Kinababa mzigo wa malezi unawahusu, wajibikeni

Dar es Salaam. Katika familia nyingi, jukumu la malezi limekuwa likiambatanishwa zaidi na mama, huku baba akiangaliwa kama mtoaji wa mahitaji.

Hata hivyo, mtazamo huu unahitaji kufanyiwa kazi, hasa katika mazingira ya sasa ambayo changamoto za kimalezi, kitabia na kijamii zimeongezeka kwa kasi.

Likizo ya shule ni kipindi cha kipekee ambacho watoto wako nyumbani muda mrefu na hivyo wanahitaji uangalizi, mwongozo na malezi ya karibu zaidi kutoka kwa wazazi wote.

Ni wakati muhimu kwa baba kushiriki kikamilifu katika malezi ya watoto wake, si tu kumsaidia mama, bali pia kutimiza wajibu wake kama mzazi mwenye dhamana ya kimalezi, kiroho na kimaadili.

Ikumbukwe kuwa baba ni mwalimu wa kwanza wa tabia na watoto hujifunza mengi kwa kuangalia na kuiga.

Baba anapojihusisha moja kwa moja na watoto wake, anakuwa mfano wa kuigwa. Watoto hujifunza nidhamu, heshima, upendo na uwajibikaji kutoka kwa baba yao. Katika kipindi cha likizo, baba anaweza kutumia muda wa ziada kuwa karibu na watoto wake, kuwafundisha kupitia mienendo yake, maneno na matendo.

Mathalani, kwa kutumia muda wake kusali pamoja na watoto, kusoma vitabu vya maadili, au kuwahimiza kushiriki kazi za nyumbani kama kusaidia majirani au kushiriki ibada, watoto hujengewa msingi wa maadili unaodumu.


Na daima katika familia bora, malezi ni jukumu la pamoja. Baba hana budi kushirikiana na mama kwa karibu kuhakikisha watoto wanapata malezi bora.

Hivyo, likizo si muda wa baba kupumzika nyumbani wakati mama anahangaika na watoto, kazi za nyumbani, au mahitaji yao.

Badala yake, baba anapaswa kushiriki kazi za kila siku kama kuandaa chakula, kusimamia usafi wa nyumba na watoto na kuhakikisha watoto wanatumia muda wao wa likizo kwa tija.

Kwa mfano, baba anaweza kupanga ratiba ya shughuli za watoto, kuwasimamia wanapofanya kazi za nyumbani au mazoezi ya kitaaluma na kuhakikisha wana muda wa kupumzika na kucheza. Hii si tu humsaidia mama, bali pia huwajengea watoto mazoea ya kupanga na kutumia muda wao kwa ufanisi mkubwa.

Wataalamu wa malezi mara zote husema kuwa wazazi wanapaswa kujenga ukaribu na watoto wao kwa kihisia.

Baba akiwa karibu na watoto wake, huzalisha uhusiano mzuri ambao huwasaidia kujiamini na kuwa na uwezo wa kufanya uamuzi wenye busara.

Wazazi mkumbuke kuwa likizo ya shule ni fursa ya dhahabu kwa baba kujenga ukaribu huu. Anaweza kutumia muda wake kucheza na watoto, kuzungumza nao kuhusu ndoto zao, changamoto wanazopitia na pia kusikiliza maoni yao bila kuwakatisha tamaa.

Baba anapokuwa rafiki kwa watoto wake, huwasaidia kuelewa dunia kwa namna salama. Anaweza kuwasaidia kutofautisha mema na mabaya.


Moja ya kazi kuu za baba pia ni kuweka mipaka inayojulikana ya kuheshimiwa. Nidhamu si ukali wa sauti au adhabu kali, bali ni kuweka utaratibu unaoeleweka ambao watoto wataufuata kwa upendo na kuelewa madhumuni yake.

Katika kipindi hiki cha likizo, watoto wako nyumbani muda mrefu, hivyo kuna uwezekano wa kujiingiza kwenye mienendo isiyofaa. Hivyo baba anapaswa kusimama imara na kuhakikisha wanawe wanazingatia maadili ya familia.

Hii inaweza kufanyika kwa kusimamia muda wa kutumia vifaa vya kidijitali, kuhimiza kushiriki ibada na kuhakikisha wanafanya kazi kwa ushirikiano.

Nidhamu ya kweli hujengwa kwa upendo, kuelewana na kuwa na mazungumzo ya wazi na ya pamoja.

Wengi huamini kwamba baba ni nguzo ya ulinzi katika familia. Watoto wanapomwona baba yao akiwa mstari wa mbele kuwalinda, kuwasikiliza na kuwapa mwongozo, hujihisi salama na kuthaminiwa.

Hivyo kipindi hiki cha likizo, watoto huwa na muda mwingi wa kuwa mitaani au nyumbani bila shughuli rasmi na hapo ndipo huweza kushawishiwa na vishawishi vya mitaani.

Baba anapaswa kuwa karibu nao kwa kufuatilia ienendo yao, marafiki wanaowasiliana nao na kuwashauri kwa busara bila ukali usio na maana.

Kwa muktadha wa sasa wa kijamii na kimazingira, ushiriki wa baba katika malezi ya watoto si hiari bali ni wajibu wa msingi.

Likizo ya shule inatoa nafasi ya kipekee kwa baba kuimarisha nafasi yake katika maisha ya watoto wake kwa kushiriki kwa vitendo kutekeleza hayo na mama.

Na kwa ushirikiano huo, baba huleta uwiano katika familia, hujenga kizazi chenye maadili na familia yenye misingi imara ya utu, heshima na uwajibikaji.

Tukumbuke kuwa malezi si maneno, ni matendo na baba ana nafasi ya kipekee ya kuonyesha hilo.

Related Posts