitia vyanzo vya ndani na nje, ambayo inaweza kuwa fursa kwa wawekezaji wa mfuko wa pensheni na taasisi za kifedha. Kuna fursa ya kuwekeza kwenye hati fungani (Treasury Bills na Bonds) za Serikali kwa wawekezaji wanaotafuta mavuno thabiti na kiwango cha chini cha hatari.
Nne, uwekezaji kwenye Soko la Hisa na bondi. Soko la Hisa (DSE) na bondi za serikali zinaweza kuwa fursa nzuri kwa wawekezaji wanaotafuta mavuno ya muda mrefu. Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana inatarajia kushirikiana na wadau wa masoko ya mitaji katika kubuni na kuanzisha bidhaa mpya sita. Aidha, Kampuni ya Uwekezaji wa Pamoja (UTT-Amis) inatarajia kuongeza rasilimali za mifuko ili kuendelea kusaidia wawekezaji hasa wadogo wanaopanga kuwekeza.
Tano, kujiandikisha kwenye Mfumo wa Ununuzi wa Umma (NeST).Wafanyabiashara wadogo na wakubwa wanaweza kujiandikisha kwenye mfumo NeST wa Serikali ili kushiriki katika zabuni za ununuzi wa vifaa na huduma kwa sekta ya umma. Hii inaweza kuwa fursa kwa wafanyabiashara kupata mikataba thabiti na mapato ya uhakika kupitia manunuzi ya serikali ambayo yanatarajiwa kufanyika ili kukidhi matakwa na matarajio ya bajeti hii.
Bajeti ya 2025/2026 ni bajeti pia inayoangalia mwaka wa uchaguzi na kuhitimisha miaka mitano ya mpango wa taifa wa maendeleo wa tatu. Ni muhimu kuangalia fursa mbali mbali zinazoweza kujitokeza kwenye sekta yako, na hata mtaani kwako. Ni vema kuchambua mipango hii kwa undani na kuchukua hatua za kufaidika na mazingira mazuri ya kibiashara yanayotolewa kupitia hotuba ya Waziri wa Fedha.