Dar es Salaam. Viongozi wa mataifa mbalimbali duniani wametoa maoni yao baada ya Marekani kujiunga rasmi na vita vya Israel dhidi ya Iran kwa kushambulia maeneo matatu ya nyuklia nchini Iran.
Hiyo ni kutokana na uvumi wa siku kadhaa kuhusu kuhusika kwa Marekani.
Marekani imevamia maeneo matatu ya nyuklia nchini Iran, hatua ambayo imechochea zaidi mgogoro wa kijeshi baina ya Israel na Iran.
Rais Donald Trump wa Marekani, katika hotuba yake aliyotoa usiku wa kuamkia leo Jumapili, Juni 22, 2025, amesema mashambulizi ya Marekani yamefuta kabisa miundombinu ya nyuklia ya Iran iliyopo Fordow, Isfahan na Natanz, huku akitishia kuendeleza mashambulizi zaidi iwapo Tehran haitachagua amani.

Iran imethibitisha kutokea kwa mashambulizi hayo, ikieleza kuwa wafanyakazi wake waliokuwa katika vituo vya nyuklia waliondolewa kabla ya mashambulizi kufanyika.
Mashambulizi ya Marekani yamekuja zaidi ya wiki moja tangu Israel ilipoanzisha yale ya kijeshi dhidi ya Iran, hatua iliyojibiwa na Iran kwa kushambulia kwa makombora, huku mamia ya wananchi wa Iran na Israel wakipoteza maisha.
Akizungumzia mzozo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, alipozungumza na umma wa nchini hiyo kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa mashambulizi hayo, ameituhumu Marekani kwa kuvunja sheria za kimataifa.
“Marekani ni mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, imekiuka kwa kiwango kikubwa Mkataba wa Umoja wa Mataifa, sheria za kimataifa, pamoja na Mkataba wa Kuzuia Kuenea kwa Silaha za Nyuklia (NPT), kwa kushambulia vituo vya nyuklia vya amani vya Iran,” amesema Araghchi na kuongeza kuwa:
“Kilichotokea asubuhi ya leo (Jumapili) ni kitendo cha kushtua na chenye madhara ya muda mrefu. Kila Taifa mwanachama wa Umoja wa Mataifa linapaswa kuchukua tahadhari na mwenendo huu hatari, wa kihalifu, usiofuata sheria.”
Amesema Iran ina haki zote za kujilinda, kulinda maslahi ya nchi yake na watu wake.

Naye Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, alipohutubia kupitia televisheni ya Israel, amempongeza Rais Trump akisema uamuzi wake wa kishujaa wa kushambulia vituo vya nyuklia vya Iran kwa nguvu kubwa, utabadilisha historia.
“Historia itakumbuka kuwa Rais Trump alichukua hatua ya kulizuia taifa hatari zaidi duniani kumiliki silaha hatari zaidi duniani.”
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, amesema:“Ninasikitishwa sana na matumizi ya nguvu yaliyofanywa na Marekani dhidi ya Iran leo.”
Amesema hiyo ni hatua hatari katika eneo ambalo tayari liko katika hali tete na ni tishio moja kwa moja kwa amani na usalama wa kimataifa.
Guterres ameyataka mataifa yote kuchukua hatua za kumaliza mvutano kwa amani na kuheshimu wajibu wao chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa.
Katika taarifa yake, kundi la Hamas limesema: “Tunalaani kwa maneno makali kabisa uchokozi wa wazi wa Marekani dhidi ya ardhi na mamlaka ya Iran.”

Taarifa hiyo imesema shambulizi hilo ni kuchochea vita hatari, ni utii wa kipofu kwa ajenda ya wavamizi na ni ukiukaji wa sheria za kimataifa.
“Tunasimama bega kwa bega na Iran, uongozi wake na watu wake, na tuna imani kuwa wataweza kujilinda,” imeeleza taarifa hiyo.
Kutoka Saudia, Wizara ya Mambo ya Nje imeandika taarifa iliyowekwa kwenye mtandao wake wa X ikielezea wasiwasi mkubwa kuhusu mashambulizi hayo.
“Ufalme wa Saudi Arabia unafuatilia kwa karibu hali ya mambo katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, hususan shambulio la Marekani dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran,” inasomeka taarifa hiyo.
Imesema nchi hiyo inatoa wito wa kuwapo kwa utulivu, kupunguza mvutano na kuitaka Marekani kuepuka kuchochea hali zaidi ya mapigano.
Pia imetoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuimarisha juhudi za kidiplomasia katika kutatua mgogoro huo kwa njia ya kisiasa.
Nchi ya Qatar nayo imeeleza hofu yake juu ya athari kubwa zitakazotokana na mashambulizi hayo ya Marekani.
“Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar inatahadharisha kuwa hali ya sasa ya hatari inaweza kusababisha maafa makubwa zaidi.
“Tunatoa wito kwa pande zote kuwa na busara, kujizuia na kuepuka kuchochea mzozo zaidi,” imeandikwa katika mtandao wa X wa Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo.

Oman, ambayo ilikuwa mpatanishi kati ya Marekani na Iran kuhusu mpango wa nyuklia, imelaani vikali mashambulizi hayo.
“Tunaeleza wasiwasi mkubwa na kulaani vikali mashambulizi ya moja kwa moja ya anga yaliyofanywa na Marekani dhidi ya maeneo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran,” limeripoti Shirika la Habari la Oman, huku Iraq ikionya kuwa mashambulizi hayo yanaweza kuathiri amani na utulivu wa eneo lote la Mashariki ya Kati.
“Mashambulizi haya ya kijeshi ni tishio kubwa kwa amani na usalama wa Mashariki ya Kati na yanaweza kuhatarisha uthabiti wa eneo hili,” amesema msemaji wa Serikali, Basim Alawadi.
Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer, ametoa wito kwa Iran kurejea kwenye mazungumzo ya kidiplomasia:
“Mpango wa nyuklia wa Iran ni tishio kubwa kwa usalama wa kimataifa. Iran haipaswi kuruhusiwa kamwe kutengeneza silaha za nyuklia, na hatua ya Marekani inalenga kupunguza tishio hilo.”
Mkuu wa Sera za Mambo ya Nje wa Umoja wa Ulaya (EU), Kaja Kallas, ametoa wito wa kuacha chokochoko na kurejea mezani kwa mazungumzo.
“Nawasihi wote kujizuia, kurejea kwenye meza ya mazungumzo, na kuzuia hali kuharibika zaidi,” ameandika katika mtandao wa X.
Hakeem Jeffries, kiongozi wa Democrat katika Bunge la Wawakilishi nchini Marekani, amesema Trump anaihatarisha Marekani kwa kuiingiza katika vita.
“Rais Trump aliidanganya nchi kuhusu nia yake, hakutafuta idhini ya Bunge kwa matumizi ya nguvu za kijeshi, na anahatarisha ushiriki wa Marekani katika vita ya maafa Mashariki ya Kati,” amesema Jeffries.
Baraza la Uhusiano wa Kiislamu Marekani (CAIR) limesema vita hiyo haina uhalali wala msingi wowote bali imetokana na mashinikizo kutoka kwa Serikali ya Israel isiyo na mwelekeo.
Lakini kundi lenye ushawishi mkubwa linaloiunga mkono Israel, la AIPAC, limepongeza mashambulizi hayo na kueleza kwamba Marekani inapaswa kushirikiana na washirika wake kuwalinda wanajeshi na maslahi yake dhidi ya mashambulizi ya Iran.
Vyombo vya habari vya Serikali ya China, kwa upande wake, vimesema Marekani inarudia makosa ya Iraq dhidi ya Iran.
“Historia imeonyesha mara kwa mara mashambulizi ya kijeshi ya Mashariki ya Kati husababisha athari zisizotabirika, migogoro ya muda mrefu na kudhoofisha uthabiti wa eneo hilo,” imeandika CGTN. Imesema suluhisho la kidiplomasia ni tumaini pekee la amani. Imelaani mashambulizi hayo, ikiyataja kuwa yasiyo na busara na hatari.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampeni ya Kimataifa ya Kutokomeza Silaha za Nyuklia (ICAN), Melissa Parke, amesema Marekani inavunja sheria za kimataifa.
Amesema mashirika ya kijasusi ya Marekani yamesema Iran haijaanza kutengeneza silaha za nyuklia, hivyo mashambulizi hayo hayana msingi wowote.
Msemaji wa Serikali ya Australia amesema: “Tumesema mara kwa mara kwamba mpango wa nyuklia na makombora wa Iran ni tishio kwa amani ya dunia. Tunachukua kwa uzito tamko la Rais wa Marekani kuwa huu ni wakati wa amani.”
Waziri wa Mambo ya Nje wa New Zealand, Winston Peters, amesema: “Hali ya kijeshi inayoendelea Mashariki ya Kati inatisha. Tunasisitiza haja ya kuepusha hali kuwa mbaya zaidi.”
“Tunasisitiza suluhisho la kudumu linapatikana zaidi kwa mazungumzo ya kidiplomasia kuliko mashambulizi ya kijeshi.”
Wizara ya Mambo ya Nje ya Mexico imezitaka pande zote kurudi kwenye meza ya mazungumzo ya amani.
“Kwa kuzingatia misingi ya kikatiba ya sera zetu za nje na msimamo wetu wa kupinga vita, tunasisitiza haja ya kupunguza mvutano,” imeandika kwenye mtandao wa X.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela, Yvan Gil, amesema: “Jamhuri ya Watu wa Venezuela inalaani vikali mashambulizi ya kijeshi yaliyofanywa na Marekani kwa ombi la Israel dhidi ya miundombinu ya nyuklia ya Iran.”
William Shao na Mashirika ya Kimataifa