Dar es Salaam. Vituo 50 vilivyo chini ya Mtandao wa Vituo vya Ubunifu Tanzania (THN) vinatarajiwa kujengewa uwezo ili viweze kuleta tija kwa wabunifu kote nchini na kuinua uchumi.
Hiyo ni baada ya Tume ya Tehama kusaini makubaliano na THN ili kuimarisha utendaji wa vituo hivyo vinavyopatikana katika mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na visiwani, ikiwa ni matunda ya tume hiyo katika kutimiza jukumu lake la kuratibu na kuhamasisha ukuaji na matumizi ya Tehama nchini, hasa katika eneo la ubunifu.
Akizungumza wakati wa kusainiwa kwa makubaliano hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Tume, Dk Nkundwe Mwasaga ameishukuru THN kwa kuamua kufanya kazi na Tume ya Tehama, hivyo kuhamasisha na kutambua mchango wa bunifu mbalimbali katika ukuaji wa uchumi wa kidijitali.
Makubaliano hayo yanakuja wakati Serikali imeweka mkazo katika kukuza uchumi wa kidijitali, na kuweka mazingira wezeshi kwa vijana, wabunifu na wajasiriamali kutumia Tehama kama kichocheo cha maendeleo.
Kupitia makubaliano hayo, Tume ya Tehama ICTC na THN wataendesha kwa pamoja shughuli mbalimbali za mafunzo, midahalo ya kitaalamu, tafiti na programu za kukuza ujuzi katika vituo vya ubunifu.
Aidha, ushirikiano huo unalenga kuhamasisha usawa wa kijinsia na ushirikishwaji wa makundi maalumu kama wanawake na vijana katika sekta ya Tehama.
Kupitia ushirikiano huu, Tume ya Tehama itaimarisha nafasi yake kama msimamizi mkuu wa sera, uratibu na uhamasishaji wa matumizi ya Tehama nchini kwa kuwa karibu zaidi na jamii ya wabunifu.
Mwenyekiti Mtendaji wa THN, Kiko Kiwanga amesema makubaliano hayo yatauwezesha mtandao wao kushirikiana kwa karibu na Serikali kung’amua na kutatua changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa kikwazo kwa vijana na wajasiriamali kuibua fursa za kiuchumi kupitia Tehama.
“Huu ni mwanzo wa ukurasa mpya kwa wabunifu nchini. Utaibua fursa mpya, kushirikisha Serikali kwenye utatuzi wa changamoto, na kuhakikisha ubunifu unakuwa chachu ya maendeleo,” amesema.