Mwanafunzi mbaroni tuhuma mauaji ya mwenzake, mwingine ajinyonga

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linamshikilia mwanafunzi wa kidato cha nne wa Shule ya Mbweni Teta, Fastiel John (17), kwa tuhuma za kumshambulia mwenzake Sabra Mohamed na kumsababishia kifo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Alhamisi, Juni 19,2025 na Kamanda wa Kanda hiyo, Jumanne Muliro tukio hilo lilitokea jana Jumatano Juni 18, 2025 katika shule hiyo iliyopo Kawe  Kinondoni. Uchunguzi wa tukio hilo unakamilishwa kwa hatua zaidi za kisheria.

“Jeshi la Polisi linamshikilia mwanafunzi wa kidato cha nne wa Shule ya Mbweni Teta, Fastiel John (17), kwa tuhuma za kumshambulia mwenzake Sabra Mohamed na kumsababishia kifo,” amesema.

Katika hatua nyingine, Kamanda Muliro amesema jeshi hilo limeanza msako kwa wahalifu watano wanaotuhumiwa kwa tukio la unyang’anyi kwa kutumia nguvu maeneo ya Mbweni Ocenic Kinondoni katika hosteli ya wanafunzi wa ST, Joseph.

Tukio hilo limetokea leo Alhamisi Juni 19, 2025 ambapo wahalifu hao wakiwa na silaha za jadi walidaiwa walipora simu, laptop, calculator na redio ndogo nne za wanafunzi kwenye vyumba vyao.

Muliro amesema mbali na kupora vifaa hivyo, wahalifu hao waliwajeruhi wanafunzi watatu ambao walitibiwa hospitali na hali zao zinaendelea vizuri.

Aidha, taarifa hiyo imeeleza jana Jumatano, Juni 18, 2025 maeneo ya Majohe Rada mwanafunzi Sabitina Ramadhani (17), kidato cha tatu Shule ya Sekondari Gunda iliyopo Korogwe, mkoani Pwani akiwa likizo nyumbani kwao Majohe Rada alijinyonga kwa kutumia shuka aliyoifunga kwenye kenchi sebuleni kwao.

Polisi wamesema, umekutwa ujumbe wa maandishi eneo hilo. (hata hivyo, polisi hawakuuweka wazi ujumbe huo ulihusu nini).

Related Posts