Mwanza. Achana na wanaokimbia mchaka mchaka kutoka huku kwenda kule, wanaocheza muziki, wanaoimba nyimbo za kizalendo mithiri ya vijana wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), kitakachokuacha hoi ni idadi ya watu waliofurika eneo la mkutano kusubiri neno la uzinduzi wa Daraja la JP Magufuli.
Hayo ni machache kati ya mengi yanayoendelea katika eneo la Kigongo-Busisi, ikiwa ni shamrashamra za wananchi wa Mwanza na maeneo ya jirani, wanaposubiri tukio la uzinduzi wa Daraja la JP Magufuli umaofanyika leo, Alhamisi Juni 19, 2025.
Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kulizindua daraja hilo leo, ikiwa ni sehemu ya ratiba ya ziara yake ya kikazi katika mikoa ya Simiyu na Mwanza.
Jua linalowaka katika eneo hilo, halikukwaza sherehe za mtindo mbalimbali zinazoendelea kabla ya uzinduzi rasmi wa daraja hilo, vijana wanazunguka huku na kule wakisherehekea.
Nyimbo za kisukuma na zile za kizalendo zinasikika kutoka katika vinywa vya vikundi mbalimbali vya vijana, wakishindana kuonyesha furaha kabla ya tukio rasmi la uzinduzi huo.
Tangu saa 3:30 asubuhi, tayari eneo la uwanja unakofanyika mkutano baada ya uzinduzi wa daraja hilo, kulishafurika makundi ya wananchi, kila mmoja akionyesha furaha ya namna yake.
Wapo wanaocheza muziki unaopigwa, wapo wanaokimbia mchakamchaka, wengine wameamua kuimba nyimbo mbalimbali, kadhalika wapo wanaozunguka kwenye magari wakionyesha mbwembwe za kila aina.
Isingekuwa rahisi kuhesabu idadi ya watu waliopo katika eneo la mkutano na wale wanaoendelea kuingia katika viunga hivyo, kwa maneno mafupi kumefurika.
Daraja hilo linazinduliwa na Rais Samia baada ya kukamilika kwa gharama ya zaidi ya Sh700 bilioni.
Utekelezaji wa mradi huo umefanywa na mkandarasi, China Civil Engineering Construction Corporation na China Railway 15 Bureau Group Corporation; na ulifikia asilimia 25 wakati Rais Samia anaingia madarakani Machi 19, 2021 baada ya kifo cha mtangulizi wake, John Pombe Magufuli.
Daraja hilo lina njia mbili za magari zenye upana wa mita 7 kila upande na njia za waenda kwa miguu kila upande yenye upana wa mita 2.5 na maegesho ya dharura yenye upana wa mita 2.5 kila upande.
Ikipita juu ya maji ya Ziwa Victoria kuunganisha eneo la Kigongo Wilaya ya Misungwi na Busisi Wilaya ya Sengerema, daraja la JPM lina nguzo za 804, kitako cha nguzo za madaraja 65, nguzo kuu 67 zikiwemo nguzo kuu 3 na nguzo za mlalo 806.
Hili ndilo daraja lenye upenyo mkubwa zaidi ya madaraja yote nchini kwa kuwa na upenyo wa mita 120 kati ya nguzo zake kuu kuruhusu meli na vyombo vingine vya usafirishaji majini kupita bila shida yoyote.
Kuanza kutumika kwa daraja hilo, kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, kutasitisha matumizi ya vivuko katika eneo la Kigongo-Busisi.
Amesema vivuko vitatu vilivyokuwa vinatumika katika eneo hilo vitapelekwa visiwa vingine ikiwemo Kome na Ukerewe, hivyo wananchi wa maeneo hayo watanufaika na ujenzi wa daraja hilo.
Mathalan, wakazi wa visiwa vya Kome na Ukerewe, amesema, watanufaika kwa kupelekewa vivuko vilivyokuwa vinatumika Kigongo-Busisi, hivyo adha ya uhaba wa vivuko inakwenda kuwa historia kwao.
Mtanda amesema hilo linakwenda sambamba na kuwaepusha wananchi na gharama ya Sh400 walizokuwa wanalipa kila wanapotumia kivuko, sasa watavuka kupitia darajani bila malipo.
“Kwa siku tulikuwa tunakusanya Sh5.2 milioni zinazotokana na nauli za wananchi kutumia vivuko. Kwa mwaka ilikuwa kama Sh1.8 bilioni. Fedha hizi zote zinakwenda kubaki kwa wananchi na wakaendelea kuzitumia kwa mahitaji mengine,” amesema.
Endelea kufuatilia Mwananchi