Rufaa ilivyomnusuru mpiga kinanda kifungo cha miaka 30 kwa ubakaji

Arusha. Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Songea, imemuachia huru aliyekuwa mpiga kinanda wa kanisa, Kenan Mduma, aliyekuwa amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela baada ya kukutwa na hatia ya kumbaka mwimba kwaya wa Ukwata aliyekuwa na umri wa miaka 14 ambaye pia alikuwa mwanafunzi.

Nakala ya hukumu haikutaja shule aliyokuwa anasoma mwathirika na  kanisa walilokuwa wakiimbia kwaya, zaidi ya kuiita kwaya ya Ukwata.

Tukio hilo lilitokea Jumamosi ya  Septemba 7, 2023 eneo la Kiuma katika kijiji cha Milonde Wilaya ya Tunduru, mkoani Ruvuma ambapo mwathirika wa tukio hilo aliyetambulishwa kwa jina la PMA alikuwa na wenzake wakifanya mazoezi ya kwaya.

Ilielezwa kuwa baada ya mazoezi kukamilika shahidi wa pili alimweleza kuwa Kenan alimtaka amsubiri, ambapo Kenan alimuomba amsaidie kupanga viti ghorofani kwa sababu kesho yake Jumapili walikuwa na wageni kanisani hapo.

PMA aliieleza Mahakama kuwa alianza kupanga viti ghafla Kenan alianza kumgusa kiuno chake na walikuwa wamebaki wawili tu kanisani hapo, ambapo alidai kuvuliwa nguo ya ndani kisha Kenan akambaka na kuwa alishindwa kupiga kelele akapiga miguu chini lakini hakusikika.

Alieleza kuwa hakusikika kwa sababu muziki uliokuwa unapigwa chini ya ngazi ulikuwa wa sauti ya juu na alipomaliza kumbaka alivua fulana yake akamfuta sehemu zake za siri kisha akaondoka.

Hukumu iliyomuachia huru Kenan imetolewa Juni 19, 2025 na James Karayemaha Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea. aliyekuwa akisikiliza rufaa hiyo ya jinai ambayo inatokana na hukumu iliyotolewa na Mahakama ya wilaya ya Tunduru.

Kupitia nakala ya hukumu iliyowekwa kwenye mtandao wa mahakama, Jaji huyo amesema upande wa mashitaka ulishindwa kuthibitisha kuwa Kenan ndiye aliyembaka PMA.

“Naona upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha kuwa mrufani ndiye aliyebaka PMA, ninakubali rufaa hii na kufuta hatia na kuweka kando adhabu naamuru mrufani aachiliwe isipokuwa kama anashikiliwa kwa sababu nyingine,” amesema.

Katika kesi ya msingi Kenan alihukumiwa katika kesi ya jinai na Mahakama ya Wilaya ya Tunduru iliyopo Tunduru, kwa kosa la ubakaji kinyume na kifungu cha 130 (1) (2) (e) na 131 (1) cha Kanuni ya Adhabu.

Shahidi wa tatu ambaye alikuwa mwalimu wa PMA na matroni, alieleza kuwa siku ya tukio kati ya saa tatu na nusu usiku alikuwa ndani ya eneo la shule PMA alimfuata akilia na kumwambia amebakwa na mpiga kinanda na kuamua kuripoti tukio hilo kwa Makamu Mkuu wa Shule, kisha wakatoa taarifa Kituo cha Polisi Matemenga.

Ilielezwa zaidi kuwa PMA ilipelekwa Hospitali ya Kiuma kwa ajili ya uchunguzi, ambapo uchunguzi ulionyesha kitu butu kilipenya.

Kenan alikamatwa Septemba 7 na kuhojiwa Septemba 8,2024  ambapo kwa mujibu wa shahidi wa sita wa Jamhuri alieleza kuwa Kenan alikiri kumbaka PMA.

Katika utetezi wake mrufani huyo aliieleza mahakama kuwa siku ya tukio alikuwa kanisani akisimamia vyombo vya muziki ila alikana kujua PMA na shahidi wa pili na kukana kumbaka.

Kutokana na ushahidi wa PMA na mashahidi wengine wa upande wa mashtaka, mahakama ya awali ilihitimisha kuwa Kenan alimbaka PMA na kumuhukumu adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela na kutakiwa kutoa Sh500,000 kama fidia kwa mwathirika wa tukio hilo.

Katika rufaa hiyo, Kenan alikuwa na sababu mbili ambazo ni kesi ya mashtaka haikuthibitishwa bila kuacha shaka yoyote na Mahakama iliyosikiliza kesi ilifanya makosa kisheria kwa kukiuka masharti ya kifungu cha 147(2) cha Sheria ya Ushahidi.

Katika rufaa hiyo aliwakilishwa na Wakili Kaukuya Yusuph huku upande wa Jamhuri ukiwakilishwa na Wakili Issa Chiputula.

Wakili Kaukuya alieleza kuwa tukio la PMA kubakwa siyo kweli kwani hakutoa taarifa kwa wanakwaya wenzake waliokuwa chini wakati wa tukio hilo, wala kwa wanafunzi wenzake waliokuwa wakimuuguza na badala yake aliwaambia anaumwa kichwa.

Alieleza kuwa  kushindwa kwa PMA kupiga kelele na badala yake kupiga miguu chini na kufika bwenini na kuoga, kwa madai hakutaka wanafunzi wenzake wasijue kilichotokea, kilithibitisha tukio siyo la kweli.

Wakili wa Jamhuri alipinga rufaa hiyo akieleza kuwa upande wa mashtaka ulithibitisha kesi hiyo pasipo shaka.

Jaji huyo amesema katika kuamua rufaa hiyo ataongozwa na kanuni kuwa lazima Mahakama hiyo ya kwanza ya rufaa itathmini upya ushahidi uliopo kwenye kumbukumbu.

Jaji amesema ni sheria kwamba ushahidi bora wa makosa ya ngono hutoka kwa mwathirika.

Amesema amezingatia kwa makini kuwa kulikuwa na ubakaji wowote uliofanywa kwa PMA na katika hilo ataongozwa na ushahidi wake na shahidi wa nne pamoja na sheria ambayo iko wazi.

“Ushahidi wa ubakaji lazima utolewe na mwathiriwa wa tukio kwani ndiye aliyeshuhudia na anajua kilichotokea na ndiye aliyehisi kilichoingizwa kwenye uke wake. Kanuni hii ilisisitizwa na Mahakama ya Rufani katika kesi za Seleman Makumba dhidi ya Jamhuri (supra),”

Jaji amesema katika kesi hii, ushahidi wa mwathiriwa ulithibitisha kwamba alibakwa, ushahidi ambao uliungwa mkono na shahidi wa nne ambaye alimchunguza na kubainisha kuwa hakuwa na birika na alikuwa akitokwa na majimaji meupe.

Jaji Karayemaha amesema kutokana na ushahidi uliotolewa na PMA ni kwamba alimfahamu mrufani kama mpiga kinanda wa kanisa na hata alipomuita kwenda kupanga naye viti hadi tukio hilo lilipotokea hakujua majina yake.

Amesema ndiyo maana kulingana na shahidi wa tatu, PMA hakumtaja jina mrufani bali alisema mpiga kinanda tu na kuwa ushahidi hauonyeshi kuwa jina la mrufani lilitajwa kwa mkuu wa shule au makamu wake, pindi  tukio hilo liliporipotiwa kwao.

Jaji amesema shahidi wa tatu alieleza akiwa ndani ya eneo la shule alifuatwa na mwanafunzi mmoja aliyemjulisha kuwa PMA analia kwani amebakwa na alipouliza nani amembaka alidai ni mpiga kinanda kanisani.

Jaji ameongeza shahidi wa sita alieleza mrufani alikamatwa siku ya tukio linalodaiwa kutokea Septemba 7,2024 siku ya Jumamosi wakati shahidi wa tatu akieleza mrufani alitambuliwa Septemba 6, 2024, jambo linaloibua maswali mengi na kudhoofisha kesi ya mashtaka kwa kiasi kikubwa.

“Uchunguzi  unaonyesha dhahiri kwamba kuna kutolingana kwa ushahidi kwenye rekodi ambao unatia shaka na haustahili kuaminiwa. Kwa jumla ninalazimika kuamini kwamba PMA hakujua ni nani aliyembaka Septemba 7,2024,”

Jaji huyo alihitimisha kuwa kutokana na dosari za kwenye ushahidi anakubaliana na mrufani kwamba mahakama ya awali ilikosea kuona kwamba mashahidi wa upande wa mashtaka walikuwa wa kuaminika na tofauti hizo zilikuwa ndogo.

Related Posts