Samia asisitiza amani akizindua mradi wa maji Lamadi

Mwanza. Rais Samia Suluhu Hassan, amewahimiza wakazi wa Lamadi kudumisha amani na utulivu ili kuiwezesha Serikali kuendelea kuwahudumia ipasavyo na kulisaidia Taifa, kusonga mbele katika kujitegemea kiuchumi.

Akizungumza na wananchi mara baada ya kufungua mradi wa maji Lamadi Wilaya ya Busega mkoani Simiyu leo Alhamisi Juni 19, 2025, Rais Samia amesema Serikali imejitahidi kupeleka huduma zote za kijamii eneo hilo, hivyo wana wajibu wa kufanya uzalishaji na kuhakikisha amani na utulivu.

Ikumbukwe, Agosti 21, 2024 yalitokea maandamano eneo la Lamadi na kusababisha vurugu, uharibifu wa mali na kifo cha mwanafunzi, waandamanaji wakidai ukimya wa Jeshi la Polisi kushughulikia matukio ya kupotea watoto ndiyo chanzo cha kuandamana.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akifungua mradi wa Maji na Usafi wa Mazingira wa Lamadi, Wilayani Busega wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi mkoani Simiyu tarehe Juni 19, 2025.



Akiendelea kuzungumza na wananchi hao, Rais Samia amesema; “Wito wangu kwenu, pamoja na furaha yangu na faraja nimeweza kuwapatia maji na huduma za kijamii, tuweke amani na utulivu ndani ya nchi yetu ili makubwa zaidi tuweze kuyafanya.”

Amewaambia Serikali yao ipo kuhakikisha maendeleo ya wananchi yanapatikana, ustawi wa afya na wa familia unaonekana na ndio maana wamejitahidi kuhakikisha huduma zote za kijamii zinapatikana.

“Nadhani Lamadi mmeona ujenzi wa shule mpya na zile za zamani kupewa hadhi, ujenzi wa vituo vya afya na hospitali ya wilaya, mmeona umeme ukisambaa mijini na vijijini, lakini pia mmepata maji hapa. Kwa hiyo kazi yetu sasa kama wananchi kwa kuwa tuna huduma zote za kijamii, kuchapa kazi kuongeza uzalishaji wa chakula, mazao ya biashara na chakula ili familia na jamii ipate nguvu na tuweze kufanya maendeleo zaidi.”

“Si mmesikia leo tunaenda kufungua daraja kubwa? Daraja la sita kwa Afrika. Haya yote yamewezekana kwa sababu nchi yetu imetulia, kuna utulivu wa kisiasa, tunakusanya fedha ndani na tunaweza kufanya maendeleo yetu. Wito wangu wa kwanza ni amani na utulivu, wa pili kuchapa kazi kwa bidii ili tuzalishe zaidi, tukusanye fedha zaidi, tufanye maendeleo zaidi na Tanzania isimame kama nchi inayojitegemea.”

Amewataka wakazi hao wa Lamadi kujitokeza kwa wingi Oktoba na kukichagua Chama cha Mapinduzi (CCM).

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Kenani Kihongosi amesema katika mkoa huo kuna baadhi ya watu wanahamasisha wananchi kuvunja amani kwa makusudi akiwataka kutoshiriki uvunjifu huo ikiwa ni pamoja na maandamano.

“Msikubali kwa namna yoyote ile tukavunja mshikamano uliopo wilaya hii na mkoa wetu wa Simiyu. Kuna baadhi ya watu wenye nia ovu, kwa makusudi tumeshuhudia wakihamasisha uvunjifu wa amani twendeni tukalinde amani yetu, amani ndiyo msingi wa maendeleo. Tusiende kushiriki vurugu za aina yoyote,” amesema.

Awali akitoa taarifa ya mradi huo, Waziri wa Maji,  Jumaa Aweso amesema utekelezaji wake umefanya hali ya upatikanaji wa maji kuongezeka kutoa asilimia 23 hadi 97, akisema kulikuwa na changamoto wakati wa utekelezaji wake, lakini wakahakikisha mradi huo unakamilika.

Naye, Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mwajuma Waziri amesema eneo la chujio la mradi wa maji Lamadi unatekelezwa kupitia ‘satelite tone program’ ambao ulikuwa unahusisha miji ya Lamadi, Misungwi na Magu kwa gharama ya Sh43 bilioni katika maeneo hayo, huku kwa eneo la Lamadi ukigharimu Sh12.8 bilioni.

Amesema miundombinu iliyojengwa pamoja na chujio la kuchujia maji ni pamoja na bomba la urefu wa mita 420, kipenyo cha mita 400 linalotoa maji hayo Ziwa Victoria huku bomba la kipenyo cha milimita 250 ambalo lipo umbali wa milimita 470 kwenye chujio likiyasukuma maji hayo baada ya kuchakatwa.

Amesema chanzo cha kutibu maji katika mradi huo kina uwezo wa kuzalisha lita milioni 400 kwa siku huku pampu ya kusukuma maji iliyojengwa eneo hilo ikiwa na uwezo wa kusukuma maji umbali wa kilomita tano kutoka eneo la mradi.

“Kuna tenki limejengwa la ujazo wa lita 400,000 lipo kwenye mnara wa mita 21, sasa hilo tenki ndiyo linahudumia eneo la Mkula hapa Lamadi Kata ya Lutubiga. Jumla ya watu wanaohudumiwa na huu mradi ni 85,000 sawa na asilimia 97 ya upatikanaji wa maji,”amesema.

Katika hatua nyingine, Rais Samia ameweka jiwe la msingi katika mradi wa mabadiliko ya tabianchi unaogharimu zaidi ya Sh440 bilioni, ambao awamu ya kwanza utahusisha miji ya Busega, Bariadi na Itilima, ambapo awamu ya pili utatekelezwa Maswa na maeneo mengine.

Amefafanua, mradi huo una vipengele vitano kikiwemo cha kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya kujenga uwezo (capacity building), huduma ya maji safi na salama, masuala ya kilimo, mbegu bora na uoto wa asili, masuala ya maji taka na usafi wa mazingira na kipengele cha mwisho ni kuwajengea uwezo watumishi wa Wizara ya Maji.

Amesema mradi huo utahusisha ujenzi wa mashamba darasa 212, ukarabati wa skimu 14 za umwagiliaji zenye mabwawa 11 ambayo yatafanyiwa maboresho.

“Usafi wa Mazingira tunajenga vyoo bora, shule, masoko na baadhi ya nyumba watapewa vifaa kama watakuwa tayari kujenga..kutakuwa na ujenzi wa mabwawa matatu hapa Nyashimo, Bariadi na Itilima pamoja na ununuzi wa magari,” amesema.

Ameongeza kuwa kipengele cha huduma ya maji safi na salama kitahusisha miji ya Busega, Bariadi na Itilima pamoja na vijiji 103.

Related Posts