Dar es Salaam. Wakati mabaraza ya madiwani katika halmashauri zote nchini yakitarajiwa kuvunjwa kesho Juni 20, 2025, wananchi na madiwani wametathmini miaka mitano ya mabaraza hayo kwenye maeneo yao, huku wakibainisha mafanikio na changamoto zilizobaka.
Mabaraza hayo yalianza kazi baada ya uchaguzi mkuu wa 2020 wa Rais, wabunge na madiwani na jukumu la mabaraza ya madiwani ni kusimamia miradi ya maendeleo katika halmashauri husika pamoja na masuala ya ulinzi na usalama, usafi na maendeleo ya wananchi.
Licha ya mafanikio yaliyopatikana katika maeneo mengi kama vile ujenzi wa vyumba vya madarasa, ongezeko la ukusanyaji wa mapato na ujenzi wa vituo vya afya, bado kuna changamoto zinazowakabili wananchi.
Baadhi ya changamoto hizo ni migogoro ya ardhi, upatikanaji hafifu wa mikopo kwa makundi maalumu ya wanawake, vijana na wenye ulemavu, upatikanaji wa maji safi, miundombinu mibovu na usimamizi mbovu wa mazingira.
Tangazo la kuvunjwa kwa mabaraza hayo lilitolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa aliyesema ameshasaini notisi za kuvunjwa kwa mabaraza hayo katika mamlaka za wilaya na miji.
Hatua hiyo ni mwanzo wa kuelekea kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, hivyo baada ya Juni 20, hakuna baraza litakaloruhusiwa kukaa kufanya uamuzi, madiwani wote watarudi kwenye mchakato wa uchaguzi katika vyama vyao na baadaye uchaguzi wa Taifa.
Wakizungumzia miaka mitano ya kazi, madiwani wamebainisha mafanikio na changamoto walizokutana nazo kwenye kazi zao, huku wananchi nao wakipima utendaji wao kwa kuangalia mambo yaliyofanyika na ambayo hayajafanyika.
Mkazi wa Dodoma Mjini ambaye pia ni mtaalamu wa masuala ya uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Ombeni Msuya amesema maendeleo yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano hayafichiki kwa sababu yanaonekana wazi.
Amesema pamoja na maendeleo hayo, bado kuna changamoto zinazohitaji utatuzi wa haraka kwenye baadhi ya maeneo ambayo kama hazitatuliwa kwa haraka, zinaweza kuleta shida kwa viongozi.
“Kuna changamoto za migogoro ya ardhi ambayo imekuwa ikiwakabili wananchi wengi, tunataka mamlaka husika kuhakikisha kuwa changamoto hizi zinatatuliwa kwa sababu kuna watu wanashindwa kufanya shughuli za maendeleo,” amesema Dk Msuya.
Ametaja changamoto nyingine kuwa ni miundombinu ya barabara iliyoharibiwa na mvua, akisema kuna nyingine hazijatengenezwa hadi sasa, hivyo kusababisha adha kwa wananchi kwenye shughuli zao za kiuchumi.
“Halmashauri zinatakiwa kutenga bajeti ya kukarabati miundombinu hiyo,” amesema.
Kwa upande wake, Mkazi wa Holili, Sarah Moshi amesema zipo jitihada zimefanywa na Serikali katika kutatua changamoto za miundombinu ya elimu, afya na barabara, lakini changamoto ya maji bado haijatafutiwa ufumbuzi wa kudumu.
Yohana Paul, mkazi wa Geita, amesema baadhi ya madiwani walichelewa kutekeleza majukumu yao.
“Miaka mitatu ya mwanzo walikaa kimya, kazi zimeanza miaka miwili ya mwisho wakati muda umeisha. Wengi walijisahau,” amesema.
Mkazi wa Kata ya Makurumla, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, Zainabu Kajo amesema ameridhishwa na utendaji wa madiwani na viongozi wa Serikali za mitaa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hata hivyo amebainisha changamoto zinazowakabili ikiwemo ukosefu wa mikopo ya asilimia 10 kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Diwani wa Kirongo Samanga, Wilaya ya Rombo, Prisila Shayo amesema pamoja na mambo makubwa ambayo Serikali imefanya, bado kuna kero ya uvamizi wa nyani kwenye maeneo ya wananchi.
“Changamoto kubwa ambayo haijakamilika ni uvamizi wa nyani kwenye vijiji vitatu vya Samanga, Sangasa na Kirongo Juu. Limekuwa ni jambo gumu kwetu na wananchi wanalizungumzia sana na imekuwa ni kero kwa wananchi.
Jambo hili limeshindwa kufikia utatuzi wake kwani wananchi hawa hawalimi na hawavuni chochote kwenye maeneo haya,” amesema diwani huyo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Donald Mejitii amesema pamoja na mafanikio waliyoyapata, lakini bado kuna changamoto hazijatatuliwa.
Amesema halmashauri inajitahidi kuwafikia wananchi wote kutokana na fedha zinazopatikana, lakini kuna wengine hawajafikiwa, hivyo kusababisha changamoto kuendelea kuwasumbua.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi, Idrisa Mgaza amesema kuna wakati mifumo ya Serikali ya kuruhusu fedha za miradi ya maendeleo inakataa, na wakati huo wanadaiwa na watu wanaofanya kazi na halmashauri, jambo ambalo ni changamoto.
Kwa upande wa Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, Diwani wa Mirerani, Salome Mnyawi amesema miongoni mwa changamoto alizokutana nazo kwenye uongozi wake ni baadhi ya walanguzi wa ardhi kuwauzia watu tofauti viwanja, hivyo kuibua migogoro.
Mnyawi amesema baadhi ya viongozi wenye tamaa ya ardhi waliosababisha migogoro na watu lakini akishirikiana na viongozi wa ngazi ya wilaya waliitatua.
Diwani wa Manzese, jijini Dar es Salaam, Eliam Manumbu ameweka wazi mafanikio ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) tangu mwaka 2020, akitaja miradi mikubwa ya maendeleo iliyotekelezwa, changamoto zilizokabiliwa na kiasi cha fedha kilichotolewa hadi sasa.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Charles Kazungu amesema baraza lake limewekeza kwa kiwango kikubwa kwenye sekta ya afya na elimu, kufuatia ongezeko kubwa la watu katika maeneo ya vijijini.
“Kwa kipindi hiki tumepata hospitali mbili za wilaya na shule mpya zenye vyumba vya madarasa, hatua iliyosaidia wanafunzi kusoma karibu na makazi yao badala ya kutembea umbali mrefu,” amesema Kazungu.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo ambaye pia ni Diwani wa Nyaruyoba, Habili Maseke amesema kwa miaka mitano ya uongozi wake, anajivunia kukamilisha miradi mikubwa ya maendeleo, huku halmashauri hiyo ikipata hati safi katika kipindi chote.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Donald Mejitii amesema kwa miaka mitano, halmashauri hiyo imekamilisha ujenzi wa zahanati nane na vituo vya afya vitatu ambavyo vimekuwa mkombozi kwa wananchi waliokuwa wanafuata huduma mbali.
Kuhusu ukusanyaji wa mapato ya ndani, Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Ibrahim Ngwada amesema yameongezeka kutoka Sh3.5 bilioni hadi Sh11 bilioni kwa miaka mitano, kutokana na usimamizi mzuri na uwazi kwenye ukusanyaji.
“Mapato haya yamewezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kama barabara, masoko, shule na huduma nyingine muhimu kwa jamii,” amesema.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Mkoa wa Kigoma, Kilanda Bernard ameipongeza Serikali kupitia madiwani kwa kurejeshwa mikopo ya asilimia 10 ambayo hutolewa kwa makundi mbalimbali. Hata hivyo, amesema upatikanaji bado hauridhishi ikilinganishwa na uhitaji.
“Tumekuwa tukiipata kwa asilimia kama 40 hivi, kulikuwa bado kuna ukakasi kwa sababu kuna kipindi fulani ilibidi kupata kwa makundi mpaka tulipolalamika kwa Rais, ndipo tukaanza kupewa. Kwa sasa hata mtu mmoja mmoja anapata ilimradi atimize vigezo,” amesema.
Diwani wa Mbalizi Road, Adam Simbaya amesema awali kulikuwa na changamoto ya uchakavu wa miundombinu ya sekta ya elimu ya msingi na sekondari, lakini Serikali ilikuja na suluhisho la kutenga bajeti kwa kuziboresha kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo.
“Mwaka 2020 wakati naingia, tulikuwa na shule ya msingi moja na sekondari, zikiwa katika hali mbaya, lakini nashukuru uongozi wa halmashauri ulitenga fedha kupitia mapato ya ndani na kuziboresha,” amesema.