Wabunge wataka tozo za miamala zipunguzwe

Dodoma. Baadhi ya wabunge wamesema tozo kubwa zinazotozwa kwenye miamala ya kielektroniki kupitia benki na simu zimekuwa kikwazo kwa wananchi, hali inayochangia watu wengi kuepuka kutumia huduma hizo za kifedha.

Wabunge wamesema hayo leo, Juni 19, 2025, wakati wakichangia kuhusu Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2025/26, hali ya uchumi wa taifa kwa mwaka 2024, na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2025/26.

Akichangia mjadala huo, Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Kilumbe Ng’enda amesema lipo tatizo la wananchi kutopenda kupeleka fedha benki na kuwa kati ya Sh10 ni Sh3 tu (asilimia 30) inayoonekana katika mfumo ulio rasmi wa simu na benki.

“Fedha nyingi ziko mikononi mwa watu, utaona tu hata yakipatikana majanga ya moto, jengo likianguka unakuta wananchi wanalia mara mbili. Unakuta mtu anasema nilikuwa na Sh200 milioni, tujiulize kwa nini watu hawataki kupeleka fedha benki?” amehoji.

Amesema watu hawapendi kupeleka fedha benki kutokana na kodi pamoja na tozo na ameitaka Serikali kuangalia jambo hilo, ili liweze kuwaweka mahali pazuri.

Ng’enda amesema mabenki yamefikia hatua ya kuhamasisha wananchi kuweka fedha zao katika akaunti za amana maalumu (fixed deposit accounts), na kutoa riba ya hadi asilimia 15 ili kuwahamasisha kupata faida zaidi.

Vilevile, Ng’enda amezungumzia tozo mpya kwenye vichwa vya malori, akisema uamuzi wa kuweka tozo ya maendeleo ya viwanda kwa kiwango cha asilimia 10 kwenye vichwa vya malori utaongeza gharama za maisha kwa wananchi.

“Leo hii usafiri unaotoka Dar es Salaam hadi Kigoma unatozwa kilo moja kati ya Sh250 hadi Sh260, lakini kwa kuongeza kodi, mzigo huu utaongeza kufika Sh300 na zaidi. Itatokea mfumko mkubwa wa bei ambao kule Kigoma tunaushuhudia,”amesema.

Amewataka mawaziri kwenda kuangalia jambo hilo kwa kuwa halimgusi anayeagiza bidhaa pekee, bali mwananchi anayetegemea kupata manufaa kutokana na usafirishaji.

Suala hilo lilizungumzwa pia na Mbunge wa Biharamulo Magharibi (CCM), Ezra Chewelesa ambaye amemtaka Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba kumsikiliza kwa kuwa kutoza vichwa vya malori vinavyoagizwa kutoka nje ya nchi kunaenda kusababisha usafiri kuwa mgumu.

“Pamoja na kwamba tuna nia nzuri ya kuongeza mapato, hili jambo tuliangalie litaumiza Watanzania wengi kwa sababu wasafirishaji wataongeza hizi gharama na atakayezibeba ni mtu wa mwisho,” amesema.

Amesema ipo miradi inayotekelezwa na bajeti hiyo na kuwa kwa kutoza tozo hiyo kutasababisha kutotekelezeka hasa kwenye miradi ya ujenzi ambayo vifaa vingi vinasafirishwa kutoka jijini Dar es Salaam hadi mikoa ya mbali, ikiwemo Kagera ambayo ni mbali zaidi.

Chewelesa amehoji ni nani ambaye wanamlinda kwa tozo hiyo wakati Tanzania haina kiwanda cha kutengeneza vichwa hivyo mbali na viwanda vya kutengeneza matrela.

Akisoma bajeti ya Serikali kwa mwaka 2025/26, Dk Mwigulu alisema Benki Kuu imetoa mwongozo kwa watoa huduma za fedha kuhusu kushusha gharama za miamala kutoka benki kwenda mitandao ya simu na kutoka mitandao ya simu kwenda benki.

Kwa mujibu wa waziri huyo, ahueni hii itakayoanza kutumika kuanzia Julai mosi mwaka huu, gharama zinapungua kutoka Sh12,000 hadi gharama isiyozidi Sh5,000.

Aliahidi Serikali kuendelea kushirikiana na watoa huduma wote katika sekta ya fedha katika kufanya mageuzi ya kupunguza matumizi ya fedha taslimu katika uchumi.

Related Posts