NIMR yabainisha Watanzania wengi hawajui matumizi vifurushi vya bima

Arusha. Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) imesema changamoto kubwa inayowakumba wananchi wengi baada ya kupata bima za afya ni kutofahamu matumizi sahihi ya vifurushi vinavyotolewa kupitia bima hizo.

Taasisi hiyo imesema hali hiyo husababisha wananchi wengi kuhudhuria vituo vya matibabu vya ngazi ya juu na kuandikiwa dawa za kiwango cha juu, ambazo baadaye hukosekana wanapohudhuria vituo vya afya vya ngazi ya msingi.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Taarifa za Tafiti na Mtafiti Mwandamizi wa NIMR, Dk Mary Mayige, wakati wa Kongamano la Kitaifa la Tiba linalofanyika sambamba na maadhimisho ya miaka 60 ya Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) jijini Arusha.

“Hii changamoto tuichukue kwa pamoja na tuanze sasa kufikiria nini tunafanya tunapoelekea bima ya afya kwa wote.


“Asilimia kubwa watapata bima, lakini wanajua kwamba wanatakiwa kuanzia ngazi ya msingi? Siyo kwenda ngazi ya hospitali ya Wilaya au Taifa ilhali anachoumwa kinaweza kutibiwa ngazi ya chini,” amesema Dk Mayige.

Amesema ni muhimu wananchi wafuate mnyororo wa rufaa ili kuongeza ufanisi wa huduma wanazozitoa madaktari, kwani wengi akishapata bima anakwenda ngazi za juu za huduma.

Dk Mayige ameshauri wananchi wafuate ngazi za rufaa ili kupunguza changamoto hiyo.

Amesema madaktari wengi huwahudumia wagonjwa pasipo ushauri wagonjwa.

“Tunapompa mgonjwa dawa, je alishatumia za mstari wa chini awali? Siyo unampa hiyo kisha kesho anaenda kituoni kwake anazikosa, akiambiwa hizo dawa hatuna, matibabu yake yanakwendaje?”

Akitoa mada kuelekea Bima ya Afya kwa Wote, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Dk Irene Isaka amesema mfumo tayari umeandaliwa na hivi karibuni wataanza rasmi uandikishaji na kwamba elimu zaidi itatolewa kwa Watanzania.

Chama cha Madaktari Tanzania, MAT kilipongeza kuona utekelezaji umeanza kwa hatua za awali.

Rais wa chama hicho, Dk Mugisha Nkoronko amesisitiza kuwa bado kuna kazi kubwa mbele ya kuhakikisha mpango huo unatekelezwa kikamilifu na kwa ufanisi.


“Changamoto itakuwa ni kuongeza uelewa kwa umma juu ya umuhimu wa kujiunga na bima, kuandikisha wananchi walio sekta isiyo rasmi, na kuhakikisha kuwa watoa huduma wanapata malipo stahiki kwa huduma wanazotoa kupitia mifumo ya bima bila urasimu mwingi.

“Tunatoa wito kwa wadau wote serikali, sekta binafsi, mashirika ya bima na hata sisi watoa huduma  tushirikiane kwa karibu ili lengo la bima ya afya kwa kila Mtanzania lifikiwe, ili kupunguza mzigo wa gharama kwa wagonjwa mmoja mmoja na familia,” amesema Dk Mugisha.

Akifungua kongamano hilo, Juni 18, 2025, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliliagiza kongamano hilo kujadili namna bora ya kutoa huduma za afya, hasa kuelekea Bima ya Afya kwa Wote.

“Tupeni ushauri wenu wa namna ya kutekeleza jukumu hili. Tumieni vema lengo la kukutana hapa, mwisho katika kuboresha huduma za afya nchini ninyi ni kipaumbele katika sekta ya afya,” aliagiza.

Related Posts