Wahamasishwa usafi wa fukwe, ufanyaji mazoezi

Dar es Salaam. Wakati Serikali kwa kushirikiana na wadau wa mazingira wakiendelea na juhudi za kuweka mazingira safi ya fukwe za bahari ya Hindi wale wenye tabia ya uchafuzi wa fukwe hizo wametakiwa kuacha mara moja.

Ikumbukwe kulinda afya ya viumbe hai wa bahari na mifumo ya ikolojia, kudumisha sekta ya utalii na uchumi wa buluu, afya na usalama wa umma ni miongoni mwa faida za utunzaji wa fukwe za bahari.


Wakati kinyume na hapo utupaji wa taka na uchafuzi wa fukwe huhatarisha afya ya jamii na viumbe bahari kwa ujumla.

Akizungumza jana Jumamosi, Juni 21, 2025 baada ya shughuli ya usafi wa fukwe ya Dengu iliyopo Dar es Salaam ulioratibiwa na Shirika la Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF), Ofisa Mazingira wa Jiji la Dar es Salaam, Shabani Manzi amesema tusipotunza fukwe zetu pia nazo haziwezi kututunza.

Ameyasema hayo baada ya washiriki wa usafi kufanya mazoezi kwa kukimbia kilomita 10 kupitia daraja la Tanzanite ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha ufanyaji mazoezi kuboresha afya pamoja na kufanya la usafi fukweni.


Amesema utunzaji wa fukwe na kufanya mazoezi si jukumu la Serikali pekee bali kwa kushirikiana na wadau na wananchi.

Amesisitiza kwamba wanaochafua fukwe wanapaswa kutambua utunzaji wa mazingira si jukumu la Serikali ni la kila mmoja.

 “Dhumuni letu ni kubadilisha fukwe kama hii ya Dengu katika miaka miwili ijayo itakuwa na mwonekano mpya na mzuri kwa kuwa tutapanda miti na kuweka mazingira safi,” amesema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Rasilimali watu WWF, Yohana Mpagama ametoa wito kwa watu wa Dar es Salaam kutunza mazingira huku akisisitiza elimu ya utunzaji mazingira izidi kutolewa.

  “Tunaweza kukomesha tabia hii kwa kutoa elimu kwa wanajamii na kuwa na miundombinu mizuri ya kuhifadhi taka. Vilevile tunaishauri Serikali kuweka nyenzo za kuhifadhi taka maeneo ya fukweni,” amesema.

Miongoni mwa washiriki wa shughuli hiyo,  Mary Mbago amesema vijana wana nafasi kubwa ya kutunza mazingira kwa kuokota na kusafisha maeneo yote yenye taka.

Related Posts