Serikali yashauriwa kuweka mafungu maalumu kwa watoto

Unguja. Wakati jamii ikiwa na mitazamo hasi juu ya michezo kwa watoto ikiwemo kuwa chanzo cha kufeli masomo yao, Serikali imetoa wito kwa walimu ma wazazi kuacha mitazamo hiyo kwa sababu michezo ni njia mojawapo ya kujifunza.

Hayo yameelezwa leo Ijumaa Juni 20, 2025 na Mkurugenzi wa Idara ya Michezo na Utamaduni kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Hafsa Aboud Talib wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto Afrika yaliyoandaliwa na Shirika la ActionAid.

 Mkurugenzi huyo amesema idara hiyo ipo kwa ajili ya kuendeleza vipaji vya watoto kupitia taaluma zinatolewa shuleni na kuimarisha afya zao.

“Sasa ni wakati wa walimu na walezi kuacha dhana ya kuwa michezo ni sehemu ya kufeli masomo kwa watoto, michezo ni njia ya kujifunza hivyo wapewe nafasi ya kucheza na kuhimizwa kusoma,” amesema Hafsa

Pia, ametoa wito kwa walimu kuwapa watoto elimu ya kujikinga na udhalilishaji na unyanyasaji ili kupunguza vitendo hivyo kwa kulindana na kuwapa haki zao za msingi ikiwemo elimu,  afya bora, lishe bora na michezo.

Mratibu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa Maendeleo kutoka Shirika la ActionAid Tanzania, Tema Hassan amesema wazazi wanapaswa kuwajenga watoto katika makuzi bora kwa kuwapa nafasi ya kucheza.

Amesema michezo ni haki kwa mtoto hivyo wanatakiwa kupewa mafunzo namna ya kucheza na ipewe kipaumbele kwani michezo kwa watoto ni dawa.

Amesema, Makuzi ya mtoto yanatakiwa kuzingatia sheria na Serikali isiishe katika maneno peke yake bali iwe na mpango thabiti wa kutenga mafungu kwa ajili ya watoto.

Hivyo, amesema jamii inapaswa kutoa makuzi salama kwa mtoto kwa kupatiwa haki zao bila kikwazo chochote.

Mwalimu kutoka Skuli ya Potoa Mkoa wa Kusini Unguja, Aziza Omar Ali amesema wameandaa klabu maalumu katika shule hiyo kwa kufanya uchunguzi juu ya chagamoto wazokutana nazo na kuzitafutia ufumbuzi.

Ali amesema kupitia klabu hiyo wanatoa elimu katika masuala ya udhalilishaji na kutambua haki zao ili wanapokutana na kadhia yoyote watoe taarifa katika sehemu husika kwa lengo la kupatiwa msaada.

Mwakilishi kutoka Taasisi ya Michezo kwa Maendeleo (Mima), Riziki Abubakar Silah amesema taasisi hiyo inajishulisha na wanawake ili kuwasaidia watoto haki zao namna ya kutatua changamoto zao.

Related Posts