Mapendekezo ya wataalamu kuokoa afya ya jamii

Dar es Salaam. Kutokana na milipuko ya magonjwa na majanga yanayoathiri sekta ya afya kuendelea kujitokeza maeneo mbalimbali duniani, wataalamu katika sekta hiyo wamekuja na mapendekezo yatakayoonesha njia za kukabiliana na athari hizo.

Ni baada ya wataalamu hao kujifungia siku mbili katika Kongamano la 13 la Sayansi lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) lililowaleta pamoja wanasayansi, wanavyuo na watunga sera lililofanyika kuanzia Juni 18 na leo 19, 2025 kwa ajili ya kuja na mikakati ya kupambana na changamoto za sekta ya afya.

Katika siku mbili hizo, mawasilisho ya tafiti ikiwemo matumizi ya akili mnemba, teknolojia katika sekta ya afya yamewasilishwa huku kamati ikichukua kwa lengo la kufanyiwa kazi nchini.

Aidha, katika kongamano hilo tafiti, mapendekezo na mawasilisho mbalimbali ikiwemo katika afya ya mama na mtoto, maradhi ya kuambukiza na yasiyoambukiza, jinsi ya kupambana na majanga ya asili yamewasilishwa kwa ajili ya kupata njia ya kukabiliana nayo.

Akizungumza baada ya kufunga kongamano hilo, Makamu Mkuu wa Chuo cha MUHAS, Profesa Appolinary Kamuhabwa amesema tafiti zinazofanywa na chuo hicho zinalenga masuala ya magonjwa, matumizi ya dawa na mifumo ya afya.

“Matokeo ya tafiti yamewasilishwa na kamati inachukua yale yote yanayofaa kwa mfano, wizara ya afya, elimu ya juu na taasisi mbalimbali itapelekwa huko,” amesema Kamuhabwa.

Kongamano hilo lililohudhuriwa na watu zaidi ya 500 kutoka nchi 11, lilifunguliwa na Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ambaye alitaka watafiti, wataalamu na wapangaji wa sera kuwekeza kwenye tafiti zenye tija kwa Watanzania ili matokeo yake yafanye kazi kwenye utoaji wa huduma hapa nchini.

Majaliwa alisema kwa sasa sekta ya afya nchini na duniani kiujumla inakabiliwa na changamoto zenye kuhitaji mbinu mpya za kukabiliana nazo.

Akizungumza zaidi, Profesa Kamuhabwa amesema mapendekezo hayo yameangaliwa na watafiti duniani kote kwa kuwa magonjwa hayana mipaka yana uwezo wa kufika popote.

“Tumekuwa na mawasilisho 218, kikubwa asilimia kubwa ya waliotoa mawasilisho ni vijana na ni mwendelezo kwao kujikita kwenye tafiti na matumizi ya teknolojia,” amesema.

“Kuna mawasilisho ya mafunzo hata katika ngazi ya jamii kuonyesha endapo tukipata majanga tumejiandaaje. Pia tafiti za afya ya mama na mtoto na namna ya kuokoa maisha ya mtoto,” amesema.

Kongamano hilo lilikuwa na kaulimbinu isemayo:Kubadili mifumo ya afya Afrika kuweka kipaumbele katika bunifu na utafiti katika kukabiliana na changamoto zinazoendelea za afya duniani limehudhuriwa na vijana ambao wengi ni wanafunzi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya kongamano hilo, Rafael Sangeda amesema matarajio ya Serikali ni kwenda kufanyia kazi mawasilisho hayo.

Related Posts