RC aeleza ulipo ugumu vita vya dawa za kulevya

Unguja. Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Ayoub Mohamed Mahmoud amesema kazi ya kupambana na dawa za kulevya ni ngumu kwa sababu inahusisha watu wenye uwezo kifedha na watendaji wa Serikali wasiokuwa waadilifu.

Ayoub ametoa kauli hiyo leo, Juni 21, 2025 baada ya kukamilisha matembezi ya hisani yaliyohusisha vikundi vya mazoezi 15 katika uwanja wa Maozedong, Mjini Unguja ikiwa ni shamrashamra kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kupambana na Dawa za kulevya Duniani, Juni 26, 2025.

“Kazi hii tunafahamu kuwa ni moja kati ya kazi ngumu, kwa sababu kwanza inahusisha watu wenye fedha na uwezo mkubwa wa kifedha na pili, inahusisha baadhi ya viongozi wasiokuwa na maadili. Kwa hiyo katika mazingira ya namna hiyo kazi inakuwa ngumu,” amesema Ayoub aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Idrissa Kitwana.

Amesema: “Katika ugumu huo, jukumu letu kama jamii tunapaswa kuunga mkono kuwapa taarifa na kuwafichua wanaojihusisha na uingizaji, usambazaji na uuzaji wa dawa za kulevya katika kisiwa hiki, ili kuiwezesha kazi hii ifanyike vizuri.”

Amewasihi wananchi kuendelea kuwaunga mkono na kuwapa taarifa, ili lengo la kutokomeza jambo hilo litimie.

“Mamlaka inafanya kazi kubwa na operesheni za kudhibiti na kukamata wanaojihusisha na dawa za kulevya, jitihada hizo tunaziona,” amesema

Amesema faida za kupambana na dawa hizo ni kupata vijana wenye afya na nguvu, hivyo kuongeza uzalishajimali na vipato vya jamii na Taifa kwa ujumla.

Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Shaaban Ali Othman aliyekuwa mgeni rasmi amesema bado kuna kazi kubwa ya kufanya, kwani wapo wafanyabiashara wa dawa hizo ambao hawaguswi.

“Tatizo kubwa bado hatujajitoa kushirikiana katika mapambano haya, wananchi hawajawa tayari kuwataja wahusika japo tunaishi nao kwenye maeneo yetu, ila lazima tujue tukiweka muhali katika jambo hili, badala ya kuungana na tukabaki kulalamika wanapoguswa wahusika, tutakuwa tunalea kidonda cha umauti,” amesema.

Amesema licha ya mamlaka zinazohusika kufanya kazi yake, bado zina kazi kubwa zaidi kwani biashara hizo zinafanyika kwenye jamii na wakati mwingine watu wanaona lakini hawatoi taarifa.

Kamisha Mkuu wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar, Kanali Burhani Nassoro amewatumia salamu wanaojihusisha na biashara hiyo kutafuta nyingine kwani kuendelea kuifanya wanajiweka katika hatari ya maisha.

Amesema kuna operesheni kubwa inafanyika kutokomeza janga hilo.

“Usithubutu, tafuta biashara nyingine hii ni haramu na inakufanya uishi maisha ya kutangatanga na sisi tumejipanga kuhakikisha tunatokomeza biashara hii,” amesema.

Hata hivyo, amesema kuna kazi kubwa kwani Zanzibar kulingana na mazingira yake ikiwa na bandari bubu zaidi ya 370, inahitaji ushirikiano mkubwa katika kutoa taarifa za watu wanaojihusha na dawa hizo.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (Zaeca), Ali Abdulla Ali amesema dawa za kulevya zinaathiri jamii nzima, hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuendelea kushirikiana kutoa taarifa za wanaojihusha na biashara hiyo.

“Kazi ya Zaeca ni kupambana na rushwa, hata fedha zinazotokana na dawa za kulevya ni haramu, kwa hiyo tuendelee kutoa ushirikiano kupambana na janga hili, Zanzibar bila dawa za kulevya inawezekana,” amesema.

Related Posts