Mgongano wa masilahi kikwazo likizo za wanafunzi

Dar es Salaam. Wazazi, walimu na wenye shule wanatajwa kuwa chanzo cha wanafunzi kuendelea na masomo katika kipindi hiki cha likizo kinyume cha waraka uliotolewa na Serikali.

Wadau wa elimu waliozungumza na Mwananchi wamesema baadhi ya wazazi wanataka watoto wao waendelee na masomo, licha ya wengine kupinga, huku shule zikiendelea na masomo ili kukamilisha mtalaa na pia kupata fedha.

Kwa mujibu wa Waraka wa Elimu namba 3 wa Mwaka 2024 kuhusu kalenda ya mihula ya masomo kwa shule za awali, msingi na sekondari kwa mwaka 2025 siku za masomo ni 194.

Watekelezaji wametakiwa kuzingatia kalenda husika kwa ufanisi ili kuepuka changamoto ya kutokamilisha ufundishaji na ujifunzaji wa mada zote kwa wakati na hivyo kulazimika kuweka mipango ya ufundishaji na ujifunzaji inayowanyima wanafunzi fursa ya kupumzika na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii katika familia na jamii zao.

Licha ya shule kufungwa tangu Juni 6, 2025 zikitarajiwa kufunguliwa Julai 8, hivi sasa wanafunzi katika baadhi ya shule za umma na binafsi wanaendelea na masomo.

Kwa wengine ambao hawaendi shuleni, wameandaliwa programu za kazi nyumbani, ambazo huwafanya baadhi kuwa sawa na wako shuleni.

Hali hii si jambo jipya, limekuwapo kwa muda mrefu. Juni 3, 2023 akiwa bungeni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda alizionya shule kuacha kuwalazimisha watoto kubaki shuleni wakati wa likizo bila kuwashirikisha wazazi.

Alitoa kauli hiyo baada ya kuwapo malalamiko ya wazazi kwamba, watoto wanatakiwa kuendelea na masomo wakati wa likizo, huku baadhi wakitakiwa kutoa fedha kugharimia programu hizo.

Akizungumza na Mwananchi Juni 17, 2025 Mkuu wa Shule ya Msingi Moga, Leonard Ntimba amesema kutotekelezwa maelekezo ya Serikali kuhusu likizo kwa wanafunzi ni matokeo ya kutosimamiwa kwa waraka uliotolewa.

Amesema wakati mwingine hilo linafanyika kwa makusudi kwa sababu baadhi ya watekelezaji ni wamiliki wa shule na taasisi zinazotoa elimu zinazojiendesha kibiashara.

“Shule siku hizi zimekuwa biashara na baadhi ya wanaofanya hiyo biashara ndiyo wanaopaswa kusimamia sheria na miongozo inayowekwa, hapo hakuwezi kuwa na ufanisi kwenye usimamizi,” amesema na kuongeza:

“Kingine haya mabadiliko ya mitalaa yanayozungumzwa bado hayajaingia kwenye fikra za watu, badala ya kuwekeza kwenye kumfanya mtoto awe mahiri nguvu kubwa inawekwa kwenye shule kuwa ya kwanza. Kwa mtindo huu ni lazima mbinu mbalimbali zitumike kuhakikisha watoto wanafaulu bila kusahau kipindi hiki cha likizo kuna fedha inakusanywa,” amesema.

“Kwa mtalaa huu unaotaka mtoto ajifunze kwa kutenda ilikuwa sahihi zaidi aitumie likizo kujifunza kufanya vitu vingine nje ya elimu, akae nyumbani afundishwe kutunza bustani, kupika, kufanya biashara na shughuli nyingine si tena kumjazia mzigo wa kazi za darasani,” amesema.

Kwa upande wake, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Paul Loisulie amesema: “Serikali haijawahi kulisimamia hili kwa ukamilifu, kwa sababu ikiamua jambo lake haishindwi lakini kwa kuwa haijaamua kuona hili likitekelezwa ndiyo maana hadi leo tunaona wanafunzi wanakwenda shuleni wakati wa likizo.”

Dk Paul Loisulie ameongeza: “Si kwamba haiwezekani kuliondoa hili kwa sababu linafanyika kwa mazoea, watu wanaamini ili mwanafunzi afanye vizuri kwenye masomo yake ni lazima apate muda wa ziada ya ule wa darasani.”

Amesema kwa shule nyingi hilo linafanywa kwa sababu za kibiashara, walimu wanatafuta njia ya kujipatia kipato kwa sababu masomo wakati wa likizo wazazi hulipia.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo alipotafutwa na Mwananchi leo Juni 19, 2025 amesema Serikali inaendelea kusimamia maelekezo iliyotoa, ukiwamo waraka wa Kamishna wa Elimu kuhusu ratiba za muda wa masomo na vipindi katika mwaka wa masomo.

“Hili suala si kwamba hatulisimamii, ndiyo maana kuna muda maalumu mtoto anatakiwa kuwa darasani na anatakiwa pia kupata muda wa kupumzika. Kinachotokea ni baadhi ya wazazi kukubaliana na shule kwamba watoto wao waendelee na masomo,” amesema.

Profesa Nombo amesema: “Hayo makubaliano yao hatuwezi kuingilia ila tunachosisitiza shule zisilazimishe wazazi kukubaliana na mpango huo, ratiba ya mihula hupangwa vizuri kabisa, walimu wafanye kazi yao kulingana na ratiba ili inapofika likizo watoto waachwe wapumzike.”

“Hata hivyo, nimepokea taarifa hii tutaenda kufuatilia, haitakiwi walimu kuendeleza vipindi vilivyo ndani ya mtalaa katika kipindi hiki cha likizo. Kazi hiyo inapaswa kufanyika ndani ya muhula husika kwa mujibu wa ratiba ya muda wa masomo ilivyopangwa,” amesema.

Kamishna wa Elimu, Dk Lybwene Mutahabwa aliwahi kuzungumzia hilo akieleza maelekezo yanashindwa kutekelezeka, kutokana na wazazi kutaka watoto waendelee kubaki shuleni ili wapate muda mwingi wa kujisomea.

“Wazazi wengi wamekuwa wakichangia hili kuendelea, unakuta mzazi anajivunia fedha zake kwamba yuko tayari kulipia ili mtoto wake aendelee na masomo wakati wa likizo. Bahati mbaya walimu nao wanatumia udhaifu wa kutoelewa kwa wazazi, hebu badilikeni kama una hela zitumie kwa namna nyingine lakini si kulazimisha mtoto asome bila kupumzika,” alisema na kuongeza:

“Huko shuleni kwenyewe hakuna hata kitu kipya wanachofundishwa wakaelewa zaidi ya kukaririshwa na kufanyishwa mitihani iliyopita, tatizo wazazi hawaelewi ndiyo maana wanapelekwa namna hii. Ukitaka nchi ipate ukombozi wa kweli ni wazazi walioamka, kokote duniani wazazi wakiamua jambo linafanikiwa.”

Theresia Maganga, mkazi wa Mwenge jijini Dar es Salaam, ambaye ni mzazi amesema anaunga mkono shule zenye utaratibu wa watoto kusoma wakati wa likizo kwa sababu unawaepusha na mambo mengi.

“Mtaani kumeharibika hakuna mazingira mazuri kwa watoto kusoma na kujifunza, hivyo sioni tatizo wakienda shule, tena hasa madarasa ya mitihani. Ni heri wakatumie muda huko shuleni kuliko kuzurura huku mitaani, kwanza wanajiepusha na hatari nyingi zilizopo,” amesema.

Magdalena Kilufi, mama wa watoto watatu (wa kiume wawili na wa kike mmoja), mkazi wa Mbagala anasema anatamani watoto wake wakati wa likizo wabaki nyumbani kujifunza masuala ya kijamii.

“Mimi pia ni miongoni mwa wazazi wanaosukumwa na mifumo iliyopo kwenye shule nyingi kwa sasa ya watoto kuendelea na masomo wakati wa likizo, lakini natamani watumie muda huo kujifunza kazi za nyumbani, upendo kwa familia kwa maana ya kwenda kusalimia ndugu, jamaa na marafiki,” amesema.

Amesema analazimika kuwalipia masomo ili wasiwe nyuma ya wenzao wanaobaki shuleni, kwani hushindanishwa licha ya kuwa gharama huongezeka.

“Serikali ingelisimamia hili, hata malalamiko ya kuwa na mabinti au vijana wasiojua masuala ya kijamii yakiwamo ya dini, kupendana na kujua kazi za mikono yasingekuwapo. Zamani wakati wa likizo watoto wanaoishi mijini walikwenda vijijini na wa huko walikuja mijini hivyo walijifunza mambo mbalimbali, sasa hawana nafasi hiyo,” amesema.

Mwanasaikolojia Ben Mrema, anasema jamii na taasisi za elimu zinapaswa kutambua umuhimu wa likizo na kuhakikisha wanafunzi wanapata muda wa kutosha kupumzika.

Anasema mwanafunzi anapohudhuria vipindi vya darasani kila siku huchoka kimwili na kiakili na kwamba, uchovu huo ukiachwa bila kudhibitiwa huweza kudhoofisha uwezo wa mwanafunzi kuelewa na kukumbuka masomo.

Amesema kupitia likizo, mwanafunzi hupumzisha akili na mwili na hatimaye kurejea shuleni akiwa na nguvu mpya na ari ya kujifunza zaidi.

Mrema amesema likizo pia husaidia kuboresha ufanisi wa kujifunza, kwani ubongo wa binadamu hufanya kazi vyema zaidi baada ya kupumzika.

“Hali hii humwezesha mwanafunzi kutafakari kwa kina masomo aliyojifunza na kujifunza mambo mapya kwa haraka zaidi anaporejea shuleni. Kipindi hiki humsaidia mwanafunzi kupunguza msongo wa mawazo,” amesema.

Amesema shinikizo la mitihani, kazi za nyumbani na matarajio ya walimu na wazazi huweza kumchosha mwanafunzi kiakili.

“Kupitia likizo, mwanafunzi hupata nafasi ya kutuliza akili, kushughulikia hisia zake, na kurejea katika hali ya kawaida ya utulivu. Hii ndiyo sababu tunasisitiza likizo si kupoteza muda bali ni uwekezaji wa kiakili,” amesema.

Stella Msonde, mwalimu wa malezi katika shule moja ya sekondari jijini Dar es Salaam amesema kipindi cha likizo ni fursa ya mwanafunzi kukuza vipaji na stadi nyingine nje ya mazingira ya darasa.

“Mwanafunzi anaweza kutumia muda wake wa likizo kujifunza ujuzi kama vile uchoraji, upishi, uimbaji, michezo au hata kujihusisha na shughuli za kujitolea katika jamii. Vipaji hivi vinaweza kuwa sehemu ya mafanikio ya baadaye ya mwanafunzi au kusaidia kuimarisha hali yake ya kisaikolojia na kijamii,” amesema.

Amesema likizo huimarisha uhusiano wa kijamii na kifamilia kwani wanafunzi hutumia muda mwingi shuleni, mbali na familia zao.

“Likizo huwapa fursa ya kuwa karibu na wazazi, ndugu na jamaa, jambo ambalo huimarisha upendo, maadili na mshikamano wa kifamilia,” amesema.

Related Posts