Mwanza. Sasa ni rasmi, ndiyo maneno unayoweza kuyatumia unapoelezea hatua ya Serikali ya Tanzania kukamilisha na kuzindua Daraja la John Pombe Magufuli, lililoanza kutekelezwa Februari 2020.
Hatua ya kuzinduliwa kwa daraja hilo, kunafungua fursa ya kuanza kutumika na Rais Samia Suluhu Hassan ndiye aliyeongoza ruhusa ya magari kupita katika daraja hilo.
Daraja hilo linaloiingiza Tanzania katika historia ya kuwa na daraja refu zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kwa mujibu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), limezinduliwa leo, Alhamisi Juni 19, 2025.
Hata hivyo, uzinduzi wa daraja hilo, unakomesha huduma za vivuko katika kivuko cha Kigongo-Busisi, vilivyokuwa vikilalamikiwa kuwachelewesha wananchi kuvuka eneo hilo kwa saa moja hadi nne.
Wapo waliofika hapo saa mbili asubuhi na walivuka saa sita mchana na wakati mwingine saa 12 jioni.
Uzinduzi wa daraja hilo umefanywa na Rais Samia kwa kukata utepe na kubonyeza kitufe, kadhalika kupeperusha Bendera ya Taifa kuashiria ruhusa ya magari kuanza kulitumia.

Matukio hayo yaliambatana na shangwe za maelfu ya wananchi waliokuwapo eneo la uzinduzi, huku madereva wa magari wakipiga honi kuashiria furaha ya kuanza kutumika kwa daraja hilo.
Idadi ya watu waliokuwapo katika uzinduzi wa daraja huo, haikutofautiana na wale waliokuwepo katika viwanja vya Chuo cha Ufundi Kaluande wilayani Misungwi katika Mkoa wa Mwanza.
Rais Samia alipokewa eneo hilo la mradi saa 8:18 mchana kwa shangwe za wananchi, huku vijana wakikimbia mchaka mchaka na kuimba nyimbo mbalimbali za kizalendo.

Baada ya mkuu huyo wa nchi kupeperusha kibendera cha kuruhusu magari yapite, mara moja magari yalianza safari za kuvuka kupitia daraja hilo papo hapo.
Daraja hilo lina urefu wa kilomita 3.2, ikiwa ni la kwanza kwa urefu nchini, Afrika Mashariki na Kati, lakini linashika nafasi ya sita Afrika.
Kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Mohamed Besta kutokana na teknolojia na kiwango cha ujenzi wa daraja hilo, litadumu kwa miaka 100 kabla ya kufanyika matengenezo makubwa.
Kwa mujibu wa Tanroads, magari 12,000 yanatarajiwa kuvuka katika daraja hilo, huku zikitumika dakika nne pekee badala ya saa moja hadi tatu zilizokuwa zinatumika kupitia vivuko.

Daraja hilo ambalo upana wake ni mita 28.45 unaowezesha kupitisha magari mawili upande mmoja na mawili upande mwingine, limegharimu Sh718 bilioni fedha ambazo kwa asilimia 100 zimetolewa na Serikali.
Pia, lina njia mbili za magari zenye upana wa mita saba kila upande na njia za waenda kwa miguu kila upande yenye upana wa mita 2.5 na maegesho ya dharura yenye upana wa mita 2.5 kila upande.
Daraja hilo limepita juu ya Ziwa Victoria kuunganisha eneo la Kigongo Wilaya ya Misungwi na Busisi Wilaya ya Sengerema.
Historia ya ujenzi wa daraja hilo, inaanzia enzi za Serikali ya Awamu ya Tano, chini ya hayati John Magufuli aliyeliasisi na kuanza utekelezaji wake hadi Machi 17, 2021 alipofariki dunia.

Wakati hayati Magufuli anafariki dunia, katika Hospitali ya Mzena, Dar es Salaam utekelezaji wa mradi huo, kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, ulikuwa katika asilimia 24.6.
Machi 19, 2021, Rais Samia aliapishwa kushika wadhifa huo na kuendeleza utekelezaji wa daraja hilo hadi sasa limekamilika.
Katika moja ya ziara zake eneo la mradi huo enzi za uhai wake, hayati Magufuli alisema siku moja alipokuwa anakwenda kuposa akiwa na pikipiki yake, alifika eneo la Kigongo-Busisi na kukuta kivuko kimeharibika.
Kwa sababu hiyo, alisema alikwenda eneo ulipokuwepo mitumbwi na walimwambia aingie na pikipiki yake ili avushwe kwenda upande wa pili.
“Nikasogea pale kwenye mwalo wakanambia ingia na pikipiki yako tutaiingiza. Nikafikiria moyo ukakataa. Alikuwepo mtu na familia yake na baiskeli wakapanda.

“Mimi nikazunguka Kamanga, nilipofika Mwanza ule mtumbwi ukawa umezama na umeuwa watu 11, ndio maana nilipofanikiwa, kwanza nikawa wizara ya ujenzi, mawazo yangu yalikuwa niokoe maisha ya watu hawa ili iwe kumbukumbu kubwa kwa watu waliokuwa wanapoteza maisha hapa,” alisema.
Simulizi hiyo, imerejea tena na Rais Samia ambaye amesema ndoto ya hayati Magufuli imetimia.
Hatima ya Kivuko Kigongo-Busisi
Akizungumzia hatima ya Kivuko cha Kigongo-Busisi baada ya kukamilika kwa daraja hilo, Mkuu wa kivuko hicho wa Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa), Mboka Kibonde amesema kuanza kwa daraja hilo kunatoa fursa kwa wakala huo kuvihamisha vivuko vilivyokuwa vinatoa huduma eneo hilo.

Amesema tayari vivuko viwili vimeshapangiwa kuhamishiwa kisiwa cha Kome na Ukerewe ili kukidhi mahitaji kutokana na uhaba uliopo kwenye maeneo hayo.
Kibonde amesema hatimaye daraja hilo linahitimisha huduma za zaidi ya miongo mitano za vivuko katika eneo hilo la Kigongo-Busisi.
Kwa mujibu wa Kibonde, eneo hilo kwa kutumia vivuko walikuwa wanavusha watu 10,000 kwa nyakati zisizo na abiria wengi hadi watu 12,000 nyakati zenye abiria wengi.
“Kujengwa kwa daraja hili kutapunguza muda wa wananchi kuvuka katika eneo hili kwa sababu ukitumia daraja muda ni mchache tofauti na vivuko,” amesema.
Amesema kuna wakati inakuwa vigumu hadi kwa watu wenye dharura kuvuka eneo hilo kutokana na matumizi ya vivuko, lakini baada ya daraja watatumia dakika nne.
Kuzinduliwa kwa daraja hilo, kutarahisisha muda wa magari kuvuka kutoka upande mmoja kwenda mwingine na kuondoa usumbufu kwa abiria, kama anavyoeleza dereva wa daladala mkoani Mwanza, Maneno Mabula.
“Unafika wakati tunaacha abiria kwa sababu ya changamoto ya vivuko, abiria anafika mapema anaachwa na gari lake hajui ni lipi, lakini linapoanza kutumika linatuondolea kero,” amesema.

Dereva wa lori, Damian Nelson amesema juzi, alifika eneo hilo saa tatu asubuhi lakini hadi saa 9:00 alasiri hakuwa amepata nafasi ya kuvuka.
Lakini baada ya kuzinduliwa kwa daraja, amesema kwa sasa itakuwa rahisi kwake kuvuka kwa dakika nne hivyo kufikisha mizigo kwa haraka.