Serukamba akomalia urejeshwaji wa Sh900 milioni za mikopo Mafinga

Mufindi. MKuu wa Mkoa wa Iringa, Peter Serukamba ameagiza halmshauri ya Mji Mafinga kuhakikisha Sh927.2 milioni zilizotolewa kama mikopo kwa vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, zinarejeshwa ili vikundi vingine vinufaike na fedha hizo.

Serukamba ametoa kauli hiyo leo Juni 20, 2025  katika mkutano maalumu wa baraza la madiwani la halmashauri ya mji Mafinga kwa ajili ya kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi  Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha unaoishia June 30, 2024.

Amesema taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2023/2024 inaonyesha kiasi hicho cha fedha Sh927.2 milioni bado hazijarejeshwa kutoka kwenye vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu vilivyokopeshwa fedha hizo.

“Naiagiza menejimenti ya halmashauri hii ihakikishe fedha hizi zilizokopeshwa zinarejeshwa mara moja, kama vikundi hivi vilikuwa vya madiwani tushughulike navyo kwa sababu tunahitaji fedha hizo zirudi ili kuwezesha vikundi vingi zaidi kuendelea kukopeshwa kupitia mfumo huu,” amesema Serukamba.

Serukamba amemsisitiza mkurugenzi wa halmashauri ya Mji Mafinga, Fedilica Myovella kujiridha kwanza kwa waombaji wa mikopo hiyo kabla ya kutolewa kwa fedha hizo kwenye vikundi hivyo ikiwemo kumkabidhi idadi ya vikundi kwa Ofisa Usalama wa Wilaya (DSO) kumsaidia kuangalia historia ya vikundi kama vipo na shughuli ambazo wanazifanya ili kuepuka wakopaji hao kushindwa kuelejesha fedha hizo.

“Mkurugenzi unda timu ambayo itakusaidia kufuatilia fedha hizo pamoja na kukusanya mapato, utashangaa mfano manispaa ya Iringa tulikuwa tunakusanya Sh42 milioni kwa wiki lakini baada ya kuundwa kwa timu ikiwemo Polisi, Takukuru na watu wengine kwa sasa wanakusanya Sh120 milioni kwa wiki, madiwani mnadanganywa sana,” amesema Serukamba.

Pia, amesisitiza menejimenti ya halmashauri hiyo ifanye utuatiliaji wa mara kwa mara kwa wadaiwa na vikundi hivyo vinavyokopeshwa fedha za mfuko wa maendeleo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ili wadaiwa hao wafanye marejesho kwa wakati stahiki.

Kwa upande wake, mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Fedilica Myovella ameahidi kuyafanyia kazi maelekezo hayo yaliyotolewa na mkuu wa mkoa.

Myovella amesema hoja zote ambazo zilizojitokeza, atahakikisha kwa kipindi hiki cha kujibu hoja, zitasimamiwa ili ziweze kufungwa huku akisema ataendelea kusimamia ili makosa hayo yasijirudie tena.

Awali, akizungumza hoja hiyo, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa halmashauri hiyo, Elias Msuya amethibitisha kuwa bado fedha za madeni ya vikundi vilivyokopeshwa hazijarejeshwa.

“Ni kweli bado fedha zipo nje kwa vikundi ambavyo vilikopeshwa, kitu kikibwa kwa sasa ni kufuata maelekezo ambayo yametolewa na Mkuu wa Mkoa, kwamba fedha hizi ambazo tumekopesha zirejeshwe ili wahusika wengine wanufaike,” amesema Msuya.

Msuya amesema wamepokea ushauri ambao umetolewa wa kuunda timu ambayo itakuwa na uwezo zaidi wa kukusanya madeni hayo kwa kutumia vyombo vingine ili wote kwa pamoja wafanikishe kuzirejesha fedha hizo.

Related Posts