Wawakilishi watakiwa kuendelea kudumisha amani, utulivu

Unguja. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amewataka wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuendelea kudumisha amani na utulivu katika majimbo yao wakati na baada ya uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba mwaka huu.

Pia, amesema Serikali haitamvumilia mtu au kikundi, taasisi na chama chochote cha siasa, kitakachoashiria uvunjifu wa amani huku akisisitiza haitosita kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria.

Hemed ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Juni 19, 2025 wakati akihutubia Baraza la Wawakilishi baada ya kukamilika shughuli zote zilizopangwa kufanyika Baraza la 10, mkutano wa 19 wa Baraza la wawakilishi, Chukwani Zanzibar.

“Serikali itaendelea kulinda na kudumisha amani kwa nguvu zote na haitamvumilia mtu au kikundi chochote, taasisi au chama chochote cha siasa kitakachoashiria uvunjifu wa amani yetu, Serikali haitosita kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria,” amesema Hemed.

Katika hotuba yake, Hemed amewasisitiza wawakilishi wanaporudi kwenye maeneo yao, wakasimamie na kudumisha amani jambo litakaloendelea sio tu kuwapa wao heshima, bali kuipa heshima kubwa Zanzibar kwa masilahi ya wananchi wake na Tanzania kwa jumla.


“Nimeamua kulisema hili ili isionekane leo tukitoka hapa ama baraza likifungwa basi tunaweza kufanya mambo mengine, bado uongozi wako utakuwepo hata ukikosa kuingia barazani utakuwa mwakilishi mstaafu na bado una wajibu wa kulinda heshima ya nchi yetu, una wajibu kulinda heshima ya viongozi wetu na una wajibu kulinda heshima ya wananchi wetu,” amesema Hemed.

 “Niwaombe pia, kwa kawaida wengi wetu humu ndani zitawekwa nia za kugombea majimbo, basi twende tukafanye kampeni za kistaarabu sana, utamaduni wa nchi yetu haupendezi, Wazanzibari na Watanzania sisi kwa sisi kutumia lugha isiyostahiki katika vikao hivi,” amesema.

Amewaomba wakalisimamie hilo na waache jaziba za vyama vya siasa bali wakatangulize masilahi ya Zanzibar kwanza.

“Kuna wale tunawaona ni watu, wanaweza kuharibu amani na utamaduni wetu, tuwe mstari wa mbele bila kujali itikadi za vyama na mambo mengine yote,” amesisitiza Hemed.

Katika hotuba yake hiyo, amesema wananchi na viongozi sambamba, wanapaswa kuheshimiana badala ya kudharauliana kwa sababu tu ya uchaguzi mkuu.

Hemed  amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) itaendesha uchaguzi mkuu wa saba tangu mfumo wa vyama vingi vya siasa urejee mwaka 1992.

Kiongozi huyo amesema kwa sasa, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), inaendelea vyema na maandalizi ya uchaguzi huo kwa kuweka miundombinu itakayowezesha kufanyika kwa uhuru, haki na uwazi.

Ili kufanikisha uchaguzi huu na chaguzi zijazo, kwa njia ya uhuru, haki na uwazi, amesema Serikali imejenga jengo jipya la kisasa ambalo limezingatia mahitaji yote ya shughuli za uchaguzi kabla, wakati na baada ya kufanyika uchaguzi.

Amesema jengo hilo limehusisha ofisi zenye huduma zote kwa ajili ya wajumbe na watendaji wa tume, ukumbi wa mikutano, studio ya kisasa ya kuandaa vipindi vya redio na televisheni na ghala lenye mifumo yote ya kiusalama na magari   ya kisasa yamenunuliwa na Serikali kwa ajili ya uchaguzi huo.

“Kwa jumla, maandalizi ya uchaguzi mkuu wa 2025, hivi sasa yamefikia hatua nzuri, zaidi ya   ya vifaa vya uchaguzi vimeshakuwa tayari,” amesema Hemed.

Amesema matarajio ya Serikali ni kupata viongozi watakaoongoza kwa awamu nyingine.

 “Naomba kuwaasa viongozi wa vyama vya siasa kuendelea kuhubiri na kulinda amani, hakika amani haina mbadala wake na tusifarakane kwasababu ya uchaguzi,”amesema Hemed.

Hemed amesema Serikali inajivunia mafanikio makubwa iliyoyapatikana katika kipindi hiki cha miaka mitano kwa kufanya mambo makubwa ya maendeleo katika sekta mbalimbali katika sekta ya elimu, afya, maji miundombinu na uwekezaji.

Amesema maboresho makubwa yaliyofanywa katika sekta ya elimu, yamesababisha kuongezeka kwa kiwango cha ufaulu wa wanafunzi wa kidato cha nne kutoka  mwaka 2021 hadi asilimia 82 mwaka 2024 na kidato cha sita kutoka  mwaka 2021 na kufikia mwaka 2024.

Amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha sekta ya kilimo ili kuongeza uzalishaji wa chakula na kuhakikisha ustawi wa wakulima na wafugaji.

“Serikali imekamilisha ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji maji katika mabonde saba yenye ukubwa wa hekta katika mabonde ya Kilombero, Cheju A na B, Kibokwa, Kinyasini, Chaani na Mlele,”amesema Hemed.

Uwezeshaji wananchi kiuchumi

Hemed amesema kupitia Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (ZEEA), Serikali  imetoa mikopo isiyo na riba yenye thamani ya Sh40.33 bilioni kupitia programu mbalimbali sawa na   ya malengo ya fedha iliyokusudiwa ya Sh46 bilioni.

Hemed amesema mikopo hiyo ilitolewa kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi zikiwamo uzalishaji, huduma za hoteli, ufugaji, ushoni, mafuta na gesi, huduma za chakula na makazi.

Katika kudumisha muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Hemed amesema wizara na taasisi za SMZ na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SJMT) zimekutana na kubadilishana uzoefu, utaalamu na maarifa katika kuwahudumia wananchi.

Amesema jumla ya hoja 15 za muungano zimeondolewa na kusainiwa kwa hati 13 zilizoondosha baadhi ya changamoto za muungano kupitia vikao vya sekretarieti ya kamati ya pamoja na vikao vya mawaziri.

Serikali kupitia Mfumo wa Sema na Rais (SNR), imepokea jumla ya malalamiko 49,099, kati ya hayo, 43, 035 yamepatiwa ufumbuzi na malalamiko mengine yanaendelea kufuatiliwa.

Akiahirisha shughuli za baraza hilo, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Zubeir Ali Maulid amesema baraza hilo litavunjwa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi Juni 23, 2025.

Related Posts