Marekani ilivyotekeleza mashambulizi ya siri Iran bila kugundulika

Tehran. Swali kubwa kwa sasa ni Marekani imewezaje kushambulia vituo vya nyuklia vya Iran bila kugundulika?

Katika taarifa yake kwa umma jana Jumapili, Rais wa Marekani, Donald Trump akizungumza na waandishi wa habari Ikulu ya White House, alisema ndege zake zimeshambulia miundombinu ya nyuklia ya Iran kwa mafanikio.

Alitaja maeneo yaliyolengwa na mashambulizi hayo kuwa ni pamoja na Kinu cha Urutubishaji Nyuklia cha kilichoko maeneo ya Fordow, Natanz na Isfahan huku Iran ikithibitisha maeneo hayo kulengwa na mashambulizi hayo.

Mashambulizi hayo, siyo tu kwamba yalionekana kuishtua Iran ambayo awali, kupitia kiongozi wake mkuu, Ayattolah Ali Khamenei ilionya kuwa endapo Marekani itajiingiza kwenye mgogoro wake na Iran, basi suala hilo litageuka kuwa ‘vita kamili’.


Mashambulizi hayo ya Marekani yanatajwa kuwa ya kipekee yanayoonekana kupangwa kwa miaka mingi na kuwashangaza Iran.

Rais Trump amekuwa akifuatilia chumba maalumu maarufu kama ‘Situation room’ akifuatilia operesheni hiyo inavyotekelezwa.

Marekani ilitekeleza mashambulizi hayo kwa kutumia ndege hatari na ya kipekee inayotajwa kumilikiwa na Marekani pekee ya ‘Northrop B-2 Spirit’ ama ‘Stealth Bomber’ yenye uwezo wa kwenda kwa kasi ya kilometa 1,010 kwa saa.

Rubani wa Marekani wanaoendesha ndege hiyo walirusha mabomu yenye ujazo wa paundi 30,000 katika vituo hivyo vya kurutubisha Uranium nchini Iran vilivyoko chini ya ardhi, wakitekeleza kile ambacho viongozi wa kijeshi wa Marekani wanaamini ni pigo kubwa dhidi ya mpango wa nyuklia wa Iran.

Jitihada za Israel kushambulia miundombinu hiyo ya nyuklia ya Iran kwa siku 9 mfululizo zilikuwa zimegonga mwamba, hivyo kitendo cha Marekani kufanya hivyo kiliongeza kicheko kwa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Ntanyahu.

“Marekani imefanya kitendo cha kishujaa na kinachopaswa kupongezwa na kila mmoja ambaye anaitaka dunia kuwa mahala salama,” aliandika Netanyahu baada ya kupata taarifa za kufanikiwa operesheni hiyo.

Jeshi la Wanamaji wa Marekani lilijiimarisha, nalo lilifyatua makombora kadhaa kutoka kwenye manowari kuelekea kwenye maeneo mengine yanayotajwa kutumika kwenye mpango wa kuzalisha nyuklia Iran.


Operesheni hiyo, iliyopewa jina “Midnight Hammer”, maofisa wa Marekani walisema lilikuwa shambulio lililofanikiwa kwa kiwango kikubwa japo Marekani inadai kuwa inaendelea kufanya tathmini ya athari zake nchini Iran.

Kwa upande wake, Iran ilikanusha kuwepo uharibifu wa aina yoyote kwenye miundombinu yake huku ikaapa kulipiza kisasi.

Ndege hiyo iliondoka Marekani ikiwa na vilipuzi ikisaidiwa na ndege za kuongeza mafuta angani na ndege za kivita baadhi zikitumia silaha.

Maofisa wa Marekani walisema Iran haikugundua shambulio hilo, wala haikuweza kufyatua risasi hata moja dhidi ya ndege hizo za siri za Marekani.

Operesheni ilitegemea mbinu mbalimbali za ujanja kama chambo ili kutunza siri, kwa mujibu wa maofisa wa Marekani waliotoa taarifa saa chache baada ya mashambulizi, ambayo yalitanguliwa na siku tisa za mashambulizi ya Israel yaliyoutikisa uongozi wa kijeshi wa Iran.

Hata kabla ndege kupaa, mikakati ya kuizubaisha Iran ilikuwa imeshaanza.


Baada ya kuanza kutekeleza mpango huo wa siri, Rais Trump alianza kuuhadaa ulimwengu kana kwamba nia yake ni kuuweka mgogoro huo katika matazamio kwa lengo la kuangalia uwezekano wa kufanyika mazungumzo, huku akielewa kuwa nia yake ni kuficha mashambulizi anayoyapopanga kwa siri.

Kundi moja la ndege za B-2 lilielekea magharibi kutoka Missouri nchini humo Jumamosi kama mtego, likivuta hisia za wapiga picha wa ndege wa kiraia, maofisa wa Serikali na baadhi ya vyombo vya habari walipokuwa wakielekea kituo cha kijeshi cha Marekani katika Bahari ya Pasifiki.

Wakati huohuo, kundi lingine la ndege saba za B-2 zenye mabomu mawili ya “bunker buster” kila moja ilielekea mashariki kwa lengo la kujenga hali ya kujiamini na taswira kwamba hakuna jambo lolote linaloweza kutokea, wala kugundulika.

Mwenyekiti wa Wakuu wa Majeshi ya Marekani, Jenerali Dan Caine, akizungumza na Shirika la Habari la Associated Press alisema katika mkutano na waandishi wa habari Jumapili amesema kuwa yote hayo yalikuwa sehemu ya hadaa ili kufanikisha operesheni hiyo.

Caine alisema kuwa kwenye operesheni hiyo ilikuwa inafahamika kwa viongozi wachache wa kijeshi ili kutoruhusu taarifa kuvuja hususan huko Washington na Florida, ambako ni Makao Makuu ya Kamandi Kuu ya Kijeshi ya Marekani (Pentagon).


Baada ya saa 18 ya safari ya siri, ndege za kivita za B-2 Spirit zikiwa na marubani wawili kila moja, zilitua kwa wakati na bila kugundulika katika eneo la mashariki katika bahari ya Mediterania na kuanzisha mashambulizi yao.

Kabla ya kuingia anga ya Iran, B-2 hizo ziliandamana na ndege za kivita za siri na ndege za upelelezi za Marekani.

Ramani kutoka Pentagon ilionyesha njia ya ndege hizo ikipitia Lebanon, Syria na Iraq. Haijafahamika iwapo nchi hizo ziliarifiwa mapema kuhusu ndege hizo.

Wabunge wengi wa Marekani pia hawakuwa na taarifa, ingawa baadhi ya wabunge wa Republican walisema walipata taarifa fupi kutoka White House kabla ya mashambulizi.

Waziri wa Ulinzi, Pete Hegseth aliwaambia waandishi wa habari jana Jumapili kuwa: “B-2 zetu ziliingia na kutoka bila kujulikana.”

Takribani saa moja kabla ya B-2 kuingia Iran, Jenerali Caine alisema kuwa manowari ya Marekani ilirusha zaidi ya makombora 24 ya ‘Tomahawk’ kuelekea maeneo muhimu, likiwemo eneo la Isfahan ambako Uranium huandaliwa kwa ajili ya kurutubishwa.


Ndege hizo za Marekani zilipokaribia maeneo yanayolengwa zilichukua tahadhari dhidi ya ndege za kivita za Iran na makombora ya ardhini kwenda angani, hata hivyo hazikukutana na upinzani wowote.

Saa 12:40 jioni kwa saa ya Washington na saa 8:10 alfajiri huko Tehran, ndege ya kwanza ya B-2 ilirusha mabomu mawili ya GBU-57 yenye uwezo mkubwa wa kupenya ardhini kuelekea kituo hicho cha kurutubisha urani.

Ilikuwa ni mara ya kwanza mabomu yanayojulikana kama “bunker busters” kutumika vitani.

Eneo kubwa la Kituo cha Fordo ilishambuliwa ingawa mabomu kadhaa pia yalishushwa pia katika kituo cha kurutubisha Uranium cha Natanz.

Kwa mujibu wa Caine, mashambulizi ya mabomu ya Marekani yaliendelea kwa karibu nusu saa, huku makombora ya ‘Cruise’ kutoka kwenye manowari yakishambulia hayo kituo cha tatu cha nyuklia huko Isfahan, Caine.

Operesheni hiyo ilijumuisha; silaha 75 yakiwemo mabomu 14 aina ya GBU-57 na B-2 saba, pamoja na makombora ya cruise ya Tomahawk zaidi ya 24 kutoka manowari ya Marekan

Pia, ilihusisha ndege 125 ikiwameo ndege hatari aina ya B-2, ndege za kivita na za kuongeza mafuta angani.


Waziri Hegseth alisema jana kwamba wanajeshi ambao walifanikisha operesheni hiyo waliwasili salama nchini humo, huku ofisa mmoja wa Marekani akifichua kuwa kulikuwa na mwanamke mmoja miongoni mwa marubani wa B-2 waliotekeleza shambulizi hilo.

Jenerali Caine alisema matumizi ya mabomu ya “bunker-buster” yaliifanya operesheni hiyo kuwa ya kihistoria.

“Hili lilikuwa shambulizi kubwa zaidi la operesheni ya B-2 katika historia ya Marekani, na ni safari ya pili kwa urefu zaidi ya B-2 kuwahi kufanyika,” alisema Caine.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.

Related Posts