Waandikishaji wapigakura watakiwa kuzingatia viapo | Mwananchi

Unguja. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imeanza rasmi mafunzo kwa waandikishaji wasaidizi na waendeshaji wa vifaa vya bayometriki (BVR) watakaosimamia kazi ya uandikishaji wa wapigakura katika vyuo vya mafunzo (Magereza) Zanzibar, huku wakikumbushwa kuzingatia maadili na viapo vyao wakati wa kutekeleza jukumu hilo muhimu.

Mafunzo hayo ya siku tatu yalianza Juni 22 na yanatarajiwa kuhitimishwa Juni 24, 2025, yakiwaleta pamoja jumla ya washiriki 35 kutoka Unguja na Pemba, wakiwemo waandikishaji pamoja na wataalamu wa uendeshaji wa vifaa vya bayometriki.

Lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwawezesha watendaji hao kutekeleza majukumu yao kwa weledi wakati wa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura kwa mahabusu na wafungwa ambao vifungo vyao havizidi miezi sita, ili kuwapa fursa ya kushiriki uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.

Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo mjini Unguja, Kaimu Mkurugenzi wa INEC ambaye pia ni Mkurugenzi wa Tume hiyo kwa upande wa Zanzibar, Adam Juma Mkina amesema kwa mujibu wa Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi ya mwaka 2024, kundi hilo la wapigakura litapewa fursa ya kupiga kura moja tu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Uandikishaji huu unawalenga wafungwa waliofungwa kifungo kisichozidi miezi sita na mahabusu. Shughuli  hii litaanza Juni 28 na kuendelea hadi Julai 4,2025 mwaka huu,” amesema Mkina.

Ameongeza kuwa kwa upande wa Tanzania Bara kutakuwa na vituo 130 vya uandikishaji katika vyuo vya mafunzo, huku Zanzibar ikiwa na vituo 10 vilivyogawanyika kati ya Unguja na Pemba.

Kuhusu idadi kamili ya watakaosajiliwa kwenye vituo hivyo, Mkina amesema bado haijajulikana kwa sababu hali ya Magereza hubadilika mara kwa mara kutokana na uingiaji na utokaji wa wafungwa na mahabusu. Amesema idadi kamili itapatikana baada ya kukamilika kwa uandikishaji.

Amefafanua kuwa Sheria mpya ya uchaguzi ya mwaka 2024 imeweka utaratibu utakaomruhusu mpigakura aliyesajiliwa akiwa mahabusu au gerezani kupiga kura hata akiachiwa kabla ya siku ya kupiga kura. Tume itaweka mfumo maalumu wa kurahisisha hilo.

Makamu Mwenyekiti wa INEC, Jaji mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Mbarouk Salum Mbarouk amewataka washiriki wa mafunzo hayo kuzingatia maelekezo yote wanayopewa ili kufanikisha kazi hiyo kwa ufanisi na uadilifu.

Pia amesisitiza umuhimu wa kutunza vifaa vya bayometriki walivyopewa, akisema vinapaswa kutumika kwa ufanisi ili kufanikisha azma ya kuwa na uchaguzi huru, wazi na wa haki.

Awali, wakati wa hafla ya kuwaapisha washiriki wa mafunzo hayo, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mwera, Mohamed Haji, aliwataka waandikishaji na waendeshaji wa vifaa kuheshimu viapo vyao na kuhakikisha wanafanya kazi kwa uaminifu na uadilifu mkubwa.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo, akiwemo Haji Ali Kheri, walionesha matumaini kwamba kupitia miongozo na elimu watakayoipata, watatekeleza kazi yao kwa weledi na kufanikisha kilichokusudiwa.

Related Posts