Mashambulizi yaliyofanywa na Jeshi la Israel (IDF) yamesababisha vifo vya raia 72 eneo la Gaza, wakiwemo 29 waliokuwa wakisubiria magari yenye misaada ya kibinadamu.
Wizara ya Afya eneo la Gaza imethibitisha kuuawa kwa Wapalestina hao katika mashambulizi ya Israel yaliyofanyika alfajiri ya leo Alhamisi Juni 19, 2025.
Kwa mujibu wa Reuters, mauaji ya raia hao yametokea katika mtaa wa Salah al-Din eneo la Netzarim na Zeitoun Gaza nchini humo.
Kundi la Hamas limelaani kitendo cha Israel kushambulia raia na watumishi wa shirika la kutoa misaada ya kibinadamu la Palestina kinyume na sheria za kimataifa.
“Mwendelezo wa mauaji ya kimbali dhidi ya raia, kuwalenga watu ambao wanaangamia kwa kukosa chakula, uhalifu dhidi ya binadamu ni miongoni mwa mambo ambayo yameendelea kutekelezwa na Israel kwa wapalestina.”
“Huu unyama dhidi ya binadamu ni miongoni mwa mambo ambayo yamekuwa yakifanywa na Israel kwa wakazi wa Gaza. Tunalaani unyama huu,” imeeleza taarifa ya Hamas.
Ilipoulizwa na Reuters kuhusu madai hayo, Serikali ya Israel imesema inaendelea kufuatilia ukweli wa madai ya vifo hivyo bila kuweka wazi iwapo imehusika kutekeleza mashambulizi hayo.
Awali, jana Al Jazeera iliripoti kuwa kuna miili ya watu 20 iliyokuwa imemiminiwa risasi Kaskazini mwa Gaza na wanaodaiwa kuwa askari wa IDF. Tayari maofisa wa msalaba mwekundu wameichukua miili hiyo na kuifanyia maziko.
Mkazi wa Deir el-Balah Gaza nchini humo, Ahmed Ghaben amesema miongoni mwa waathiriwa wa ukatili huo ni mtoto wa kaka yake ambaye aliuawa akienda kuchukua msaada wa chakula kwa ajili ya familia yake.
“Alikwenda asubuhi ya leo kuchukua msaada wa chakula bahati mbaya tumepokea mwili wake akiwa ameshauawa,” amesema Ghaben.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya nchini Palestina imesema watoa huduma ya dharura zaidi ya 300 wameuawa katika mashambulizi ya Israel tangu kuanza mzozo huo Oktoba 7, 2023.
Takwimu zinaonyesha wapalestina zaidi ya 59,000 wameuawa katika mashambulizi ya Israel eneo la Gaza huku zaidi ya 110,000 wakijeruhiwa. Hata hivyo, raia zaidi ya 1,200 wa Israel waliuawa wakati Hamas ilipovamia Israel huku ikiwachukua zaidi ya mateka 251.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari