Dodoma. Vikundi 467 vilivyopewa mikopo ya asilimia 10 ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu havijaresha Sh1.2 bilioni walizopewa na Halmashauri ya jiji la Dodoma.
Wakati vikundi hivyo vikiwa havijarejesha mikopo hiyo, wanufaika wa mikopo hiyo wamesema kinachochangia kusuasua kwa urejeshaji ni waombaji kupewa fedha ndogo kuliko kiwango walichoomba.
Mikopo ambayo haijarejeshwa ni ya asilimia 10 iliyotolewa na halmashauri kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kabla ya kusitishwa Aprili 13, 2023 na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ili kupisha utaratibu mpya.
Akizungumza leo Juni 20, 2025 katika mafunzo ya vikundi 12 vilivyokidhi vigezo vya kupata mikopo hiyo itakayotolewa na Jiji la Dodoma kupitia Benki ya CRDB, Kaimu Mkurugenzi wa Jiji hilo, Joseph Fungo amesema nyuma kulikuwa na ugumu katika urejeshaji wa mikopo hiyo.
Amesema kuwa na kusuasua kwa urejeshaji wa mikopo ambapo katika Jiji la Dodoma kuna Sh1.2 bilioni wanazozidai kutokana na kusuasua kwa urejeshaji wake.
Fungo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Utoaji wa Mikopo hiyo kwenye jiji la Dodoma, amesema hata wakati mikopo hiyo imesitishwa jiji lilikuwa likitenga fedha hiyo ambapo hivi sasa wanazo Sh7 bilioni zinazotakiwa kukopeshwa kwa makundi hayo.
“Katika mwaka huu wa fedha tutaingiza Sh4 bilioni kwa ajili ya mikopo kwa makundi haya…kwenye mfumo wetu sisi vikundi ambavyo viliomba kupewa mikopo vilifikia 541,” amesema.
Amesema lengo la kuweka mchujo huo si kuwabana bali ni kuwezesha watakaopata kuzirejesha.
Fungo amesema kutokana kutokidhi masharti yaliyowekwa katika kata ni vikundi 439 ndivyo maombi yao yalikwenda kwenye halmashauri, lengo ni kuepuka mikopo chechefu.
Amesema baada ya kuviangalia walibaini vikundi 308 tu ndivyo vilivyokidhi masharti ambavyo viligawanywa katika benki mbili ikiwemo CRDB ambayo ilipelekewa maombi ya vikundi 179.
“Sasa katika vikundi hivyo wenzetu wamefanikiwa kutembelea vikundi 50 na katika mchujo ndio wamefanikiwa kuvipata 12.
Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii, Charity Sichona amesema vikundi hivyo 12 ni wanufaika wa kwanza tangu kurejeshwa kwa mikopo hiyo baada ya kusitishwa na Serikali.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo Idara ya Biashara wa CRDB Foundation, Fadhili Bushagoma amesema vikundi ambavyo havikupata mikopo vimepewa maelekezo ya kufanyia marekebisho ya kitaalamu.
Amesema vikundi vilivyobaki vitakapotimiza mafunzo kama hayo waelekee katika hatua ya kupatiwa mikopo.
“Hata vikundi ambavyo havipo hapa, kuna session ambayo itafanyika kwa ajili ya kuwapa maelekezo ya kina na waelewe changamoto iko wapi ili waweze kutatua changamoto zao,” amesema Bushagoma.
Mmoja wa wanufaika wa mikopo hiyo, kutoka kata ya Chihanga jijini Dodoma, Bahati Atanasi amesema ugumu wa kurejesha mikopo unatokana na vijana kupewa mikopo ambayo haifikii lengo walilopanga.
“Tunaiomba Serikali yetu itupatie mikopo kama tunavyoomba ili kuweza kukidhi lengo tulilolipanga kufanyia, tufanyie kazi na kurejesha kama tulivyokubaliana badala ya kuishia katika migogoro baina ya wanakikundi,” amesema.
Aprili 16, 2024 Waziri wa Nchi katika Ofisi za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa akisoma bajeti ya ofisi yake kwa mwaka 2024/25 alitangaza kurejeshwa kwa mikopo hiyo.
Alisema halmashauri 10 za majaribio ikiwemo Dodoma, zitaanza utoaji wa mikopo hiyo wakati kwa kutumia benki.
“Mikopo inayotarajiwa kutolewa ni Sh227.96 bilioni ambapo Sh63.67 bilioni ni fedha za marejesho zilizokuwa zikiendelea kukusanywa kutokana na mikopo iliyotolewa kabla ya kusitishwa,” amesema.