Dar es Salaam. Katika kusherehekea Siku ya Mtoto wa Afrika inayoadhimishwa Juni ya kila mwaka,Benki ya CRDB imetembelea wodi ya watoto katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na kutoa misaada mbalimbali kwa wazazi.
Licha ya ziara hiyo iliyofanyika leo Juni 19, 2025 katika wodi ya watoto njiti hospitalini hapo, uongozi wa CRDB pia imetumia nafasi hiyo kumuaga aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Profesa Mohammed Janabi ambaye sasa ni Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika.
Akizungumza kwenye ziara hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema siku zote wamekuwa wakitoa elimu ya fedha na kuwahamasisha wananchi kutumia huduma za benki tangu wakiwa wadogo, ili kujenga msingi imara wa uchumi binafsi siku zijazo.

“Katika wiki hii ya kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika tumeona ni vyema kuja kuzungumza na wazazi hapa Muhimbili. Tunasisitiza elimu ya fedha ianze kutolewa tangu kwa watoto wadogo na ili kuliweka suala hili kwa vitendo, watoto wote waliopo hapa tutawafungulia Akaunti ya Junior Jumbo yenye Sh10,000 ya kuanzia, ili mzazi akitoka hapa akaendeleze utaratibu wa kumtunzia mwanaye fedha zitakazomsaidia siku zijazo,” amesema Nsekela.
Kwa akiba yoyote iliyomo kwenye Akaunti ya Junior Jumbo, CRDB hutoa riba ya mpaka asilimia tano kwa mwaka hivyo, kumpa uhakika mzazi au mlezi pindi mwanaye atakapoanza shule au atakapokuwa na mahitaji mengine yanayohitaji fedha.
“Akiba inawekwa kidogokidogo ingawa matumizi yake huwa makubwa pale yanapojitokeza. Ni vizuri kujenga utamaduni wa kuhifadhi fedha kidogo ambazo kadri muda unavyoenda zitazidi kuongezeka hivyo kutosha kwa ada na matumizi mengine ya shule au kwa jambo jingine, ambalo mzazi atahitaji kulifanya kwa ajili ya mtoto wake,” amesema Nsekela.
Akimuaga Profesa Janabi anayetarajia kuondoa wiki ijayo kwenda kuanza majukumu yake mapya, Nsekela amemsifu kwa mikakati makini aliyonayo na kumuahidi kwamba, benki hiyo ipo tayari kushirikiana naye huko na anakokwenda.

“Nilikusikiliza wakati wa kampeni za kuomba uchaguliwe kuiongoa WHO. Ulikuwa na mikakati 10 lakini mimi nimevutiwa na mitatu ambayo ni utafiti na ubunifu, ubia pamoja na ufadhili wa huduma za afya kwa vyanzo vya ndani. Naamini vipaumbele hivi sio tu vitazifaa nchi zote 47 utakazokuwa unazihudumia bali vinatoa nafasi kwetu sekta binafsi kushiriki zaidi kuimarisha huduma za afya katika mataifa yetu, tutashirikiana nawe,” amesema Nsekela.
Kwa upande wake, Profesa Janabi ambaye ameimarisha ufanisi huduma hospitalini hapo tangu alipoteuliwa mwaka 2022, ameishukuru CRDB kwa kwenda kumuaga akisema ni kampuni ya kwanza kufanya hivyo.
“Uhusiano wangu na benki hii ni wa muda mrefu. Tangu nilipokuwa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) tulikuwa pamoja mkitusaidia kugharimia matibabu ya watoto. Nafurahi mmenikumbuka leo na kuja kuniaga,” amesema Profesa Janabi.
Akitarajiwa kuondoka wiki ijayo, Profesa Janabi anaiacha Tanzania akikumbukwa kwa utoaji wake wa elimu kupitia mitandao ya kijamii jambo lililoongeza hamasa ya kuepuka ulaji usiozingatia mahitaji ya kiafya unaoweza kumsababishia mtu magonjwa yasiyoambukiza.
Katika kuendeleza elimu hiyo, Profesa Janabi aliwaeleza wafanyakazi wa benki hiyo kuwa wangepata chakula cha mchana pamoja na akasisitiza: “Mlo wetu leo utakuwa tunda moja la apple (tufaa).”
Akiwa mkurugenzi mtendaji mwanzilishi wa JKCI, Profesa Janabi alifanikiwa kuifanya taasisi hiyo kuwa mahiri inayohudumia wagonjwa wa ndani na watokao nje ya nchi, hivyo kuacha mchango ambao hautosahaulika.
Balozi wa Akaunti ya Junior Jumbo, Paula Masanja aliwatia moyo wazazi waliojifungua watoto njiti na kuwahamasisha kuitumia akaunti hiyo kwa ajili ya watoto wao akisema, ni muhimu kuwa na akiba kwa ajili ya matumizi yatakayojitokeza wakati wowote.
“Nami ni mzazi mwenye mtoto mdogo kama ninyi. Akaunti ya Junior Jumbo ni nzuri, itumieni kwa ajili ya watoto wenu,” alihamasisha Paula.